23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Kesi mwalimu aliyemvunja mwanafunzi uti wa mgongo yafufuliwa

Na Elizabeth Kilindi-NJOMBE

JESHI la Polisi Mkoa wa Njombe linatarajia kurudisha mahakamani kesi ya aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Madeke, Focus Mbilinyi, anayedaiwa kumpiga aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Hosea Manga (10), mkazi wa Kijiji cha Madeke, Kata ya Mfriga wilayani hapa na kumsababishia kuvunjika uti wa mgongo.

Hatua hiyo imekuja baada ya gazeti hili kuripoti kwa kina kisa cha mwanafunzi huyo aliyedaiwa kupigwa na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu na mwalimu Mbilinyi miaka miwili iliyopita.

Kesi ya awali iliyofunguliwa mwaka 2017 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Njombe ilifutwa baada ya daktari aliyemtibu mtoto huyo kwa mara ya mwisho Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam  kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nne.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Salum Hamduni, alisema walimshikilia kwa siku mbili mwalimu huyo na baadae kutoka kwa dhamana kwa  sababu kesi iliondolewa mahakamani chini ya kifungu cha sheria namba 325.

Kamanda Hamduni alisema kifungu hicho pia kinaipa mamlaka polisi pamoja na waendesha mashtaka kumkamata ili kurudisha kesi mahakamani.

Alisema kuwa jalada la kesi hiyo tayari lipo kwa wakili wa Serikali.

“Jalada lipo kwa wakili wa Serikali ni hadi hapo tutakapopata majibu yake tutakuwa na uhakika ni lini atakwenda mahakamani,” alisema Kamanda Hamduni.

Tukio la mtoto huyo kudaiwa kupigwa hadi kuvunjika uti wa mgongo lilitokea Machi 21, 2017 na mwalimu huyo anadaiwa alimpa adhabu hiyo kwa sababu ya kukosa somo la hesabu.

Hosea alimwambia mwandishi wa habari hizi alipomtembelea nyumbani kwao Kijiji cha Madeke kuwa wakati akiwa katika kipindi cha somo la hesabu, mwalimu huyo aliwapa majaribio ya hesabu 10 ambazo alikosa zote.

“Ilikuwa asubuhi tukiwa tunasoma somo la hesabu, mwalimu alitupa hesabu 10 na akasema ukikosa utachapwa kulingana na hesabu ulizokosa, hivyo mimi nilikosa hesabu zote na kutakiwa kuchapwa fimbo 10.

“Wakati mwalimu anatuchapa tulikuwa watatu, alituning’iniza kichwa chini miguu juu katika moja ya dirisha darasani, lakini wakati tukio hilo likiendelea, ndipo nilipoangukia mgongo na kuhisi maumivu makali yaliyosababisha hadi leo hii natumia muda mwingi nikiwa hapa kitandani,” alisema Hosea ambaye wakati huo alikuwa darasa la tatu.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Boniface Manga, aliwahi kulieleza gazeti hili kuwa wakati tukio hilo lilipotokea alichelewa kupata taarifa na kwamba alizipata alipokwenda shuleni hapo kwa ajili ya mwanae mkubwa.

Manga alisema alipofika shuleni hapo alishangazwa kuulizwa na walimu iwapo Hosea alikuwa ni mlemavu, swali ambalo lilimshangaza kwa kuwa aliondoka nyumbani akiwa mzima.

Alisema alipokwenda kumwangalia, alikuta hawezi kusimama na muda mrefu ulikuwa umepita, na tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu bila mafanikio na amelazimika kusimama masomo kwa kuwa hawezi kufanya chochote.

Hata hivyo, baada tukio hilo kutokea, inadaiwa mwalimu Mbilinyi alihamishiwa Shule ya Msingi Uhelela iliyopo Kata ya Mtwango, wilayani Njombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles