25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

DHAHABU, SHABA KUANZA KUCHIMBWA BAHARINI KWA KUTUMIA ROBOTI

Na JUSTIN DAMIAN

KWA mara ya kwanza katika historia, uchimbaji wa madini ya dhahabu na shaba unatarajiwa kufanyika kwenye kina kirefu chini ya bahari ifikapo mwaka 2019.

Kwa mujibu wa kampuni ya Nautilus Minerals Inc ya nchini Canada, uchimbaji huo utafanyika pwani ya nchi ya Papua New Guine ambayo inaelezwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini hayo na utafanywa kwa kutumia roboti anayeendeshwa kwa rimoti.

Roboti hao ambao mdogo ana uzito wa tani 200, watakuwa na uwezo wa kuvunja miamba iliyopo chini ya bahari na kutoa madini na hivyo kurahisisha uapatikanaji wa madini hayo yenye soko kubwa duniani.

Watu wengi hawafahamu kuwa chini ya bahari kuna madini mengi kuliko hata ardhini. Tatizo limekuwa ni namna ya kuyachimba, tunashukuru teknolojia kutuwezesha kufanya uchimbaji huu wa aina yake,” anasema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nautilus, Michael Johnston.

Mikataba mingi imetolewa na Shirika la International Seabed Authority (ISA), lililopo chini ya Umoja wa Mataifa ili kufanya utafiti wa madini yaliyopo baharini.

Chini ya bahari kuna utajiri mkubwa wa madini yenye ubora wa hali ya juu,” anasema Katibu Mkuu wa ISA, Michael Lodge.

Kampuni ya Nautilus inasema tayari wameshafanya majaribio na upatikanaji wa madini ya shaba katika eneo hilo chini ya bahari ni mara kumi zaidi ya yale yanayopatikana ardhini, huku ubora wa midini hayo ukiwa mara saba zaidi ya yanayopatikana ardhini.

Roboti watakaofanya kazi ya uchimbaji wametengenezwa kumudu kufanya kazi katika mazingira ya baridi inayoweza kugandisha huku presha ikiwa ni mara 150 zaidi ya iliyopo kwenye usawa wa bahari.

Roboti wa kwanza atakuwa akifanya kazi ya kuvunja vunja miamba ili kuwezesha roboti wa poili ambaye ni maalumu kwa ajili ya kusaga na kuchambua madini yatakayokuwapo kwenye miamba hiyo.

Roboti wa tatu atakuwa nyuma ya watangulizi wawili, ambapo kazi yake ni kuchukua madini yaliyochanganyikana na udongo kidogo wa miamba na kupeleka juu ya bahari ambako kuna meli.

Meli hiyo itakuwa na mitambo maalumu ya kuchambua na kupata madini safi. Mabaki ya udongo yatarudishwa baharini huku yale safi yakisafirishwa moja kwa moja kwenda sokoni nchini China.

Hata hivyo, uchimbaji huo unakabiliwa na vikwazo kutoka kwa wanamazingira ambao wanasema bado haujafanyika utafiti wa kutosha kuonesha kama hautakuwa na athari kwa mazingira ya baharini na viumbe wake.

Kuna mambo mengi hayafahamiki juu ya uchimbaji wa madini chini ya bahari,” anasema mwanamazingira wa nchini Australia, Natalie Lowrey anayependekeza uchimbaji madini baharini usitishwe.

Anasisitiza: “Tumeharibu kiasi kikubwa cha ardhi kwa sababu ya uchimbaji madini, si jambo jema kuharibu na mazingira ya baharini.”

Lowrey anasema miamba itakayovunjwa na roboti wakati wa uchimbaji inaweza kusafiri na mawimbi na kuharibu ekolojia ya baharini ikiwa ni pamoja na keleta madhara kwa viumbe waishio majini.

“Kuna tishio kubwa katika uchimbaji huo unaoweza kusababisha madhara kwa binadamu wanaotegemea vitoweo kama samaki kutoka baharini, hasa kwa jamii zinanazoishi katika pwani ya Papua New Guinea,” anasema.

Kampuni ya Nautilus inachukulia suala la mabaki ya miamba kwa umakini mkubwa hivyo mashine za uchimbaji zimetengenezwa kwa kuzingatia suala hilo.

Wakati kampuni ya Nautilus ikijiandaa kwa ajili ya uchimbaji, kampuni nyingine za madini zimekuwa zikifuatilia kwa ukaribu maendeleo ya mradi huo na kama itafanikiwa, nyingine zitafuata.

“Kama Nautilus ikifanya vema, itakuwa imefungua dirisha jipya katika sekta hii,” anasema Lowrey.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles