Na Balinagwe Mwambungu
NIMEFUATILIA mjadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu siasa na dini, nimebaki kujiuliza hivi unachora mstari gani, mnene au mwembamba wa kutenganisha mambo haya mawili?
Tumezoea tangu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere na awamu ya nne, tukiwaona viongozi wa dini wakiwaalika wanasiasa na viongozi wa kisiasa wakiwaalika viongozi wa dini katika shughuli mbalimbali za kisiasa na kidini.
Jambo la kushangaza sasa hivi tunaona viongozi wa dini wakiandamwa na wanasiasa kwamba wanachanganya dini na siasa.
Kuna watu wanataka kuwaaminisha Watanzania kwamba viongozi wa dini wanapoonya kuwa wananchi wanajengewa hofu, wanaingilia mambo ya kisias, au viongozi wa dini wanapoitaka Serikali itoe tamko kuhusu mauaji, kutekwa watu na kupigwa risasi mchana kweupe kwa kiongozi mashuhuri wa upinzani na Serikali kukaa kimya, ni kuchanganya siasa na dini.
Hofu wanayoizungumzia viongozi wa dini inatokana na taarifa za maiti za watu kuopolewa Mto Ruvu, Bagamoyo, miili ya watu iliyofungwa kwenye viroba na kuokotwa ufukweni, Dar es Salaam, mauaji yaliyokuwa yanaendeshwa na watu wasiojulikana kule Mkuranga na Kibiti mkoani Pwani, yameleta hofu katika jamii na kuitaka Serikali itoe maelezo ya kina, ili kuwaweka wananchi sawa na kuwaondolea hofu, ni jambo ambalo viongozi wa dini hawapaswi kulisema.
Hata hivyo, hilo haliondoi ukweli kwamba mauaji yale yaliyofanywa yameleta hofu, si kwa wakazi wa maeneo hayo tu, bali nchi nzima. Maaskofu wanapozungumza kuwa wananchi wamejazwa hofu, wanaambiwa hayo ni mambo ya kisiasa, hayapaswi kuzungumziwa kwenye nyumba za ibada! Hakuna mwanasiasa aliyepanda jukwaani na kuyasema haya. Nani sasa ayaseme!
Wanasiasa waliowashambulia maaskofu, hawakufanya ‘home work’ yao vizuri. Miaka yote, kama kumekuwapo mahusiano mazuri na mashauriano, tena katika ngazi za juu kabisa, kati ya viongozi wa dini na Serikali na hatukuwahi kusikia kuna migongano ya pande hizi mbili.
Viongozi wa dini walikuwa na uhusiano wa moja kwa moja, bila urasimu na waliruhusiwa kumpa Rais ushauri katika kutafuta mustakabali wa nchi. Katiba pia inatamka kwamba mtu yeyote anaweza kumpa ushauri mkuu wa nchi ama kwa kuombwa au kujitolea, ila si lazima Rais akubaliane na ushauri huo, aidha, Katiba haijatamka ushauri huo unapaswa kutolewa kwa njia gani.
Ushauri unaweza kuwa mbaya au mzuri, inategemea anayeshauriwa anaupokeaje na kuutafsiri vipi. Katika Biblia tunasoma kwamba Mfalme Herode alipata taarifa za kuzaliwa Mfalme (Yesu), washauri wake wakatafsiri kuwa mtoto huyo atanyang’anya ufalme wake. Herode akaamuru watoto wote wa kiume waliokuwa chini ya miezi mitano, wauawe. Hii ni kwa sababu washauri na yeye mwenyewe Herode, hawakuweza kufanya uchambuzi wa habari ile.
Wanaowashambulia viongozi wa dini ninawafananisha na Mtawala Herode, wanafikiria nafasi za siasa walizonazo, kuwa watazipoteza. Herode alimwona Yesu, angemnyang’anya nafasi yake ya ufalme. Ufalme uliokuwa unatamkwa haukuhusu ulfame wa hapa duniani.
Viongozi wa dini hawatafuti utukufu, wala nafasi au vyeo vya kiserikali, wanayasema mapungufu wanayoyaona katika jamii na uongozi na ni wajibu wao kuyasema, kwa sababu wao ni viongozi wa kijamii na ni sehemu ya jamii.
Kuna kiongozi mmoja anasema, viongozi wa dini hawaruhusiwi kuikosoa Serikali, ila wanaruhusiwa kuisifu! Hii ni sawa na kuwafanya viongozi miungu watu wa kupewa sifa. Mungu pekee anayestahili sifa, lakini hata yeye watu wanamkosea, tena wengine humwaasi kabisa!
Wananchi wasitegemee kuwapo kwa amani bila ushiriki wao, wasiwategemee viongozi tu, wanao mchango mkubwa katika kudumisha amani. Chimbuko la amani katika nchi yetu, halitokani na chama fulani, wala si kwa wananchi kufanyakazi halali pekee, bali Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki na mipango ya kuwawezesha wananchi hasa  vijana, kufanya kazi. Kundi kubwa katika nchi kama lina njaa, amani hutoweka. Angalia yanayotokea Iran hivi sasa, wananchi wanasema kila kitu kinapatikana nchini mwao, lakini hawana uwezo wa kuvinunua, bei hazikamatiki.
Viongozi wa dini nchini wanazungumzia ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na haki za binadamu (katika upana wake), wanasiasa wanasema huo si uwanja wao, wanaingilia mambo ya kisiasa!
Viongozi kuambiwa kwa kuwa wanaapa kuitii na kuilinda Katiba ya nchi, halafu wanakwenda kinyume, wakikumbushwa wanasema hayo ni mambo ya siasa! Inashangaza sana. Wanasiasa waache kutumia misahafu wanapoapishwa, kwa kuwa kunaleta mwingiliano wa dini na siasa. Kusema kuwa maudhui haya kuwa na staha, matusi si sehemu ya msamiati wa waongofu.
Kiongozi wa kidini anapowaambia viongozi watubu, si siasa. Wanatamka hayo kwa mamlaka waliyopewa kutoka juu. Mbona viongozi wanakwenda misikitini na makanisani kwa ajili ya ibada ya toba, lakini hata huko viongozi wa kisiasa, wanajua kuwa si uwanja wa siasa, lakini hutamka mambo ya kisiasa.
Tutafakari nafasi ya viongozi wa kisiasa na wa kidini, kila mmoja wao ana nafasi yake. Viongozi wa kidini ni sehemu ya jamii na Serikali inapokwenda ndivyo sivyo, wao ndio vipasa sauti vya jamii. Hakuna mstari mwembamba au mnene wa kutenganisha dini na siasa. Ndivyo ilivyo.
Naomba kuwasilisha.