Kupunguza mishahara ni mawazo ya kimasikini

maguuliKUNA  watu ambao wameonyesha kufurahishwa na azma ya Rais Dk. John Magufuli kupunguza mishahara ya baadhi ya watendaji wa taasisi za umma.

Furaha yao hiyo inatokana na kile kinachoelezwa kuwa watu hao wanalipwa fedha nyingi sana ukilinganisha na watumishi wengine wa umma.Kwa hiyo, watu wanaona ni bora na wenzao wanaolipwa zaidi wapunguziwe ili wafanane vipato. Sikubaliani nao.

Siku zote nitaendelea kuamini kuwa Mtanzania anastahili kulipwa fedha nyingi kutokana na kazi anayoifanya. Siku zote nitaendelea kuamini kuwa moja ya njia kubwa za kupambana na umasikini wa kipato ni kuwalipa Watanzania mishahara ambayo itawawezesha kumudu gharama za maisha.

Siku zote nitaendelea kuamini kuwa kufikiria kuwalipa watu mishahara midogo ni mawazo ya kimasikini ambayo chimbuko lake ni ufinyu wa kufikiri njia na namna ya kuboresha mapato ya taasisi ili ziweze kulipa mishahara mizuri.

Athari ya hilo ni kuwa na jamii ambayo kipato chake hakiwezi kumudu gharama za maisha, jambo ambalo tunalishuhudia hivi sasa.

Mwaka jana, kuliibuka kilichoitwa kashfa dhidi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TDPC) kuwa walikuwa wamepanga kujilipa mishahara mikubwa.

Ilinishangaza sana pale watu wengi walipolipinga hilo wakati kila siku ya sherehe za Mei Mosi tumekuwa tukishuhudia madai ya ongezeko la mishahara zikianikiza na kuchukua sehemu kubwa ya ujumbe mkuu katika sherehe hizo.

Kila siku kilio cha Watanzania kimekuwa ni kudai ongezeko la mishahara wakidai kuwa mishahara wanayolipwa hivi sasa haiendani na gharama za maisha.

Lakini katikati ya madai hayo, bado watu wanashabikia azma ya Rais Magufuli kupunguza mishahara ya baadhi ya watumishi wa umma.

Hata kama fedha zitakazopunguzwa kwenye mishahara hiyo zitapelekwa kuongeza mishahara ya wale wanaolipwa kidogo, bado haitasaidia sana kwa sababu hakutakuwa na kigezo cha ziada cha kudai nyongeza zaidi ya mishahara iwapo watumishi wote watakuwa wanalipwa kidogo.

Hivi sasa, zaidi ya gharama za maisha, kigezo kingine kinachotumiwa kwenye madai ya nyongeza za mishahara ni kukua kwa pengo kati ya wale wanaolipwa zaidi na wale wanaolipwa kidogo.

Mimi nilidhani moja ya njia bora za kupunguza pengo hili ni kuacha kuwaongezea wale wanaolipwa zaidi na kuwaongezea wale wanaolipwa kidogo ili angalau wawakaribie wale wa juu ili wafanane fanane.

Sidhani kama kuwapunguzia wale wanaolipwa zaidi ni njia mwafaka kwa sababu itawafanya nao walipwe kidogo. Si ajabu baada ya muda nao wakajiunga kwenye kundi la wale wanaodai ongezeko la mishahara.

Iwapo watu watakubaliana na hatua ya kuwapunguzia mishahara wale wanaolipwa zaidi, hata kama wale wanaolipwa kidogo wakiongezewa, baada ya muda mfupi watabaini kuwa ongezeko hilo haliendani na kupanda kwa gharama za maisha, hapo wataanza kudai tena nyongeza za mishahara lakini mara moja watakuwa wameondokewa na kigezo cha pengo la kipato kwa sababu wale wanaolipwa zaidi watakuwa wamepunguziwa mishahara yao na kuwiana na wale wanaolipwa kidogo.

Kwa maana nyingine, kufurahia na kushangilia watu kupunguziwa mishahara ni kufurahia na kushangilia kufifia kwa juhudi za kudai mishahara bora kwa watumishi.

Nadhani kinachowasukuma baadhi ya watu kufurahia azma ya kuwapunguzia baadhi ya watumishi wa umma mishahara ni wivu wa kijinga. Kama watu tungekuwa na wivu wa maendeleo, kiwango hicho cha mishahara ya baadhi ya watumishi wa taasisi za umma ambao tunaamini wanalipwa vizuri kingekuwa ni kigezo kwetu na chachu ya kuona na sisi tunafikia kiwango kama hicho au kinachokaribiana nacho.

Mathalani, naamini kabisa kuwa hao wanaosemekana kulipwa vizuri zaidi wanalipwa kwa sababu utendaji wao na ufanisi wa shughuli za taasisi zao unawezesha kulipa mishahara ya aina hiyo.

Wakati watu wanashangilia na kufurahia kupunguzwa kwa mishahara hiyo hawajiulizi ni kwa namna gani taasisi hizo zinamudu kuwalipa watendaji wake mishahara hiyo minono.

Na ukiangalia karibu taasisi zote ambazo zinatajwa kuwa watendaji wake wanalipwa mishahara mikubwa, zinafanya vizuri katika eneo lao husika.

Kamwe watu hawakitumii hicho kama kigezo katika sehemu ambazo nao wanafanya kazi ili kuhakikisha kuwa na wao wanaongezewa mishahara na kuwafikia wale wanaowaonea wivu hivi sasa.

Ninaamini kuwa iwapo kila mtu atajituma kwenye eneo lake na kuifanya taasisi anayoitumikia ikazalisha zaidi, itasaidia na kuleta tija sana katika madai ya nyongeza za mishahara kuliko kuonea wivu  mishahara ya watu wengine. Suluhisho la kudumu la mishahara midogo haliwezi kuwa kupunguza mishahara ya baadhi ya watu.

Lakini naamini pia kuwa suluhisho la kudumu la tatizo la mishahara midogo ni kuongeza tija na uzalishaji katika sehemu ambayo mtu anafanya kazi.

Sijui itamsaidia vipi mtu anayeplipwa mshahara mdogo iwapo yule anayelipwa mshahara mkubwa atapunguziwa. Sana sana tutakuwa tunaongeza idadi ya watu ambao watakuwa wanalalamika kuwa mishahara haitoshi kwa sababu hata kama punguzo la wale wanaolipwa sana litapelekwa kwa wale wanaolipwa kidogo, sidhani kama kutakuwa na ongezeko kubwa la mishahara katika kada za chini kwa sababu wale waliosemekana kulipwa sana ni wachache sana.

Kushangilia kupunguzwa kwa mshahara wa mtu mwingine, hasa anayelipwa zaidi kuliko wewe ni sawasawa na kujipiga nyundo utosini mwenyewe kwa sababu kiwango unachoshangilia ndicho ambacho Serikali itakitumia kama kikomo hata pale inapokadiria mshahara wako.

Na uzoefu unaonyesha kuwa ni vigumu sana kwa Serikali kukubaliana na kupandisha mshahara. Kwa hiyo, azma hii ya kushsusha mishahara kwa upande mwingine inalenga kuisaidia Serikali kupambana na madai ya nyongeza za mishahara.

Na kwa bahati mbaya, watu ambao wanapaswa kushadidia kuongezwa kwa mishahara wametekwa na hatua za Serikali na sasa wamekuwa ni mashabiki wa mishahara kushuka.

Serikali itawashangaa sana watakapoanza kudai nyongeza za mishahara. Na itakuwa na silaha ya kujitetea kwani nyie wenyewe, juzi juzi tu, mlishangilia hatua ya Serikali kushusha mishahara.

Narudia tena, njia bora ya kupunguza pengo la wanaolipwa vizuri na wale wanaolipwa kidogo ni kuwaongezea wale wanaolipwa kidogo ili wawakaribie wale wanaolipwa vizuri. Kumbuka kuwa lengo la kila mfanyakazi ni kulipwa vizuri.

Inashangaza sana iwapo mfanyakazi anashangilia mwenzake kupunguziwa mshahara ili walingane kulipwa kidogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here