
NA THERESIA GASPER,
KUELEKEA Siku ya Mtoto wa Afrika, mwanamuziki Damian Innocent ‘Damian Soul’, leo anaachia wimbo unaoitwa ‘Watoto wetu’ ambao umedhaminiwa na taasisi inayojishughulisha na upingaji wa adhabu kwa watoto shuleni ‘Save the Children’ na Kampuni ya Ubongo Limited.
Damian Soul alisema wimbo na video hiyo ni moja ya mradi ya kutetea haki za watoto shuleni pamoja na kupinga adhabu za watoto ikiwemo kuchapwa viboko.
“Kesho (leo) ni siku ya mtoto Afrika, video hii itaanza kuonyeshwa Uwanja wa JMK Kidongo Chekundu, ujumbe uliopo humo ni funzo kwa wazazi, walimu na wanafunzi pia ili kila mmoja atambue kwamba mwanafunzi anaweza kuelewa bila kuchapwa,” alisema.
Meneja wa taasisi hiyo, Sharon Kassohun, alisema wanataka kufanya mchakato utakaosaidia wanafunzi kupenda masomo yote na kuleta adhabu mbadala na kuchapwa viboko.
“Wimbo huu ni somo tosha kwa walimu wanaotoa adhabu za viboko kiasi kwamba baadhi ya wanafunzi hukimbia shule,” alisema.
Naye msemaji wa Kampuni ya Ubongo Limited, inayofundisha masomo ya hisabati na sayansi kwa watoto, Mohamed Juma, alisema mradi huo utaongeza hamasa ya kupatikana kwa haki za watoto.