Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameielekeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) isimamie kikamilifu fedha zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu ili wazipate kwa wakati na bila usumbufu wowote.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo wakati akifungua Mashindano ya Kitaifa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) huku akisema fedha hizo zinatengwa ili ziwasaidie kuendeleza kazi zao.
Pia, Waziri huyo ameilekeza COSTECH kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha ubunifu wote uliofikia katika hatua ya fainali unaingia katika mpango wa kuendelezwa ili uboreshwe na hatimaye kutumiwa na jamii ili wabunifu hao wanufaike na vipaji vyao huku akisema akili yao ndio mtaji wao katika kufikiria mambo ambayo yanaleta suluhu katika changamto zilizopo katika jamii.
“Sisi kama serikali zawadi pekee tunayoweza kuwapa ni kuwaendeleza ili ndoto zao za kutatua matatizo katika jamii ziwe kufanikiwa, naomba msimamie sana fedha ambazo zinatengwa kuwaendeleza wabunifu kuhakikisha wanazipata kwa wakati bila usumbufu wowote ili kazi yao njema iweze kuendelea,”amesisiti Prof. Ndalichako.
Aidha, amezungumzia kuhusu changamoto zinazowakabili wabunifu wachanga kuwa ni pamoja na kukosa mahali pa kutengenezea ubunifu wao huku akisema kwa kutambua changamoto hiyo serikali kupitia COSTECH imeanzia vituo atamizi 17 kwa ajili ya kukuza na kuendeleza bunifu nchini.
Amesema katika kuanzisha vituo hivyo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuanzishwa kwa makampuni machanga 94 yanayotokana na bunifu ambayo yamewezesha kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana takribani 600.
“Ili kuhakikisha vituo hivyo vya kuendeleza bunifu vinaendelea kuanzishwa na wadau mbalimbali, wizara kupitia COSTECH imewezesha kuanzishwa kwa kumbi za bunifu na atamizi katika taasisi za elimu ya juu,”amesema
Ndalichako.
Aidha, ametumia mashindano hayo kutoa wito kwa vijana wa Taasisi za Elimu ya Juu wenye bunifu wasisite kuonyesha bunifu zao na kwamba,serikali itaendelea kuwawekea mazingira wezeshi ili waweze kuziendeleza bunifu za vijana hao.
Amesema, kupitia COSTECH Serikali imetoa Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu wakiwemo 130 waliochaguliwa kupitia MAKISATU ya 2019 na 2020 ili ubunifu wao ufikie hatua ya kubiasharishwa na kutatua changamoto katika jamii.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo amesema katika kipindi cha miaka miwili yaani 2019 na 2020 ambayo MAKISATU imefanyika, jumla ya wabunifu wa teknolojia mbalimbali wapatao 1,066 waliibuliwa na kutambuliwa na wizara.
Amesema kati ya hao wabunifu mahiri 130 wanaendelezwa na serikali kupitia COSTECH ili ubunifu wao ufikie hatua kubiasharishwa na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana .