Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 1,815 za dawa za kulevya aina ya skanka katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ukamataji huo uliohusisha watuhumiwa watano wanaodaiwa kuhusika na dawa hizo umefanyika kupitia operesheni iliyofanyika Agosti 28 hadi Septemba 2 mwaka huu katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam
Akizungumza leo Septemba 10 2024 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema uwekezaji unaofanywa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya utasaidia kulinda kizazi cha sasa na kijacho kwa kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya na kuendelea kutoa elimu nchini.
“Skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya TetrahydrocannabInol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu,akili na kusababaisha magonjwa ya maambukizi kama vile moyo, figo na ini,” alisema.
Kamishna Lyimo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Richard Mwanri (47)mfanyabiashara mkazi wa Mbezi Makonde Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, Felista Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguruni Mbezi Wilaya ya ubungo jijini Dare s Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilizokutwa dawa hizo za kulevya.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Athumani Mohamedi (58) ni mfanyabiashara na mkazi wa Tanga , Omary Mohamed (32)dereva wa bajaji ni mkazi wa buza Dar es Salaam na Juma Chapa (36)mkazi wa Kiwalani Dar es Salaam .
Aidha atika operasheni hiyo gari aina ya Mistubishi Pajero yenye namba za usajili T551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa.
Kamishna Jenerali Lyimo alifafanua kuwa mtuhumiwa Richard Mwanri ni mharifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuzisambaza nchini kwa usafiri wa magari.
Alisema mtuhumiwa huyo huwa anazificha dawa hizo kwa kuzichanganya na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mmbalimbali nchini.
“Kwa siku za hivi karibuni dawa za kulevya aina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara nchini ,”alisema.