22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema tengenezeni chama chenu

CdX9GCWXIAAoeQ4-620x309SAFARI ya mafanikio haina njia ya mkato, kama kuna kanuni basi ni lazima uifuate na kama ni njia ndefu basi ni lazima upite njia hiyo yenye miiba  na tabu za kila aina, kwenye kutafuta mafanikio njia ya mkato si njia sahihi. Nimekitizama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nikaona ni heri niwashauri mambo kadhaa kama bado wana nia ya kushika dola kwenye siku zijazo.

Chama hiki kwa miaka ya karibuni ndio chama cha upinzani ambacho kimeonesha kuwa na uhai, hiki ni chama ambacho kimefanikiwa kujivisha sura ya uanaharakati japo kiuhalisia ni chama cha siasa ambacho lengo lake kuu ni kushika madaraka hayo mengine huwa ni njia ambayo husaidia chama kujipatia wafuasi. Kwenye uchaguzi uliopita nilijaribu kuangalia masuala kadhaa kwenye chama hiki na nikagundua kuwa chama hiki bado kina kazi ya kufanya ili kujiimarisha kabla ya kushika madaraka.

Chama ni kama mtoto, ambaye akizaliwa itambidi akae, atambae, asimame na mwisho atembee na kadri jinsi anavyokuwa ndivyo anazidi kuelekea kwenye mazingira ya kujitegemea na kukabidhiwa majukumu kadhaa. Kutokana na maelezo haya nakiona Chama cha Demokrasia na Maendeleo kama chama ambacho kinahitaji kutafuta wanachama kuanzia ngazi ya chini, nchi yetu ni kubwa na ukiangalia matokeo yaliyopita kwa asilimia kubwa chama hiki kilipata matokeo mazuri maeneo ya mjini na hizi ndio sehemu ambazo wananchi wengi wanapata huduma za msingi kama habari, huduma za kijamii kama hospitali, elimu na mengineyo ila kwa maeneo ya vijijini inaonekana kabisa kuwa chama hiki bado hakijafanikiwa kupata wafuasi katika maeneo hayo, ni kosa kubwa kwa chama kama Chadema kujidanganya na namba ya watu wanaokuja kwenye mikutano badala ya kujivunia namba ya wanachama mlionao katika eneo fulani.

Tuliona kwenye uchaguzi uliopita Chama Cha Mapinduzi kikijivunia mtaji wa wanachama na ndio maana ilikuwa ni ngumu kuwashawishi baadhi ya watu kuwa Chadema ilishinda kwa sababu walikuwa na mapokezi makubwa ya wananchi kwenye mikutano, tunasahau kuwa kwenye mikutano ni sehemu ambazo wananchi huenda kusikiliza sera za wagombea bila kubagua chama na kwa nchi kama ya kwetu ambapo kampeni hutawaliwa na burudani kama muziki na maigizo ni ngumu kugundua ni kitu gani haswa wananchi walifuata kati ya kampeni au burudani.

Uchaguzi ulipita na kwenye siasa tunasema mwisho wa uchaguzi mmoja ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine hivyo kwa kuwa tupo katika kipindi cha mwanzo kabisa sasa nafikiri ni muda kwa Katibu Mkuu wa chama hiki kuzunguka akikinadi ili wajipatie wanachama ambao wataenda nao kama mtaji kwenye uchaguzi wa 2020 kuliko kusubiri matukio yatokee bungeni na wabunge wa upinzani wayashikie bango ili yawapaishe kisiasa, huko vijijini kuna watu watajengewa hospitali halafu watashangilia kuwa tumejengewa hospitali kwa sababu hawafahamu kuwa ile ni haki yao, watajengewa shule wataambiwa mnaona tumewajengea shule nao watashangilia kwa sababu hawajui kama ile ni haki yao, watapelekewa umeme watashangilia bila kujua kuwa ni stahiki yao sasa kutokana na hayo anahitajika mtu atakayeenda kuwaambia kuwa huduma za kijamii kama shule, hospitali, umeme na barabara hizi ni huduma za msingi kwa wananchi na ni wajibu wa Serikali kuwapatia wananchi wala si zawadi kama wananchi wanavyodhani, lakini nani atawaambia wakati chama kipo mjini huku kikisubiri kuandaa maandamano ya chama yatakayofanyika mjini?

Ni ujinga kujidanganya kuwa vyombo vya habari vinatosheleza kwenye upatikanaji wa taarifa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, yawezekana kweli taarifa zinafika lakini Je, una uhakika kuwa taarifa kuhusu chama chako zinafika kule? Je, ni taarifa chanya? Maana hata taarifa hasi nazo ni taarifa na Je, unapataje mrejesho? Siasa ni kama biashara na wananchi ndio wateja na bidhaa unayoiuza ni chama chako hivyo ili kupata wateja ni lazima ujitoe kwenye kukitangaza ili watu wapate kuifahamu vyema bidhaa mnayoiuza, nafikiri vyama pinzani vyote vinafahamu nguvu ya chama tawala kwenye kueneza propaganda hivyo ni lazima vyama vijihakikishie kuwa vinajitenganisha na taarifa zozote ambazo zinaweza kupelekea kushuka kwa thamani ya bidhaa yao.

Chama kihakikishe kimezunguka sehemu mbalimbali kujielezea na kujipambanua, kwenye ulimwengu wa leo taarifa zina nguvu (Information is Power). Ukishawapatia taarifa nafikiri ni rahisi kupata wanachama ambao watageuka na kuwa rasilimali watu ambao chama kitaweza kuwatumia kwa njia mbalimbali maana chama ni taasisi, chama kinahitaji kujihakikishia kuwa kina wanachama wa kutosha wa kuwapatia kura zitakazowapa ushindi, wanachama hao hao pia watakuwa kama chanzo cha mapato ya chama, chama kinahitaji kuwa na watu ambao watawatumia kwenye njia mbalimbali za kusuka mbinu za ushindi, chama pia kinahitaji watu ambao watatumika kwenye ngazi ya utawala lakini watu hawa wote watapatikana endapo mtanadi chama chenu.

Chama hakitakiwi kusubiri nguvu ya mgombea ndio iwaokoe hapana, ni lazima chama kiwe kimesimama imara ili hata mgombea au mwanachama ambaye anaonekana ana nguvu atakapoondoka bado chama kitabaki imara, waangalie CCM waliondokewa na Lowassa japo walionekana kuyumba lakini chama bado kipo, leo hii unaweza kujiuliza kwa mfano Lowassa asingeenda Chadema na kusingekuwa na Ukawa ina maana Chadema wangekuwa peke yao Je, kwa mfano Dk. Slaa angeondoka kipindi karibu na uchaguzi ni mgombea gani wangemleta ambaye angeuzika kiurahisi? Bado chama kina kazi kubwa ya kufanya.

Salamu zangu kwa Katibu Mkuu wa chama Dk. Vincent Mashinji, kama kweli mna mpango wa kushika dola basi ni lazima mchukue hatua za dhati, siku si nyingi Chama Cha Mapinduzi kitaenda kuwa chini ya Rais Magufuli hivyo msitarajie upinzani mlioupata miaka ya karibuni kuwa ule ule, wazungu wana msemo wao unasema hivi “To be the best you have to beat the best” tafsiri  “Ili uwqe bora ni lazima umshinde aliye bora” na ili uwe bora ni lazima uwe umejiandaa sawa sawa maana safari ya mafanikio haihitaji njia ya mkato.

Nawasilisha.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles