30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MAGUFULI JIBU LA SWALI LA KATIBA LIRUDIWE

magufulliWIKI  kadhaa zilizopita tulishuhudia tukio la kihistoria pale Rais Dk. John Magufuli alipowaalika waandishi wa habari Ikulu kwa nia ya kujitathimini kwa mwaka mmoja aliofanya kazi tangu alipoapishwa kuwa Rais.

Kwanza ninampongeza Rais Magufuli kwa kutimiza mwaka mmoja kazini, lakini pia nimpongeze sana kwa kuona umuhimu wa kukutana na waandishi wa habari ambao ni wahariri wa vyombo vya habari na kuwapa fursa ya kumwuliza maswali kuhusu kipindi ambacho amekuwa madarakani.

Pengine kwa kipindi hiki pia nishukuru sana kuwa suala hili lilikuwa mubashara katika vyombo vya habari na tukapata fursa ya kuona moja kwa moja.

Sitapenda kuingia sana kuangalia maswali yote yalioulizwa na yalivyojibiwa lakini  nitaangalia baadhi ya maeneo ambayo katika upekee wake naona ni vyema kuyajadili.

Rais alijibu vizuri suala la rushwa na mafisadi kuwa pamoja na kuwa Mahakama ya mafisadi kama inavyotajwa imeanza kufanya kazi, rushwa ni suala mtambuka na haliwezi kushughulikwa na Rais peke yake.

Nilibahatika pia kusikia swali lililoulizwa kuhusu mchakato wa Katiba mpya kuwa umefikia wapi. Nilisikiliza jibu kwa makini sana kwani suala hili kwa upande wangu na wenzangu wengi ni muhimu sana na jibu la Rais lingetusaidia kutoa mwelekeo kwani ni muda mrefu sasa umepita tangu mchakato uwe kimya na hatuna majibu ya moja kwa moja kuhusu hatima yake.

Rais alijibu kwa kusema kuwa katika kampeni aliyoifanya wakati akitafuta kuwa Rais hakuna sehemu yoyote ambayo alizungumzia suala la Katiba mpya.

Hata hivyo, akasema suala la Katiba mpya limefikia pazuri. Na hatimaye akasema “niacheni kwanza ninyooshe nchi”.

Hili jibu katika utatu wake linahitaji kuangaliwa na kuhojiwa ili kupata maana yake kwetu tulio wadau wa kupata Katiba mpya.

Rais alitaja hata kiasi cha kilomita alizotembea wakati wa kampeni na kuwa katika umbali wote huo hakutaja suala la Katiba mpya.

Huenda ni kweli kwa vile sikufuatilia mikutano yote aliyokuwepo Rais alipokuwa katika kampeni. Ninachofahamu ni kuwa Rais Magufuli alikuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwa katika kampeni zake hasa zile nilizobahatika kumsikiliza hakutaja sana ilani ya chama chake.

Lakini baada ya kuwa Rais nimemsikia akisema anatekeleza Ilani ya CCM. Ni kweli asingeweza kutaja yale yote yaliyokuwa katika ilani ile, ila ndio anayoitekeleza. Niliposikia jibu hili, nilirejea ilani ya CCM na  nilikuta sehemu yenye kichwa cha habari: UTAWALA BORA, DEMOKRASIA  NA UWAJIBIKAJI.

Kichwa hiki kipo ukurasa wa 163 wa Ilani hiyo. Kifungu cha 144 kinaelezea mafanikio ya CCM katika kutekeleza  kichwa hicho cha habari. Moja ya mafanikio ni katika kifungu cha 144 (e) kinachosomeka “mchakato wa kutunga Katiba mpya umeendeshwa na umefikia hatua ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, ambayo itapigiwa kura ya maoni ya wananchi”.

Kifungu cha 145 cha ilani hiyo ya CCM kinaelekeza yatakayofanyika iwapo watashinda uchaguzi ambayo mojawapo ni katika kifungu cha 145(g) kinachosema “kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuutekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba”.

Kwa mujibu wa ilani hii mchakato ulifikia kupigiwa kura ya maoni na serikali iliyopo madarakani sasa inatakiwa kwa mujibu wa ilani hii kukamilisha mchakato na kuanza kuitekeleza.

Rais aliposema kuwa mchakato sasa upo mahali pazuri nilitaka kuamini kuwa kura hiyo ya maoni inatarajiwa kupigwa hivi karibuni. Sentensi iliyofuata haikuonyesha hivyo hasa pale aliposema aachiwe ainyooshe nchi.  Sentensi hii ikiunganishwa na ile ya kwanza ya zile kilomita ambazo hakuiongelea hiyo Katiba inaonyesha kuwa suala hilo si kipaumbele kwa Rais.

Ningependa kushauri tu kuwa ni vyema kabisa Rais aachiwe ainyooshe nchi kwa vile ni kweli kabisa kuwa ilikuwa imepinda. Lakini kama alivyosema katika suala la kupambana na mafisadi na hata suala la maadili, kazi hizi si za Rais peke yake.

Ili aweze kuinyoosha hii nchi na ibaki imenyooka hata yeye atakapomaliza muda wake, suala la Katiba inabidi liwe kipaumbele kwani si yeye wala sisi tunaoweza kuiweka nchi hii katika hali ya kunyooka kwa matamshi na kufuatilia hili au lile bila kuwa na mifumo thabiti ya kikatiba na kisheria.

Kilio cha uwepo wa Katiba mpya nchini kilianza, miaka mingi iliyopita kwa vile ilikuwa wazi kuwa pamoja na kuwa tuna Katiba haijaweza kusaidia kutibu mambo mengi yanayotokea nchini na hivyo tukiwa na Katiba nzuri itakayojengwa na wananchi wenyewe basi mengi ya yale yaliyopinda yatanyooshwa na nchi itaweza kwenda katika misingi hii inayotajwa katika ilani ya CCM ya kuwa na Utawala Bora, Demokrasia na Uwajibikaji.

Rais wetu asidhani hali ilivyo inaweza kubadilika kwa ufuatiliaji binafsi tu. Hata kilio cha Rais cha kuwasaidia wanyonge hakitakamilika bila kuwa na Katiba itakayodhibiti mambo yanayoendeleza  umasikini kwa wengi wa watu wakati wachache wakijinufaisha.

Inabidi hapa tuunganishe suala la Katiba mpya na maendeleo ya watu na Katiba na vita dhidi ya ufisadi na rushwa. Kwa vile nililisikia hili jibu, ninadhani Rais anapaswa aangalie kwa upya suala hili kwani ni msingi mkubwa sana utakaomwezesha Rais na serikali anayoiongoza iweze kufanya kwa wepesi na kwa mafanikio makubwa yale yote yaliyo katika ilani lakini yale mengi Rais aliyoyatamka wakati wa kampeni.

Msingi mkuu wa hili ni kuwa litakuwa jambo endelevu kwani Rais anaweza kapambana kweli  kuinyoosha hii nchi na kwa kukosa misingi ya kikatiba nguvu zake zikaishia pale utawala wake utakapoishia na akaja mwingine akaturejesha tulikotoka au pabaya zaidi. Katiba ni suala la msingi na mchakato wa Katiba mpya ni la uharaka.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles