24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yaiweka Italia kwenye karantini

ROME, ITALIA

VIFO vitokanavyo na virusi vya corona nchini Italia vimefika 463 na watu walioambukizwa wamefika 9,172 hali iliyofanya nchi hiyo yenye watu milioni 60 kuweka karantini kwa watu wote ambapo sasa watatakiwa kutoka nje ya nyumba zao pale tu kutakapokuwa na ulazima.

Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte, ameamuru watu wabaki majumbani na sharti waombe ruhusa na kupata kibali kwa safari zenye umuhimu pekee.

Alisema hatua hizo zmewekwa kuwalinda wale walio hatarini kupata maambukizi.

 ”Hakuna muda zaidi,” alisema Conte alipohutubia raia kwa njia ya televisheni.

Idadi ya maambukizi imefikia asilimia 24 kutoka siku ya Jumapili, huku vifo vikifikia 463 kutoka 366 Jumatatu, ikiwa ni athari mbaya zaidi baada ya ile ya China.

Watu wenye virusi hivyo wanaelezwa kuwepo kwenye miji yote 20 ya Italia.

Conte alisema hatua bora zaidi ni watu wasalie majumbani.

“Kuna ongezeko kubwa la maambukizi na vifo, Italia nzima itakuwa kwenye uangalizi, sote tunapaswa kujitoa kwa ajili ya Italia. Tunapaswa kufanya hivyo sasa.

”Hii ndio sababu nimeamua kuchukua hatua ngumu zaidi ili kulinda afya za raia wote,” alisema Conte.

 

MAENEO YA MARUFUKU

Waziri Mkuu Conte alieleza hatua hiyo inajulikana kwa jina ‘ninabaki nyumbani’ – watu wakipigwa marufuku kukusanyika.

”Hakuna mikusanyiko ya starehe za usiku, hatuwezi kuruhusu hili tena,” alisema Conte

Kutokana na hali hiyo, michezo ikiwamo mechi za kandanda zimezuiwa nchi nzima. Shule zimefungwa na vyuo vitabaki kufungwa hadi Aprili 3.

Serikali ilisema wale wenye sababu za kikazi na kifamilia ambazo haziwezi kuahirishwa wataruhusiwa kusafiri.

Abiria wanaotaka kuondoka wanatakiwa kuwa na sababu za msingi, kama watakavyofanya wanaoingia na ndege kutoka nje.

Kwenye vituo vya treni kuna udhibiti pia, abiria hupimwa kiwango cha joto cha mwili. Meli pia zimezuiwa kutia nanga katika bandari kadhaa nchini humo.

Mapema Jumatatu, wafungwa saba walipoteza maisha kutokana na vurumai kwenye magereza nchi nzima baada ya mamlaka kupiga marufuku kuwatembelea wafungwa ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa.

Ghasia zilianza katika mji wa kaskazini wa Modena katika gereza la Sant’Anna.

Inadhaniwa watu wawili walipoteza maisha kutokana na kuzidisha kipimo cha dawa baada ya kuvamia hospitali ya gereza kwa ajili ya dawa ya methadone.

Katika gereza la San Vittore mjini Milan, wafungwa walichoma moto sehemu ya gereza, kisha walipanda darini kupitia dirishani wakipunga bendera.

Shirika la Habari la Italia la Ansa liliripoti kuwa kwenye gereza kusini mwa mji wa Foggia, wafungwa kadhaa walitoroka nje ya jengo wakati wa maandamano, wengi walikamatwa na tisa bado hawajulikani walipo.

Pia kulitokea vurugu katika magereza kaskazini mwa Italia mjini Naples na Roma.

 

HALI YA SASA DUNIANI

Idadi ya maambukizi dunia nzima sasa ni zaidi ya 111,000 na vifo takribani 3,890.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Natanyahu alisema kila atakayewasili nchini humo atawekwa karantini au kutakiwa kujiweka karantini kwa siku 14.

Iran imeripoti vifo 43 vipya kutokana na virusi vya corona katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Takribani watu 237 wamepoteza maisha na 7,161 wameambukizwa nchini humo tangu katikati ya Februari.

RAIS XI JINPING

Katika hatua nyingine, Rais wa China, Xi Jinping, aliutembelea mji wa Wuhan jana ikiwa ni mara ya kwanza tangu ulipokumbwa na virusi vya corona Januari.

Hatua ya Rais Xi kwenda Wuhan ambako ni kitovu cha maradhi yanayosababishwa na virusi vya corona, ni dalili kubwa inayowafanya maofisa kuamini kwamba mlipuko huo umedhibitiwa.

 Ziara ya Xi imekuja baada ya hatua ya mji wa Wuhan na Mkoa wa Hubei kuwekwa kwenye karantini tangu mwishoni mwa Januari kuonyesha kufanikiwa ambapo maambukizi mapya yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha wiki za karibuni.

Hatua iliyopigwa China ni kinyume na jinsi ugonjwa huo unavyoendelea kutanuka duniani ambapo sasa unasambaa kwa kasi nje ya China na Italia.

NCHI ZA GHUBA

Saudi Arabia, Kuwait, Qatar na Misri zilithibitisha kuwa na watu wenye maambukizi ya virusi vya corona katika ukanda wa Ghuba.

Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imeripoti maambukizi mapya matano kuifanya idadi ya walioambukizwa nchini humo kufikia 20.

 Kati ya wenye virusi hivyo, watano ni raia wa nchi hiyo ambao miongoni mwao watatu waliwasili kutoka Iran na Iraq na Mmisri mmoja.

Saudi Arabia imechukua hatua kadhaa za tahadhari kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo, ikiwemo kuzuia safari za ndege za kuingia na kutoka katika nchi 14. Kadhalika nchi hiyo imeweka sheria ya kufungwa kwa misikiti mikuu mitukufu ya Mecca na Madina nyakati za usiku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles