23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DK. KAHANGWA: SIWEZI KWENDA CCM, HAITAKI KATIBA MPYA


Na EVANS MAGEGE

KWA wafuatiliaji wa siasa za mageuzi nchini wanamfahamu vema, Dk. George Kahangwa, ambaye amepata kushiriki siasa za vyama vingi takribani miaka 22.

Mbali na mambo ya kisiasa, Dk. Kahangwa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Katika ulingo wa siasa amewahi kutia nia ya kuwania urais kupitia NCCR- Mageuzi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Hata hivyo, ndoto yake ilizimwa baada ya chama hicho kutomsimamisha mgombea wa nafasi hiyo.

Hivi karibuni Dk. Kahangwa ametangaza  kuachana na shughuli za siasa, uamuzi huo umeacha maswali mengi ambayo gazeti hili linakupatia majibu kupitia mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi.

Endelea kufuatilia mahojiano haya…

MTANZANIA Jumapili: NCCR –Mageuzi kilikuwa chama kikuu cha upinzani, chanzo cha kuporomoka ni nini?

Dk. Kahangwa: Swali lako zuri, kuanzia miaka ya 1990, NCCR –Mageuzi kilikuwa chama kikuu cha upinzani na baadaye kikaanza kushuka. Kuna vitu vingi unaweza kuangalia kwa mfano matokeo ya hivi karibuni ya chaguzi  ndogo.

Pia ndani ya chama kuna matatizo mengi ambayo Watanzania walioko nje ya chama hawayaoni.

MTANZANIA Jumapili: Ni vema ukaufahamisha umma matatizo hayo ni yapi.

Dk. Kahangwa: Naweza kutolea mfano wa kuangalia malengo ya chama, chama chochote cha siasa kina safari ya kushika dola na kutawala kwa maana ya kuongoza nchi.

Sasa unapokuwa na chama ambacho kimepoteza mwelekeo na hakifanyi jitihada za kujijenga kitaifa, hata kugombea kwenye nafasi za wazi ni kwa mbinde, kumbuka kulikuwa na kata 43 zilizokuwa zinagombewa NCCR-Mageuzi kilisimamisha mgombea mmoja tu kati ya kata 43, naye aliambulia kura tatu tu, unaweza kujiuliza kwamba chama kina matawi na bila shaka katika kata hiyo kuna tawi la chama, na kawaida tawi huwa halina pungufu ya wanachama kumi, sasa inakuwaje mgombea anapata kura tatu? Hapo ndipo unagundua kuwa kuna udhaifu ndani ya chama, ingawa vinaweza kuwapo visingizio vingi vya kuibiwa na kadhalika.

Na kwa mambo yalivyo ndani ya NCCR –Mageuzi, hata yule mgombea hakuwa na uungwaji mkono na chama, kuanzia ngazi ya taifa kana kwamba hawakutaka awanie nafasi hiyo.

Haya yamekuwa yanatokea na hata sasa kuna uchaguzi mdogo wa majimbo na kata, kuna kata moja ambayo amepatikana mgombea kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, lakini ameambiwa na viongozi wakuu atoe jina lake sababu hazieleweki, ingawa kuna vyama vimesema vinaondoa wagombea wao kwa sababu mbalimbali lakini hizo si sababu za ndani ya NCCR- Mageuzi.

Kuna shida nyingine, unafahamu chama kina mbunge mmoja kinapata ruzuku ndogo na wanachama wanachangia ada kwa hiyo chama kina udhaifu kidogo wa mapato.

Sasa mnapokuwa na udhaifu wa mapato lazima matumizi yenu yafanywe kwa akili sana, lakini inastaajabisha wafanyakazi wa ndani ya chama wanaomba msaada wa fedha mara kwa mara ukiuliza wanasema hawajalipwa mshahara wakati chama kinapata ruzuku.

Niliwahi kuchukua hatua ya kuwauliza baadhi ya viongozi sababu za kutowalipa mishahara wafanyakazi, wakadai kuwa jambo hilo halina ukweli wafanyakazi wamelipwa mishahara yao. Huenda baadhi ya viongozi ndani ya chama wanajua kuwa fedha zimetoka kwa ajili ya kuwapa posho watumishi zimeishia kwa nani, hii ni shida kubwa.

Wakati vyama hivi tunavyozungumza kuwa ni vya upinzani vina ajenda kubwa ya ufisadi angalia aina ya matatizo yaliyomo ndani ya vyama hivyo. Kwamba kuna watu wako ndani ya hivi vyama kazi yao ndiyo hiyo.

Najua kuna shida nyingi na nyingine zimenihusu hata mimi binafsi. 

MTANZANIA Jumapili: Chanzo cha hayo yote ni nini?

Dk. Kahangwa: Sababu kubwa ni unafiki miongoni mwa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia malengo ya chama.

Kwa kuwa wamepewa nguvu na wanachama, wanachokiamini wao ndicho wanachokifanya, wanapokosa uadilifu na chama kinaugua ugonjwa huo huo na ndiyo maana hata ilipotokea misuguano wengi waliokiasisi chama wakakikimbia. Laiti kama chama kikipata uongozi sahihi mambo yanaweza kueleweka.

MTANZANIA Jumapili: Kama mwanasiasa msomi kwanini usingetumia nafasi yako kutatua matatizo hayo.

Dk. Kahangwa: Swali zuri kabisa, ukweli ni kwamba mimi nisingeweza kutafuta mwanga ndani ya chama, kama kushauri  nimeshauri kwa miaka mingi lakini kwa sababu sikuwa mwenye mamlaka ya maamuzi, si  kiongozi wa juu hakuna kilichobadilika.

Na ukizingatia mimi mtumishi wa umma siwezi kugombea uongozi, kwa kanuni na sheria za nchi naruhusiwa kuishia kwenye ngazi ya kuwa mwanachama tu.

MTANZANIA Jumapili: Unapozungumzia uongozi ni suala pana kwa maana ya kuwa kuna mwenyekiti, makatibu na kadhalika, hapo unamlenga nani kama kiranja mkuu?

Dk. Kahangwa: Labda niseme kwa hili ni uwajibikaji wa pamoja kwa viongozi wote wakuu wa chama, hata kikatiba chama na vyama vingine vya siasa, hakuna kilichoamua kuwa na kiongozi mmoja.

NCCR-Mageuzi ina viongozi wakuu saba, miongoni mwao wapo wanaoweza kuwa wahusika wakuu wa matatizo yanayoendelea ndani ya chama.

Kwa mfano nilipozungumzia suala la watumishi kutopata mishahara yao, anayehusika kuhakikisha watumishi hao wanapata stahiki zao yumo kati ya viongozi hao na kama kaidhinisha fedha zikatoka benki basi anapaswa kujua zilikokwenda.

Kama nikisema uongozi una udhaifu wa kutofanya siasa za kukijenga chama, wajenzi wenyewe ni hao hao viongozi.

Nikisema kuwa chama kinakataza watu kuwania ubunge au udiwani wanaokataza ni miongoni mwa hao hao viongozi. Kwa hiyo kama mmoja akiandika waraka wa kumwambia mgombea fulani ajitoe kwenye kinyang’anyiro bila sababu, halafu viongozi wanashindwa kumkosoa basi hilo ni tatizo.

MTANZANIA Jumapili: Ndoto yako ya kuwania urais mwaka 2015 ilizimikaje?

Dk. Kahangwa: Kwanza nieleze kitu kinachoweza kuwasaidia Watanzania kujua ukweli. Neno sahihi la kutumia kuhusu mimi ni kwamba, nilikuwa mtia nia ya kuwania urais lakini sikuwahi kugombea urais.

Suala hilo lilitokana nilipozungumza na baadhi ya vijana wakasema wanahitaji kuwa na mgombea mwenye mtazamo tofauti kupitia chama chetu na wakanifikiria mimi.

Tulikubaliana wakanichukulie fomu na walifanya hivyo, lakini fomu hiyo haikuwahi kupata heshima stahiki ya chama. Kwa hiyo tabia ya kuzuia watu wasigombee hata mimi wakati ule ilitumika kwa sababu chama hakikuwahi kupitisha jina langu kugombea.

Kwa hiyo watu wanaosema nilipendekezwa miongoni mwa wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi- Ukawa, nasema maelezo hayo si sahihi kwa sababu sikuwahi kupendekezwa na chama kuwa mgombea urais.

