24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

CUF waja na sera ya ‘kuleta furaha’

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kuwekeza katika afya ya mama na mtoto kuna thamani kubwa kwa taifa na kunasaidia kupata nguvu kazi yenye tija.

Suala hilo ni miongoni mwa mambo matano yaliyomo katika sera ya chama hicho yenye lengo la kuwaletea furaha Watanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa sera hiyo jana, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema sera hiyo imejikita katika masuala ya afya, elimu, ajira, miundombinu na Tehama.

 “Tafiti zinaonyesha Tanzania ni ya nne kutoka chini kati ya nchi 153 zenye furaha duniani, nchi zingine za chini ni Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Afighanistan. Hawa wana vita, sisi tuna amani na utulivu, lakini watu hawana furaha… wengine hata ukiwatekenya hawacheki,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema sera hiyo imejikita katika maisha halisi ya Mtanzania na kwamba inalenga kuhakikisha wajawazito wanapata lishe bora na kujifungua salama, elimu bora itakayowasaidia watoto kuwa na ujuzi wa kutosha, mazingira ya sekta binafsi kutoa ajira kwa wingi, ujenzi wa miundombinu, pensheni kwa wazee na matumizi ya Tehama katika kuwezesha vijana kuendelea kujifunza.

“Mambo haya yanawezekana, kwa miaka 45 nimekuwa nikifanya utafiti na kujifunza masuala mbalimbali ya uchumi, hivyo ninayozungumza nayaelewa. Tutumie utaalamu na ujuzi tulionao kujenga nchi ambayo wananchi wake watakuwa na furaha wakati wote,” alisema.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema baadhi ya mambo waliyokuwa wakiyapigania kama suala la elimu bure, Serikali ya sasa inatekeleza na kuitaka iongeze kasi katika kutekeleza madai yao mengine.

“Hatuwezi kusimama hapa kupinga yale mazuri tuliyokuwa tunadai, ila tunasisitiza yaweze kutekelezwa ipasavyo. Tunaunga mkono juhudi za Serikali watoto waende shule, lakini wasome na tuwekeze kwa walimu ili wawe na hari ya kufundisha,” alisema.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa 2020, Profesa Lipumba alisema Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yatakuwa sehemu ya sera na ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles