33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

DALILI MBAYA KWA UTAWALA WA TRUMP ZAANZA KUJITOKEZA

trump-family-presidential-candidateAKIANDAMWA na wakosoaji kwa kuteua au kufikiria kuteua watu wenye sifa mbaya ikiwamo ukiukaji wa haki za binadamu katika nyadhifa mbalimbali za utawala wake, Rais mteule Donald Trump sasa anaonywa juu ya uwezekano wa kutodumu madarakani.

Ni kutokana na kuonesha nyendo zinazotia shaka za mgongano wa maslahi katika kipindi hiki cha mpito, akijiandaa kuingia Ikulu ya Marekani, White House.

Kipindi cha wiki mbili tangu ashinde uchaguzi wa Novemba 8, ahadi yake ya kutenganisha biashara zake na maisha yake ya urais imezua maswali.

Amekuwa akikutana na wafanyabiashara na wanasiasa katika hoteli yake kubwa ambayo haiko mbali na White House na kuwatia wasiwasi wakosoaji iwapo kweli ataweza kutenganisha biashara zake na Ikulu.

Simu za Kamati ya Bunge ya Uchunguzi ziliripotiwa kukumbwa na msongamano wa miito ya simu Ijumaa iliyopita kufuatia mitandao ya jamii kuitaka kamati hiyo imchunguze Trump kwa kile wanachoona mgongano wa maslahi.

Wiki hii Trump alikutana na wafanyabiashara wa India ambao ana ushirika nao, Atul Chordia, Sagar Chordia na Kalpesh Mehta, wanaojenga pia jengo la kifahari la Trump mjini Mumbai.

Wakati Msemaji wa Trump Organization akiliambia gazeti la New York Times kuwa  mkutano huo haukuwa rasmi, vibopa hao wa India walitumia fursa hiyo kukutana na watoto wa Trump.

Watoto hao wanachukua uendeshaji wa biashara zake, wakati huo huo wakibakia katika timu ya mpito ya baba yao huyo wakionekana kuwa na ushawishi katika teuzi mbalimbali.

Mehta aliliambia gazeti la Economic Times kuwa Donald Trump Jr. ameeleza kuridhishwa na biashara za kampuni nchini India na ameonesha nia ya kupanua zaidi biashara nchini humo.

Akizungumza baada ya ushindi wa Trump, aliliambia gazeti hilo la uchumi: “India ina idadi kubwa ya miradi ya Trump hasa mali zisizohamishika, ikiwa kubwa zaidi nje ya Amerika ya Kaskazini. Trump ana mikataba inayoendelea mitano nchini humo yenye thamani ya dola bilioni 1.5.

“Uzalishaji umeanza katika miradi miwili na miradi mitatu zaidi inatarajia kuzinduliwa mwaka 2017 na tunaendelea kusaka fursa zaidi,” alisema.

Miradi ya Trump nchini  India ni miongoni mwa biashara alizonazo ng’ambo ikiwamo nchini Uturuki, Indonesia, Israel, Dubai, Panama na  Philippines.

Nyota huyo wa zamani wa televisheni pia anadaiwa mkopo wa dola milioni 364 na pia anadaiwa na Benki ya China na Goldman Sachs.

Aidha ameonana na mabalozi kutoka nchi za Kiarabu katika hoteli yake ya nyota tano mjini Washington na kuzua utata mkubwa kwa vile wanadiplomasia hao wameripotiwa kulala katika hoteli hiyo mpya.

Wakati akionana na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe mwishoni mwa wiki, katika tukio lingine lililozua utata ilhali Rais Barack Obama bado yu madarakani, binti yake Ivanka alikuwapo katika mkutano huo sambamba na mumewe Jared Kushner.

Si Ivanka wala Kushner ambao wana kibali kinachowaruhusu kuwapo katika mkutano kama huo.