MTANZANIA Jumapili: Tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 umalizike umekuwa kimya, siri ya ukimya wako ni nini na kwanini chama hakikupitisha jina lako kwenye uchaguzi ule?

Dk. Kahangwa: Vijana walionichukulia fomu waliambiwa chama hakikuwa na fedha ya kuitisha mkutano mkuu ambao ndio ulikuwa na mamlaka ya kunipitisha kugombea.

Waliambiwa hakuna mjadala wa kupitisha mgombea urais wa chama, sasa ndio ujue kuwa inawezekana huo ndio udhaifu wa chama chenyewe.

Hapakuwa na jina lolote la mtia nia ya urais lililokwenda kwenye majadiliano ya Ukawa, upande wa Ukawa kwa maana ya Chadema na CUF walikuwa wanajua kuna mtu upande wa NCCR-Mageuzi  anatajwa kuwania urais. Wakati ule nilipokutana na Profesa Ibrahim Lipumba na Dk. Wilbrod Slaa, mimi sikuwa na hadhi ya kukiwakilisha chama kwenye mjadala huo ingawa Profesa Lipumba na Dk. Slaa, walikuwa wanajua kuwa nitapewa dhamana na NCCR-Mageuzi.

Kwa hiyo unaposema nimekuwa kimya  baada ya mchakato ule, kiuhalisia sikuwa na cha kuongea. Nawaheshimu Profesa Lipumba na Dk. Slaa na katika vikao vya kuteua mgombea urais wa kuwakilisha Ukawa, tulikubaliana kwa pamoja kuwa Dk. Slaa ndiye agombee urais baadaye Chadema wakaleta mgombea mwingine.

Sababu nyingine ya ukimya mimi ni mtumishi wa umma hivyo siruhusiwi kusimama kwenye majukwaa ya kisiasa, nafasi yangu ni kutoa maoni na kuzungumza na vyombo vya habari.

MTANZANIA Jumapili: Uamuzi uliouchukua wa kuacha siasa unadhani utaaminika tena kwenye ulingo wa siasa?

Dk. Kahangwa: Nadhani kama Watanzania na wanasiasa wanapenda haki, baada ya uamuzi wangu ni wakati wa kuniamini zaidi, kwa sababu tufike mahali Watanzania wawe wanaamini ukweli.

Kuna msemo unaopendwa kuwa “ukweli mchungu lakini ukiusema unauma” huu ni ukweli.

Kwani viliundwa vyama vya siasa  kwa ajili ya kazi gani? Lengo la vyama vya siasa si kulenga kuwa watu fulani wajinufaishe na wengine wakitaka kusimama kuitumikia siasa kama kugombea wanazuiwa.

Kama tunasema kuwa tunajenga demokrasia, ieleweke kuwa demokrasia ni kuwapa uhuru watu na kuwapa nafasi ya kugombea, inapotokea chama kinazuia watu kugombea hicho chama cha nini?

Inabidi tuseme haya ili jipu lililopo ndani ya chama litumbuliwe ili vifike mahali viweze kusimamia misingi na kujitambua vipo kwa malengo yapi.

Nakwambia ukweli mambo yanayoendeshwa ndani ya NCCR-Mageuzi, kama hayasemwi hakika chama kitazidi kusogea kaburini. Lakini kikijitathmini na kuondoa giza lililopo kitarudi kwenye hadhi yake ya awali.

MTANZANIA Jumapili: Kama mwanga ukipatikana ndani ya NCCR-Mageuzi, utarudi?

Dk. Kahangwa:  Si kwamba ninaweza kurudi huko kwa sababu mwanga umepatikana, nimewapa nafasi wawashe taa kwa sababu aliyezima anajulikana, aliyefunga kufuli anajulikana na ndiyo maana nilisema awali tatizo ni uongozi.

MTANZANIA Jumapili: Unaamini ili mwanga upatikane ni lazima uongozi uliopo uondoke?

Dk. Kahangwa: Hapana uongozi uliopo unayo nafasi ya kujirekebisha, ninajua watakuwa na uchaguzi mwakani labda wanaweza kuchagua viongozi wapya, lakini wanatakiwa kuchagua viongozi wanaojua wanafanya nini na wenye kujua malengo ya chama.

