ELIUD NGONDO, MOMBA
MKUU wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Juma Irado amewataka wafugaji wote kuanza kuchanja mifungo yao ili kutokomeza vimelea vya ugonjwa wa Kimeta vilivyosababisha watu wanne kufariki dunia na wengine 81 kuugua.
Irando aliyasema hayo jana, wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Nzoka ambacho mifugo imeathirika na vimelea vya ugonjwa huo na kuwataka waepukane na ulaji wa mizoga na kunywa maziwa katika kipindi hiki.
Alisema kampeni hiyo, inaenda sambamba na kutoa chanjo kwa mifugo dhidi ya ugonjwa huo wa kimeta kuanzia kijijini kilichoathirika na kisha kampeni hiyo kuendelea wilaya nzima na kuhakikisha mifugo yote inayoingizwa wilayani humo iwe imechanjwa.
“Wakati wa zoezi hii wafugaji wote waipeleke mifugo yao ili iweze kutibiwa na wale watakao kuwa wakiingiza mifugo ndani ya Wilaya wahakikishe wameshaipima na wamepewa kibali la sivyo hawataruhusiwa kuingiza mifugo yao wilayani humo,” alisema Irando.
Ofisa Mifugo wa Kata ya Nzoka, Sydeney Ngonyani alisema tayari amekamilisha kuchanja ng’ombe zaidi ya 500 waliopo na anatarajia kuanza vijiji vingne vinavyounda kata hiyo.
Alisema amepokea chupa 70 za dawa ambazo zinatarajia kuchanja ngombe 700, hivyo amewataka wakazi wa kata hiyo kujitokeza kuchanja mifugo yao na endapo mfugo wowote utaugua au kufa wasile nyama bali wafikishe taarifa kwa viongoziili uchunguzi ufanyike.
Alisema kama wafugaji wataungana kuweza kuipeleka mifugo yao kuweza kutibiwa basi ugonjwa huo unaweza kutokomea kwani ni ugonjwa ambao ukiwaishwa kupatiwa tiba ni rahisi kuweza kupona na kupotea.
Baadhi ya wananchi wa kata hiyo walioathirika na ugonjwa huo wamepongeza jukumu lililotolewa na mkuu wa wilaya na kuwa kuchanja mifugo yao litasaidia kutokomeza vimelea vya kimeta na kutoa wito kwa wananchi wengne kujitokeza kuchanja mifugo yao.
Hamis Simkonda, mfugaji alisema ugonjwa huo umekuwa ni tishio kwa muda mfupi hivyo wafugaji wakiichanja mifugo yao ni rahisi kuweza kuutokomeza.
Alisema wananchi wamekuwa wakaidi sana pale wanapoambiwa wasile nyama ya ng’ombe aliyekufa mwenyewe kutokana na kuamini kuwa mnyama huyo amekufa kwa magonjwa mengi ambayo sio hatari kwa afya zao.