Na WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolijia, Dk. Ashatu Kijaji, leo Jumatatu Oktoba 25, 2021, amekutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari, huku akiahidi kushughulikia changamoto zilizopo katika tasnia hiyo.
Amesema wizara yake inatambua changaomoto zote, zitafanyiwa kazi kwa maslahi ya pande zote na hakuna atakayeumizwa.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam, wahariri wametoa maoni na maombi mbalimbali wanayotaka kushughulikiwa ili kufanya kazi kwenye mazingira mazuri tofauti na sasa.
Akizungumza katika mkutano huo Dk. Kijaji amesema anataka kufanya kazi kwa pamoja na Wanahabari ili kumdhihirishia Rais Samia Suluhu mchango wa sekta hiyo.
Waziri huyo amesema lengo la kuitisha mkutano huo ni kujitambulisha yeye pamoja uongozi mzima wa wizara hiyo na kuwashirikisha waandishi wa habari mambo mbalimbali kuelekea sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
“Tupo tayari kupokea maoni ya changamoto za waandishi wa habari na kuzifanyia kazi, zitashughulikiwa kwa maslahi ya pande zote mbili na hakuna atakayeumizwa.
“Namhakikishia Mheshimiwa Rais utendaji uliotukuka, namshukuru kwa kuniamini na napenda kuwahakikishia ushirikiano mwema,” amesema Dk. Kijaji.
Ameeleza kuwa Serikali inathamini na kutambua mchango wa sekta ya habari, ndiyo sababu imefanyia kazi kwa haraka ombi la kuhamishwa wizara ndani ya miezi miwili.
Katika hatua nyingine Dk Kijaji, ameviomba vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuelemisha jamii kuhusu chanjo ya Uviko-19.
Pia ameaomba ushirikiano vyombo vya habari katika kutangaza sherehe za Uhuru na matukio yote ili wale wasiokuwepo kipindi hicho waweze kufahamu historia nzima.
“Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama atakutana na vyombo vya Habari kutoa ratiba ya maadhimisho hayo, naomba tujipange tutangaze shughuli za maadhimisho haya,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza wizara hiyo kuonesha muelekeo wa kutatua kero za sekta ya habari kwa muda mfupi.
“Wanahabari tufanye kazi kitaaluma, lengo kubwa la kukutana leo ni kufahamiana na wizara, tunaomba kuiunga mkono,” amesema Balile.