24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

DARASA LA UNYAGO HADI SIKU TISINI

  • Ni moja ya mila ‘zinazowatafuna’ wanafunzi wa kike Nanyumbu

Na ASHA BANI, NANYUMBU

UNAWEZA kukiita kinyang’anyiro. Kinyang’anyiro hiki si cha fedha wala mali. Siyo cha kombe katika michezo wala mashindano yoyote yale.

Hiki ni kinyang’anyiro cha matumizi ya siku za masomo kwa wanafunzi katika mwaka, baina ya serikali na jamii zinazoishi katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

Wakati serikali ikiwa imetangaza kwamba siku 194 kwa mwaka zitatumika kwa ajili ya masomo kwa mwaka huu, baadhi ya jamii hizi zinatumia karibu nusu ya siku hizo kwa ajili ya masuala ya mila za unyago kwa watoto wa kike.

Imebainika kuwa shughuli za unyago miongoni mwa jamii zinazoishi wilayani Nanyumbu huanza kwa wahusika ambao ni mabinti wadogo kuwekwa ndani kwa siku kadhaa (kati ya miezi miwili hadi mitatu) na baada ya hapo hutolewa kwa ajili ya kufundwa (unyagoni) kwa siku kama 30.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Chipuputa wilayani humo, Osmund Mkanuwoga anasema unyago ni miongoni mwa vikwazo vya elimu kwa watoto wa kikle.

Mkanuwoga anasema wana ushahidi wa baadhi ya wanafunzi ambao huwa hawaonekani kwa muda mrefu shuleni, walipofuatilia wakabaini kuwa waliwekwa ndani kama wanawali kwa muda mrefu.

“Mwingine anawekwa ndani kwa kipindi hata cha miezi miwili au mitatu akisubiri kuchezwa,” anasema mwalimu huyo huku akisisitiza kuwa mila hizo zina athari kubwa za kielimu kwa wanafunzi wa kike.

Ripoti ya utafiti iliyopewa jina la “Ndoa za Utotoni nchini Tanzania: Mtazamo wa Haraka ya Machi 2017 inataja unyago kuwa miongoni mwa mila na desturi zinazochangia mimba za utotoni nchini huku zikiathiri elimu kwa watoto wa kike.

“Ziko ibada nyingi za unyago, ngoma za asili, ukeketaji na shughuli nyingine za kijamii ambazo kimsingi huwaandaa mabinti kuingia kwenye ‘umama’ kwa kuwapa mafunzo, mara nyingine watoto miaka tisa hufundishwa mambo ya ndoa na kujamiiana,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza:

“Mabinti hawa wakijifunza mambo hayo huamua kuyafanyia kazi kwa kuanza matendo ya ngono mapema katika umri mdogo na wengine kuamua kuolewa kabisa.”

Ripoti hiyo ambayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Repoa kwa niaba ya serikali na mashirika kadhaa ya ndani na nje ya nchi, inayataja makabila ya Wamakonde, Wayao na Wamakua yanayopatikana katika mikoa ya  Lindi na Mtwara kuwa miongoni mwa jamii za Kitanzania ambazo bado zinatukuza mila na desturi za aina hiyo.

MTANZANIA liliambiwa kuwa baadhi ya ngoma ambazo huchezwa ni pamoja na Tontoo, Litiwoo na Singenge. Zote huchezwa baada ya binti kuwa amewekwa ndani (mwali) kwa kipindi kirefu. Baada ya hapo hutolewa kwa ngoma.

Hufundishwa nini?

Mabinti wawapo unyagoni hufundwa na watu wanaoitwa Manyakanga. Miongoni mwa mafunzo hayo ambayo hutolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka minane hadi 13 ni pamoja na jinsi ya kumtunza mume, kulea familia na wakati mwingine hufundishwa ‘jinsi ya kumridhisha mume’ pindi wanapokuwa katika tendo la ndoa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chipuputa, Rachel Nanguka anasema uzoefu unathibitisha kuwa watoto wengine wakishatoka kwenye unyago hujiingiza moja kwa moja kwenye vitendo vya ngono jambo ambalo ni hatari.

“Unaweza kukuta binti wa miaka 13 ana wanaume saba hali ambayo hata mkubwa hawezi kuifikia, lakini yeye anaona sawa kwa sababu anakuwa anataka kuonyesha ujuzi kwa kile alichojifunza,” anasema Nanguka.

Nyakanga aliyejitambulisha kwa jina la Bibi Katoro kutoka kijiji cha Sengenya, anasema shughuli yao kubwa baada ya wali kuwekwa ndani huwa ni kutoa mafunzo malipo ya fedha kidogo.

“Huwa tunawafunza wali mambo mbalimbali ya kijamii ambayo ni kama jinsi ya kutunza familia, kutunza mume na ujuzi pindi awapo kwa mume wake,” anasema Nyakanga Katoro.

Anasema kwa watoto wajeuri huwa wanafundwa waachane na tabia mbaya na ujeuri na kwamba wakati mwingine hulazimika kuwachapa viboko kama adhabu pale wapokeapo mashtaka kutoka kwa wazazi wa watoto husika.

Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Nanyumbu, Ahamad Tabia anasema zamani mafunzo hayo yalikuwa yakitolewa kwa mabinti wenye umri mkubwa waliokuwa na umri unaowaruhusu kuingia katika ndoa tofauti na sasa.

“Kwa sasa miaka mitano, sita au saba anafanyiwa unyago hii inakuwa changamoto kubwa kweli wanafundishwa na kisha wanakwenda kufanya mazoezi ya huo mchezo,” anasema Tabia.

Ripoti ya mwaka 2015 inayoitwa ‘Athari za mimba na ndoa za utotoni kwa wasichana kielimu nchini Tanzania, inabainisha kuwa unyago una athari kubwa kwa watoto wa kike kwa kuwa hufundidhwa masuala ya familia na unyumba katika umri mdogo.

Ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Shule za Sheria za Vyuo Vikuu vya Washington na Lee vya Marekani kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC).

“Mabinti hujifunza majukumu ya kutunza nyumba kama vile kupika na usafi pamoja na jinsi ya kumtunza mume. Tendo la ndoa pia ni sehemu ya mafundisho hayo… kwa hiyo wasichana wengi huamua kuolewa mara tu baada ya kumaliza kuchezwa ngoma hizo,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Mkazi wa Kijiji cha Lidede katika Kata ya Kilimanihewa, Hidaya Kuria yeye anasema watoto wa kike wenyewe hawafugiki licha ya kwamba mila kwa kiasi kidogo zinachochea.

Kuria anapinga kuwa unyago siyo sababu ya watoto kushindwa shule na kwamba ni mila kama ilivyo kwa makabila mengine.

“Utandawazi pia kwetu umeingia kwa kasi, mtoto wa darasa la saba anaweza akalala hata na baba yako pia kuna starehe ‘vumbi’ huku ambazo zinamfanya mtoto aweze kuingia na kuanza kuangalia mambo ya utandawazi na kujifunza,” anasema Hidaya.

Wanafunzi je?

Fadhila Jadini anayesoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Chipuputa, anasema athari za unyago zipo na kwamba walipoanza kidato cha kwanza walikuwa wasichana wengi lakini sasa wamebaki watano.

Anasema kuchezwa ngoma katika umri mdogo kumechangia kwani mambo wanayofundishwa ya kumtunza mume na familia huwashawishi wengine kuyafanya kwa vitendo.

Mkuu wa Shule ya Chipuputa, Osmund Mkanuwoga anasema wasichana wa kidato cha nne ambao hivi sasa wamebaki watano tu, walianza wakiwa 17 na kwamba wengine waliacha masomo.

Naye mwanafunzi Anjoshola Ismail anasema yeye alichezwa unyago na kwamba anakumbuka mengi aliyofundihwa hadi leo.

“Lakini namuomba Mungu nisijiingize katika kuyafanyia mazoezi kwa vitendo kwani madhara yake ni makubwa maana nina ndoto za kusoma na kufika chuo,” anasema.

Kwa upande wake Riziki Hokororo anayesoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Sengenya anakiri kwamba alichezwa unyago akiwa na miaka 10.

“Yaani huko tulifundishwa mambo mengi hasa ya ndoa na kumtunza mume, kulea familia na mambo mengi tu ya wakubwa,” anasema Riziki.

Mwingine ni Hatimaye Shaibu anayesoma kidato cha kwanza katika shule hiyo ambaye anasema yeye alichezwa akiwa na miaka minane na kwamba alifundishwa kumtunza mume ikiwa atampata.

Fatuma Anusa ambaye anasoma kidato cha pili anasema: “Usipojizuia mambo unayofundishwa kwenye unyago unaweza ukayafanya na yakakuletea madhara.”

Fatuma anasema wapo wasichana ambao huwalazimisha wazazi wao kuwapeleka kwenye unyago kwani usipofanya hivyo mabinti wenzao huwazomea na kuwatenga.

Mwanafunzi mwengine ambaye hakuweza kuendelea na masomo kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo licha ya kufaulu  na sasa ana watoto wawili, Naumia Ismail anasema hata yeye siku ya kwanza kukutana na mwanamume hakuona tabu kwa kuwa mafunzo alishayapata tangu akiwa darasa la tano.

Hatua za kuchukua

Mkazi wa Mangaka aliyejitambulisha kwa jina la Mohammed Bakari anawatuhumu wazazi wa kike kuwa sababu ya kushamiri kwa mila zinazotukuza unyago.

Anasema serikali kupitia Afisa Utamaduni walipiga marufuku kufanya unyago muda wote na badala yake iwe wakati wa likizo. lakini wanawake wamebuni mbinu mpya.

“Baada ya kupangiwa siku za kufanya unyago hawa wanawake wamebuni njia mpya…kila Ijumaa, Jumamosi au Jumapili wanafanya kitu kinaitwa ‘nipeni raha’ ni kama vile ‘disko vumbi’ huko wanafanya mambo yale yale tena hadharani anamfunza nini mtoto?”anahoji Bakari na kuongeza:

“Yaani hawawezi kuvumilia bila kufanya mangoma ngoma na hata wakati mwingine hiyo ‘nipeni raha’ wanawaalika hata madiwani wanahudhuria na kuserebuka nao, mambo yanayofanywa hapo ni hatari kabisa.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Hamis Dambaya anasema wamepiga marufuku jando na unyago wakati wa masomo.

“Tumeamua kwamba hizo mila na desturi za kuchezana ngoma zifanyike Juni na Desemba (wakati wa likizo), labda itasaidia kumfanya mtoto wa kike apate elimu badala ya kuwekwa ndani kwa kipindi kirefu,”anasema Dambaya.

Ofisa Utamaduni wa Wilaya, Tabia anasema kutokana na unyago kuchangia kuporomoka kwa elimu ya mtoto wa kike, wameanzisha utaratibu wa kutoa vibali maalumu kwa sherehe hizo.

Anasema vibali hivyo hutolewa wakati wa likizo tu na si vinginevyo. Kuhusu ‘nipeni raha’ anakiri kwamba matukio hayo yapo na kwamba yanafanyika kwa vibali vya halmashauri.

Anasema nipeni raha ni tofauti na ngoma za unyago. “Lakini hata huo muziki tunatoa kibali na hawezi kucheza pia bila kibali cha polisi. Wanaruhusiwa Jumamosi na Jumapili tu,” anasema Tabia.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles