27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Trump: Nilifikiri kwa sekunde moja na kuahirisha kuishambulia Iran

WASHINGTON DC, MAREKANI

RAIS Donald Trump amesema kuwa alifikiri kwa sekunde moja na kubatilisha uamuzi wake wa kuishambulia Iran baada ya kuambiwa kuwa watu 150 wangefariki endapo Marekani ingetekeleza shambulio hilo.

Akizungumza na kituo cha habari cha NBC, Trump alisema Marekani iko tayari kwa mazungumzo, lakini haitakubali Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Alisema hataki vita, lakini akaionya Iran kuwa itakabiliwa na makosa ya uharibifu vita vikizuka.

“Mpango wa kuishambulia Iran ulikuwa tayari na ulikuwa unasubiri amri yangu, lakini nilipoambiwa na majenerali wangu ni watu wangapi watauawa katika shambulizi hilo, nilisitisha hatua hiyo.

“Niliwaza kwa sekunde moja hivi, kisha nikawaambia mnajua nini, wao wameangusha ndege isiyokuwa na rubani, sisi tukiamua kulipiza kisasi tutawaangamiza watu 150,” aliiambia NBC.

Tehran imesema ndege ya Marekani ambayo haikuwa na rubani iliingia anga lake mapema Alhamisi iliyopita.

Marekani inasisitiza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikipaa juu ya anga la kimataifa.

Hali ya taharuki imekuwa ikiongezeka kati ya mataifa hayo, huku Marekani ikiilaumu Iran kwa kushambulia meli za mafuta zinazohudumu katika eneo hilo.

Iran imetangaza kuwa hivi karibuni itazidisha kiwango cha kimataifa kinachodhibiti uzalishaji wa madini ya uranium katika mpango wake wa nyuklia.

Mwaka jana, Rais Trump alijiondoa katika mkataba wa kimataifa wa nyuklia uliofikiwa mwaka 2015 lengo likiwa kudhibiti shughuli za nyuklia za Iran.

Marekani sasa imeomba kukutana na Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hatua ya Iran.

Trump alikanusha madai kuwa ndege zake tayari zilikuwa njiani kuelekea Iran kwa operesheni hiyo.

“Hakuna ndege ilikuwa angani,” alisema.

Trump alimwambia rais wa Iran; “huwezi kumiliki silaha za nyuklia, na kama unataka tujadiliane kuhusu hilo ni sawa, la sivyo utaendelea kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi.”

HATUA YA TRUMP IMECHUKULIWAJE?

Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, alisema alishukuru kuwa Rais hakuchukua hatua ya kuishambulia Iran na kuongeza kuwa ni vyema wakati mwingine awasilishe ombi bungeni kabla ya kuchukua hatua ya kijeshi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya hapa vimeripoti kuwa shambulizi hilo lilikuwa limeidhinishwa na Pentagon, huku vingine vikiripoti kuwa maofisa wakuu wa Pentagon walikuwa wameonya kuwa hatua hiyo ingelihalalisha hali ya vikosi vya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Gazeti la Associated Press liliripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, na mshauri wa kitaifa wa masuala ya usalama, John Bolton, walikuwa wameshikilia misimamo mikali kuhusu suala hilo, lakini waliombwa na viongozi wengine kuwa makini.

Mamlaka ya Usafiri wa Angani Marekani (FAA) imetoa agizo la kuzuia mashirika ya ndege za Marekani kupaa juu ya anga la Ghuba ya Uajemi na Oman.

Huku hayo yakijiri, mashirika kadhaa ya ndege yamefuta safari zao au kujiepusha na anga la Iran baada ya ndege ya ujasusi ya Marekani isiyokuwa na rubani kudunguliwa na majeshi ya ulinzi ya nchi hiyo.

Hii ni baada ya Iran kuthibitisha kuwa iliangusha ndege hiyo ikisema ilikiuka sheria za anga lake japo Marekani inapinga madai hayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, mashirika ya ndege yaliobadilisha njia ni Cathay Pacific, Emirates, Fly Dubai, British Airways, KLM, Qantas, Singapore Airlines na Lufthansa.

IRAN IMESEMAJE?

Ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa Iran, ameonya kuwa mashambulizi yoyote dhidi yao yatakuwa na athari ya kimataifa.

“Mlikiuka sheria za anga la Iran, na sisi tukajilinda,” Seyed Sajjadpour, mmoja wa manaibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo aliiambia BBC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles