33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Madudu yalioibuliwa baada ya kufukuzwa wanafunzi UDOM  

necta.Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KUFUKUZWA kwa wanafunzi 7,802 wa Stashahada za Sayansi, Hisabati na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwishoni mwa Mei mwaka huu, kulizua tafrani kubwa miongoni mwa wanasiasa, wazazi na walimu.

Pia suala hili liliibua hisia tofauti miongoni mwa wasomi na wanaharakati ambao walipinga vikali uamuzi huo baada ya wanafunzi waliofukuzwa kuonekana wakiwa katika hali ngumu ya kurandaranda mjini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, wanafunzi hao walilalamika kukosa nauli ya kurudi nyumbani na wengine wakidaiwa kufanya ukahaba ili kupata fedha za kujikimu.

Awali Waziri wa Eilimu na Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alitaja sababu ya wanafunzi hao kuondolewa chuoni ni mgomo uliokuwa ukifanywa na walimu wanaowafundisha.

Kauli yake hiyo ilipingana na ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye alisema wanafunzi hao hawakuwa na sifa za kujiunga na chuo kikuu.

Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Televisheni ya ITV hivi majuzi, Profesa Ndalichako alibadili kauli yake na kusema kuwa wapo wanafunzi ambao walikuwa wakiendelea na masomo chuoni hapo huku wakiwa hawajafanya vizuri katika mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.

Anasema kuwa baada ya mgomo wa walimu na wanafunzi hao kurudishwa nyumbani, walifanya tathmini na kugundua madudu mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi.

“Baada ya kuwaondoa wale wanafunzi chuoni, nilihojiwa na kipindi cha BBC nikajibu kwamba walifaulu vizuri kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu.

“Lakini niseme tu kwamba nilikuwa sijafanya uchunguzi na kujiridhisha na taarifa nilizopewa, hivyo baada ya kupeleka faili lao Baraza la Mitihani, tumegundua kuwa wapo na daraja la nne, yaani walipata ‘division four’ lakini wamepata nafasi chuoni,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema kuwa program ile pia ilikuwa inasema kwamba ni lazima mtu awe na ‘principle’ awe amefaulu na kupata credit katika masomo yanayohitajika, lakini baada ya uchunguzi wamegundua kuwa wapo ambao hawana credit hata moja katika masomo wanayosoma.

Kwa sababu hiyo, anasema kuwa wale ambao hawana sifa hawatarejea chuoni kuendelea na masomo na kwamba Serikali haitahusika na hasara waliyoipata ya kusitisha masomo ikiwamo muda walioupoteza.

“… lakini pia labda nirudi nyuma kuangalia hii programu jinsi ilivyokuwa imepitishwa, makubaliano yalikuwa ni kwamba baada ya miaka miwili wanafunzi walitakiwa kufanya mtihani wa kidato cha sita, lakini jambo la kushangaza waliopo mwaka wa pili hakuna aliyefanya mtihani huo ambao ulifanyika Mei mwaka huu.

“Programu hii haikutekelezwa kwa mujibu wa andiko, kwahiyo kuna mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa upya, hivyo hata hawa wenye sifa kurudishwa kwao tutaangalia curriculum

(mtaala) wao ili kuona wanaostahili wataendelea na masomo kwa utaratibu upi.

“Tusingekuwa na mgomo haya yote tusingeyajua, mgomo wa walimu ndio umetufanya tuanze kufuatilia kwani hawa wanafunzi wamekujaje hapa?” anasema na kuongeza kuwa Serikali makini haiwezi kuzifumbia macho changamoto hizi hivyo ni lazima kutafuta ufumbuzi.

Profesa Ndalichako anataja suala la uandikishwaji wa wanafunzi 7,802 kwamba pia ni kinyume cha utaratibu kwani uwezo wa maabara zilizokuwapo chuoni hapo ni kuchukua wanafunzi 600 tu, huku uwezo wa walimu na madarasa yaliyopo yanaweza kukidhi wanafunzi 1080.

“Hii ni changamoto kubwa, idadi ya wanafunzi waliopaswa kuandikishwa ni ndogo kuliko wale walioandikishwa.

“Uamuzi wa kuandikisha watoto wengi kiasi hiki wa kidato cha nne ambao wanakwenda kufundishwa kwa mfumo wa mihadhara, yaani lecture haukuwa sahihi kwa kuwa uwezo na uelewa wao si mkubwa hivyo wanahitaji ukaribu wa walimu.

“Hawa wanatakiwa kukaa kwenye darasa ambalo si kubwa sana ili mwalimu anayewafundisha aweze kuwaona vizuri na kuwasaidia kwa karibu zaidi hatimaye waweze kuelewa,” anasema.

Akizungumzia suala la siku ya wanafunzi hao kurejea chuoni, alisema kuwa hawezi kusema ni lini watarudi kwa sababu matatizo yamekuwa mengi, hivyo wenye sifa watarudi lakini wanapaswa kuvumilia.

“Wasubiri tunayafanyia kazi, pengine watarudi ndani ya wiki mbili tatu tutakuwa na majibu.

Kuhusu suala la atakayewajibika na hasara iliyojitokeza tangu kuanza kwa program hii, alisema ni mapema mno kumtaja lakini waliokwenda kinyume na utaratibu watawajibika.

“Katika serikali hii ya awamu ya tano hakuna jiwe hata moja litakalobaki bila ya kugeuzwa, kila mtu aliyehusika katika hili atawajibishwa,” alisisitiza Profesa Ndalichako.

 

Kuanzishwa kwa programu

Kuanzia Novemba 2014, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilianza kupokea wanafunzi wa Stashahada Maalumu ya Elimu katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama (DE-SMICT), lengo likiwa ni kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Nne kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la walimu wa Sayansi katika shule za sekondari nchini.

Serikali iliamua kuwapeleka wanafunzi hawa UDOM badala ya vyuo vya ualimu ikiamini kwamba chuoni hapo kuna miundombinu ya kutosha hasa majengo na rasilimali watu ya kutosha kuweza kuwahifadhi, lakini mambo yameharibika ndani ya utawala wa Rais Dk.  Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles