NA MWANDISHI WETU
WAKATI mwanamuziki kutoka Oakland, California nchini Marekani, Antique Davis, akitarajia kufanya ziara ya kimuziki nchini Tanzania mwezi ujao amewataka mashabiki wake kupambana na changamoto wanazokutana nazo huku wakifikiria namna watu watakavyowaangalia kama zitawashinda.
Mwanamuziki huyo anayeimba muziki Afro pop, Afro Beat, Reggae na Dancehall, aliliambia MTANZANIA kwamba watu wengi wanakumbana na changamoto lakini wanakata tamaa mapema bila kuangalia namna gani wanatazamwa lakini wakitazama namna watakavyotazamwa kama watashindwa kupambana na changamoto.
Akizungumzia ziara yake mwanamuziki huyo alisema itaanzia nchini Ghana kwa wiki sita kisha atatua Tanzania na kumalizia nchini Hispania.
Antique alisema ziara hiyo ni maandalizi ya kutangaza albamu yake mpya ya ‘Remember Vol. II’ inayotarajiwa kutoka Juni ikiwa imebebwa na muziki wa Kiafrika ulioandaliwa nchini Ghana na nchi nyingine za Afrika Magharibi.
“Kiukweli nashukuru kwa nchi za Afrika kutokana na asilimia kubwa ya muziki wangu kuandaliwa huko na sasa nina ziara ya kimuziki kwa ajili ya kutangaza albamu hiyo na nimepanga kutembelea, DC& Ghana na Tanzania na kisha nitaelekea Hispania,” alisema Antique.