Hata kama wakifanya hayo siwezi kurudi nitabaki nje ya wigo, lakini nitakuwa tayari kutoa ushauri kwao na kukosoa kama bado kuna tatizo lolote.

MTANZANIA Jumapili: Kwa sasa upo nje ya ulingo wa siasa ikizingatiwa kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi la makada wa vyama kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine, je, tutegemee utajiunga na chama kingine cha siasa?

Dk. Kahangwa: Hapana, sijiungi na CCM wala chama kingine chochote. Na mimi napenda kuwakaribisha Watanzania kwenye chama cha maendeleo kwa Watanzania, ambacho hakina mfungamano wowote na siasa nchini.

MTANZANIA Jumapili: Miaka 25 ya mfumo wa vyama vingi, unadhani vyama vya siasa hususani vya upinzani vimekuwa kidemokrasia?

Dk. Kahangwa: Ni ajabu ya Tanzania, nchi hii imekuwa na upekee katika ukanda wa maziwa makuu kwamba vilipoanzishwa vyama vingi, tumeona vyama tawala ilifika mahali viliondoka kwa Tanzania mpaka sasa hilo halijatokea.

Mfano kwa Kenya, chama cha KANU hakijulikani kama kipo lakini kwa Tanzania imebaki CCM iliyoundwa na vyama vilivyopigania uhuru  wakati upande wa pili tunaona upinzani unaundwa na vyama dhaifu.

Naweza kufafanua tu kuwa katika kambi ya upinzani, chama ambacho angalau kina nguvu ni Chadema. Chama hiki kiko vizuri sana.

Mimi kama mtafiti  nazunguka sehemu mbalimbali nchini si kwamba natafiti masuala ya siasa la hasha! Nipo kwenye mambo ya elimu lakini unapofika vijijini hasa Tanzania Bara utaikuta Chadema.

Kwa kweli kazi waliyofanya ya kusambaa nchi nzima si ya kubezwa, imefika mahali watu wanahusisha vyama vyote vya upinzani kuwa ni Chadema.

Ingawa Chadema nao wana shida zao  lakini wamefanikiwa kujenga hizo nguvu. Ukiangalia kwa upande wa visiwani bado hawajajiimarisha, kuna haja chama hicho kuongeza nguvu upande huo ili siku moja kiwe chama tawala.

Uzuri wa Chadema ni kuwa kimefanikiwa kuhimili makombora  mazito ya kukimaliza hivyo kinaweza kupita katika hali yoyote ngumu. Binafsi natamani hata vyama vingine vya upinzani viwe na hadhi kama Chadema, kwani wana viongozi wenye kujiamini pia wana moyo wa kuisimamia siasa.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini hutaki kwenda CCM ambako ni kimbilio la makada wengi kutoka upinzani?

Dk. Kahangwa: Siwezi kwenda CCM kwa sababu chama hicho nacho kina matatizo yake.

Vyama ambavyo ni vya rika lake vilikufa kama nilivyokuambia awali, lakini chenyewe kikabaki basi ujue kina siri kubwa ya kukifanya kiishi japokuwa kinaonekana wazi kusaidiwa na dola.

Pamoja na kufanikiwa kwake kuishi bado CCM ina shida moja ambayo ni kero kubwa kwa Watanzania. Shida hii ni kukataa habari ya Katiba Mpya.

Kwa hiyo hata nikienda CCM nitakuwa ni mtu niliyesaliti jitihada zangu na za Watanzania wengi za kuitafuta Katiba Mpya.

Binafsi bila kuwa ndani ya chama naamini kwamba kweli Taifa hili linahitaji Katiba Mpya kwa sababu nyingi ambazo zipo wazi na Watanzania wanazifahamu.

Inaonekana kabisa CCM hawataki Katiba Mpya na huo ndio mtazamo wao. Kumbuka wakati ule nilipokuwa ndani ya upinzani tuliinyooshea kidole Serikali kuwa kuna ufisadi, Rais Dk. John Magufuli na Serikali yake wamejitahidi kupambana nao lakini hili la Katiba bado hawajanywa kikombe cha pili cha ukamilifu.

Yaani huu ni mfano kama ule wa Adam na Eva, baada ya kuondolewa kwenye bustani ya Eden kwa kula mti wa matunda ya kupata akili, sasa laiti kama wangekula na huu mti wa matunda ya uzima.

Naweza kusema CCM imeshtuka kwamba ufisadi ni tatizo, lakini haijashtuka jambo la pili la Katiba Mpya ambalo litakuwa limekata mzizi wote wa fitina katika Taifa hili.

Kwa hiyo hadi hapo CCM itakapokuwa na mwelekeo wa kuleta Katiba Mpya kwa Watanzania ndio hapo itakaponipendeza na kuwavutia wengi wenye mtazamo kama wangu.

MTANZANIA Jumapili: Unauzungumziaje uongozi wa Rais Dk. Magufuli?

Dk. Kahangwa: Bahati nzuri mimi ni Mkristo, ninaamini kuwa uongozi kuwapo, uwe ni uongozi mzuri au mbaya basi Mungu ana makusudi yake hivyo ndivyo tunavyofundishwa katika imani yetu.

Na katika historia iliyoandikwa ndani ya Biblia kwenye eneo la Mesopotamia, ambako Waisraeli walichukuliwa mateka alikuwapo kijana Danieli ambaye alikuwa na roho ya kinabii ambaye alimweleza mtawala wa kule awamu za utawala.

Alimweleza mfalme kuwa awamu ya kwanza ya utawala huwa ni dhahabu, unafuata wa fedha, unafuata wa shaba, kisha unakuwa wa chuma na una malizika utawala wa chuma na mchanga kisha Mungu ataweka utawala wake.

Kwa hiyo awamu tano hadi sita zipo ambazo nabii alijaribu kuzungumzia kwa mfano wa dunia nzima lakini kama taifa aliyoyasema Danieli tunaweza kuyaona hata kwenye picha ya Tanzania.

Tulikuwa na uongozi mzuri sana hapa nchini ambao uliongozwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Na uongozi huo ni sawa sasa na utawala wa dhahabu.

Wakafuata waliofuata baada ya dhahabu kilichofuata ni fedha  kwa mujibu wa ule unabii, ambapo tunakumbuka utawala wa Mzee Ali Hassan Mwinyi na ikaja awamu ya shaba ambayo nadhani iliwaunganisha watu wawili Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, viongozi hawa walikuwa na kufanana kwa karibu hawakubadilisha sana milengo iliyokuwa imewatangulia.

Sasa tupo kwa Rais Dk. Magufuli, binafsi ninaweza kusema kwamba kwa jinsi alivyotambulishwa na mtangulizi wake, akamtaja kabisa kwamba ametuletea chuma. Naweza kusema tupo chini ya uongozi wa Dk. Magufuli ambao ni awamu ya chuma kwa taifa letu.

Inawezekana Mzee Kikwete alisema pasipokujua kwamba hayo yapo katika unabii wa Danieli, lakini alitwambia kabisa kwamba “nimewaletea chuma hiki”.

Kwa mantiki hii enzi ya chuma itaisha na siku moja tutaelekea kwenye enzi ya chuma na mchanga na hapa naomba nikazie kidogo kwamba katika enzi ya chuma na mchanga pengine tunaweza kwenda kwenye Serikali ya umoja wa kitaifa na hii inaweza kuletwa na Katiba Mpya. Na kama tutaendesha vizuri huko tuendako tunaweza kuwa kwenye mwelekeo wa mafanikio makubwa.

Na huu ndio umuhimu wa kumwomba Mungu atuweke pamoja bila kujali dini au itikadi yoyote ya kisiasa, nadhani hata Danieli alitoa unabii huo kwa kutambua kwamba baada ya kuvuka awamu zote tano, awamu ya chuma na mchanga itakuwa ina maana ya binadamu kuweka tofauti zao pembeni na kuungana kwa upendo lakini pengine kwa mshikamano wao wanaweza wasishikamane vizuri.

Hivyo Danieli alivyozungumza kwamba baada ya awamu zote hizo kupita, Mwenyezi Mungu ndiye ataamua kubadilisha aina ya utawala na kuweka wa kwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles