ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amesema ana wasiwasi na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kama watamuelewa kuhusu kumaliza kabisa tatizo la rushwa ndani ya chama hicho.
Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa Dodoma hivi karibuni.
“Katika awamu hii tumefanikiwa kupunguza tatizo la rushwa lakini bado ipo, sisi tunatamani sana rushwa ipotee kabisa lakini sidhani kama Polisi au Takukuru watanielewa! Sijui…kwa sababu pale ndio kuna mkate wao,”alisema Dk. Bashiru.
Dk. Bashiru ambaye pia alizindua vyombo vipya vya bendi ya chama hicho ya TOT, aliutaka uongozi wa bendi hiyo kutunga nyimbo ambazo zitaelimisha jamii kuhusu tatizo la rushwa.
Dk. Bashiru akizungumzia nidhamu kwa watumishi wa umma na rushwa alisema kuna mabaki ya watumishi wasiojali na wasiokuwa na usikivu na kuwataka TOT kufanyia kazi kampeni hiyo ya kuelimisha.
Kuhusu maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, alisema pamoja na mambo mengine wamekubaliana namna ya kuimarisha mashina ya CCM nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha inaonekana na kuwafikia wananchi.
“Tayari naibu katibu mkuu wetu bara (Rodrick Mpogolo), ameagiza kufanyika mafunzo kuanzia kwenye mashina kutoa elimu kuhusu chama chetu ikiwa ni pamoja na katiba yetu ya chama na historia kwa sababu wanachama wetu wengi uelewa wao kuhusu chama ni mdogo,”alisema.
Alisema katika eneo la ubunifu wa miradi ya chama hawajafanya vizuri hivyo watafanya namna ya kubuni ili wajitegemee.
Vilevile alisema chama hicho, hakina bajeti ya kununua sare za wanachama na kutaka kila mmoja ajinunulie yake.
“Kila mwananchama anunue mavazi kama ni mkulima wa korosho tenga bajeti yako kwa ajili ya sare ili mwaka ujao nchi yote iwe kijani, chama hatuna mpango wa kununua sare za wanachama isipokuwa tutaziuza kwa bei nafuu,”alisema.
Alisema mkakati wa tatu ambao Kamati Kuu ya CCM imeazimia ni upande wa sanaa, michezo na utamaduni ambapo bendi ya TOT watatakiwa kuwa wabunifu kwa kutunga nyimbo mpya za kuhamasisha.
“Lazima muwe wabunifu, kuna wimbo nausikia huo huo kila siku ni huo mmoja, sasa mbadilishe vinginevyo kina Harmonize watawaondoa mchana kweupe,”alisema.
Alisema mkakati wa nne ni taarifa za wanachama na mali za CCM kusajiliwa kwa mfumo wa kisasa wa kieletroniki.
“Tutakuwa tunasajili bila kujali umelipia au hujalipia lakini baada ya kusajiliwa ile kadi ndio utalipia mpaka sasa tumesajili wananchama milioni 1.5 na hadi Februari mwakani wanachama wote watakuwa wameingizwa kwenye mfumo huo,”alisema Dk. Bashiru.
Pia aliwataka makatibu waenezi ngazi zote kuanzisha madarasa ya itikadi kwa kuemilisha wananchama kuhusu katiba ya chama hicho na historia.