Baadhi ya wanasheria wanaonya Trump anaweza kushitakiwa bungeni na hata kuvuliwa urais atakapoapishwa kwa kitendo hicho.

Barua pepe iliyotumwa na kampuni yake Ivanka inayojishughulisha na vito vya thamani kufuatia kuonekana kwake katika kipindi cha luninga cha “60 Minutes” akiwa na baba yake pia ilikuja kama mshangao.

Iliwafahamisha wateja wapi wanaweza kununua bangili zenye thamani ya dola 10,800 sawa na Sh milioni 22 alizokuwa amevaa Ivanka siku hiyo.

Trump amesema atawaachia wanae waendeshe himaya yake ya kibiashara katika mfuko ujulikanao kama “Blind Trust.”

Lakini kinadharia, blind trust ambao huhusisha kuuza mali na kuzibadili kwa kuzifanya ziwe tofauti na zile Trump anazozijua , kwa mfumo wa sasa kuwatumia wanawe ni kitu kisichowezekana.

Kushner ameripotiwa kutafuta ushauri iwapo anaweza kuingia katika utawala wa Trump, huku timu ya mpito ya Rais Mteule ikijaribu kupata kibali kwa ajili ya mkwewe huyo, ambaye pia ni mfanyabiashara wa majengo na mmiliki wa gazeti la New York Observer.

Sheria inayokataza upendeleo wa kindugu ilipitishwa mwaka 1967 miaka michache baada ya Rais John F. Kennedy kumfanya kaka yake Robert, kuwa mwanasheria mkuu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, Rais hawezi kumteua mwanandugu kuingia katika shirika wakala au wadhifa wowote serikalini.

Ushawishi wa Kushner tayari umeelezwa kufanya yake. Ni baada ya Gavana wa New Jersey, Chris Christie kuondolewa kwa mshangao wa wengi kutoka uenyekiti wa timu ya mpito sambamba na wasaidizi wake wengine licha ya kazi nzuri waliyofanya wakati wa kampeni.

Inasemekana chanzo ni ushawishi wa huyu Kushner, uhasama ukianzia mapema miaka ya 2000 wakati baba yake Kushner, bilionea wa majengo Charles Kushner, ambaye pia alikuwa mfadhili maarufu wa chama cha  Democratic aliposhitakiwa kwa mashitaka ya ukwepaji kodi na kujaribu kuharibu ushahidi.

Kesi hiyo ilikuwa chini ya Christie, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa New Jersey, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kwa kuisimamia vyema huku vyombo vya habari vikitengeneza vichwa vya habari zilizouza mno.

Katika kesi hiyo, Charles alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela.

Miaka zaidi ya kumi baadaye imemkuta Christie akiwa ndani ya timu moja na mtoto wa bilionea huyo, lakini habari mbaya sana kwake ni mkwe wa bosi wake.

Kwamba kijana Jared Kushner (35), mtoto wa bilionea Charles, ni mume wa Ivanka Trump na zaidi ya hilo ni mshauri mwenye nguvu na ushawishi na anayeaminiwa zaidi kuliko wote na Trump.

Minong’ono iwapo wanafamilia wa Trump wataendelea kuwapo White House, inabakia kutokuwa rasmi lakini wanaweza kuikwepa sheria hiyo ya upendeleo kwa kitu kama Kushner kuwa mshauri wa bila malipo.

Makamu wa Rais Mteule Mike Pence tayari amejaribu kuzima wasiwasi unaozingira mgongano wa maslahi wakati akihojiwa hivi karibuni na Fox News.

Ni kuhusu iwapo watoto wa Trump kuendesha biashara kunaweza kutengeneza mgongamo hatari wa maslahi.

Gavana huyo wa Indiana alisema kuwa ana imani Trump atajikita katika masuala ya wananchi na kuhakikisha kuna utengano mzuri wa biashara zake na siasa.

Hata hivyo, hilo ni suala la kusubiri na kuona.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles