29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Dk. Slaa: Magharibi hawatatuheshimu   kama tutapiga magoti kila siku

slaa* Asema ni heri tufunge mikanda

Na Elizabeth Hombo

TANGU Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) litangaze kusitisha msaada wake wa zaidi ya Sh Trilioni moja kwa serikali ya Tanzania na zaidi kundi la nchi wahisani zipatazo 10 zitangaze kujitoa kuchangia bajeti ya mwaka huu, Taifa limebaki njia panda.

Kumekuwa na maoni tofauti, juu ya uamuzi huo ambao unaelezwa kutokana na kukiuka misingi ya demokrasia hasa katika suala la Uchaguzi wa Zanzibar, na sheria ya makosa ya mitandao (Cyber Crime Act).

Wakati wabobezi wa masuala ya kiuchumi wakisema uamuzi huo unaweza kuitikisa nchi, baadhi ya wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali wanasema ni heri tufunge mikanda tujitegemee.

Mjadala ni mkubwa  na ama kwa hakika unaweza kusema umeliacha Taifa njiapanda.

Kutokana na hilo, MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano ya moja kwa moja kutoka nchini Canada aliko msomi, mwanasiasa aliyepata kushika wadhifa wa Ukatibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibrod Slaa. Yafuatayo ni mahojiano kamili;

SWALI:  Unadhani kitendo cha Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) kuifutia Tanzania msaada wa zaidi ya Sh. Trilioni moja utaathiri Taifa?

Dk. Slaa:  Ni dhahiri Kitendo cha ” kuifutia misaada ya MCC” kitaathiri Taifa. Kwa muda mrefu mipango yetu imekuwa ikitegemea fedha na Misaada ya Wahisani.

Aidha kwa muda mrefu Bajeti yetu ya Serikali Kuu, na kwa kiasi kikubwa pia Bajeti ya Hamashauri zetu zimekuwa Tegemezi.

Mwalimu Nyerere aliiona na kuonya zamani sana jambo hilo. Wabunge mbalimbali kwa nyakati tofauti, na hasa kuanzia Bunge la 8 wamekuwa wakipiga kelele Serikali zetu ( zote 2) . Zipunguze utegemezi huo. Kimsingi hatua zimekuwa zikichukuliwa.

Nikilinganisha na wakati nilipokuwa Mbunge ambapo utegemezi ulikuwa karibu ya 80% kwa bajet ya Matumizi (Recurrent Expenditure) na karibu ya asilimia 95 hadi asilimia  takriban 40 ya sasa ni hatua kubwa sana. Lakini naamini haitoshi, kwani “uhuru” kamili ni kuwa na uwezo na uhuru wa kupanga na kutumia fedha na rasilimali zako kwa jinsi unavyotaka uhuru huu bado hatunao.

 

Unadhani hizi ni sababu za msingi walizotoa kwamba ni kutokana na uchaguzi wa Z’bar na sheria ya makosa ya mtandao (Cyber Crime)?

Dk Slaa: Kimsingi, mimi sipendi kuzungumzia sana msingi wa maamuzi yao, nje ya zile hoja ambazo wamezitoa. Kwa mambo makubwa kama haya nisingilipenda kuwa ” mganga wa kienyeji kuanza kubadhiri sababu halisi.

Lakini ni ukweli kuwa kwa muda mrefu nchi za magharibi zimekuwa zikihusisha sana misaada yao na mambo kama “hali ya Demokrasia” na  “Utawala bora” katika nchi zinazoitwa ” Nchi zinazoendelea” (Developing Countries).

Nchi yetu siyo tu imeweka Saini bali pia imeridhia Mkataba wa Cotonou ( zamani Lome convention wa 1975) kati ya nchi, wakati ule 12 za Jumuia ya Ulaya kwa Upande mmoja na Nchi 77 za Afrika, Caribean na Pacific kwa upande mwingine. Msingi mkubwa wa Misaada inayotokana na mkataba wa Cotonou kama ulivyosainiwa Mauritius, ni hali ya Demokrasia katika nchi husika.

Mkataba huo bado unaendelea hadi leo,japo mambo mengi yamekuwa yakiamuliwa kwa msingi wa ushirikiano wa kikanda (EPA).Nakumbuka,  wakati nikiwa mwakilishi wa Bunge la JMT  katika Bunge la ACP/EU ( joint Assembly) moja ya hoja kubwa iliyojitokeza ni ” nini hasa tafsiri ya neno Demokrasia na Good Governance”. Mpaka nimemaliza kipindi changu hoja hiyo ilikuwa haijapata Tafsiri sahihi kwakuwa falsafa ya nchi za magharibi na nchi za ACP zilikuwa hazifanani.

Hivyo, mimi sipendi kuzungumzia msingi wa hoja yao, nje ya sababu walizozitoa wao (MCC) na mimi sijaona sababu zingine. Hivyo sitaki kutabiri.

Kama hizo ndizo sababu za MCC basi ni ” application” ya principles ambazo wamekuwa wakizisema, na kwa nyakati mbalimbali wamekuwa wakijadiliana na Serikali ya Tanzania na nyaraka kuhusiana majadiliano hayo ziko nyingi, na nyingine niliisha zitoa hadharani huko nyuma.

 

SWALI:  Kutokana na hilo unadhani uamuzi huo unaweza kuiteteresha Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo?

Dk. Slaa: Ni kweli uamuzi wa kukosa mabilioni ya fedha kutoka kwa Wahisani mbalimbali wa Marekani na wa Ulaya unaweza kuwa na athari kubwa katika mipango yetu. Kwa kuwa kutatokea pengo katika Bajeti yetu.

Aidha pia kwa ” Taarifa  ya ndani isiyotoka ‘Research Desk ya Developing Nations’  wenzetu wa Mashirika ya Fedha ya Marekani na Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ( kama Taarifa hizo ni za kweli) wameiweka ( listed) Tanzania kama ” Risky investment destination”.

Kwa kawaida listi ya aina hii ina maana ya kuwa, siyo tu mashirika ya kiserikali kama MCC na Misaada baina ya nchi kwa nchi kwa ilivyo kwa ‘Bajet Support” na aina mbalimbali za “Basket Funding” zitaathirika, bali pia ” Private Sector” ya Tanzania na za Nje zinaxofanya kazi Tanzania hazitaweza  ku ” access ” fedha kutoka kwenye Taasisi za Fedha za nchi za ulaya na North America.

Kimsingi hakuna kikwazo ” Rasmi” cha kiuchumi bali mashirika ya Nje kama ya utafutaji wa Mafuta, Gesi, Uranium na madini yote kwa ujumla, yatashindwa kufanya kazi kwa kukosa fedha. Kutokana na ” masharti magumu” ya kupata fedha hizo kama ilivyo sasa. Aidha biashara itadorora na hata utalii hatimaye utadorora kwa kuwa utakuwa ghali sana.

Lakini Mimi naamini, kuwa tuko kwenye ulimwengu ” unaoojiita wa kidemokrasia”. Tunafuata misingi ya International Law. Bila kuingia kwenye uhalali au kutokuwa halali uchaguzi wa Zanzibar, ambapo a ” Sovereign” country ” Taifa uhuru kwa mujibu wa Sheria ya Kimataifa” imefanya maamuzi. ..”

inayoamini ni kwa mujibu wa Sheria zake”, maamuzi hayo ( kama hayakuvunja sheria zingine za kimataifa kama genocide, ( ambayo historia inaonyesha walifumbia macho wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda), wanapaswa kuheshimu uamuzi wa Taifa huru ambayo imetekeleza matakwa ya Sheria zake( rejea juu nilipoeleza ( Tunapotofautiana katika Tafsiri ya Good Governance na Democracy.

Hawana haki kabisa ku ” impose” (kushinikiza) matakwa yao. Na ndio maana ninavyoona, wamechukua njia tofauti ya ” kuzuia misaada na kutu “list” kama nilivyoeleza hapo juu. Haya mambo mawili yanatofautiana sana na effect zake ni pia tofauti.

Kwa kutambua kuwa Taifa huru, halipaswi kutetereka kama inaamini ilifanya maamuzi yake kwa mujibu wa sheria zake na ” inaamini” kwa dhati hakuna ” haki za msingi” ( sizungumzii ‘political rights!) bali ” human Rights”.

Tuna mifano mingi huko nyuma.

1) Mwalimu Nyerere aliipa Taifa moja kubwa masaa 48( kama nakumbuka vizuri) kuondoka na makontena yao ya misaada yaliyokuwa Bandarini Dar es Salaam, kwa kuwa tu walitaka kutuchagulia ‘Marafiki’ . Hatua ilituumiza kwa muda kwa kukosa ile misaada, lakini ilijenga heshima ya Utu wetu Watanzania na dunia nzima ikatuheshimu, na kwa muda mrefu hatukuchezewa tena na Taifa lolote la nje.

2) Afrika ya Kusini wakati wa ubaguzi wa Rangi (apartheid) siyo tu ilinyimwa misaada bali iliwekewa vikwazo vya kiuchumi. Na hapa pia nieleweke sizungumzii uzuri au ubaya wa apartheid policies bali nazungumzia ” uamuzi halali” wa Taifa huru kwa mujibu wa sheria zake.

Tofauti na wengi wanavyofikiri, Afrika Kusini walifunga mikanda yao kulinda Sovereignity na autonomy yao kama Taifa. Matokeo yao walijenga uchumi imara, walikuza rasilimali watu yao na kupata wanasayansi bora duniani (succesful heart transplant ya kwanza duniani ilifanyika Afrika ya Kusini na Daktari Kabouroo! Leo wana viwanda vya magari, wana heavy industries, wana ndege za kutosha. Kimsingi wanashindana na Ulaya na Marekani.

Wanaogopwa na kuheshimika. Hatutafikia hatua hiyo iwapo kila wakati tutapaswa kupiga magoti. Wao pia wanahitaji “Resources” tulizonazo, ni suala la muda tu. Watarudi wenyewe bila kubembelezana. Watakaporudi tutaheshimiana kwa kuwa wakati huo na sisi tutakuwa tumejenga uwezo wetu.

Hii habari ya kuwauzia ” raw materials” kisha “finished products” zinarudi kwetu kwa bei ambayo asilimia 90 ya watu wetu ( yaani wale waliozizalisha) hawawezi kununua bidhaa hizo ni lazima ifike mahali tuseme basi. Inahitaji ” Bold decision” ( maamuzi magumu yasiyoyumba).

Kusimamia rasilimali zetu vizuri, tuwatumie walio tayari kutusaidia ” wakati wa shida” kama ambavyo tayari wako wenye nia njema wamejitokeza, ila na wao wasituletee masharti yasiyo na kichwa wala miguu.

Kwani mara ya kwanza China kututoa kwenye shida. Watanzania tumesahau wakati wa mapambano ya ukombozi ” Marekani alivyokataa kutusaidia ” ujenzi wa barabara ya ukombozi”- ujenzi wa Barabara na reli ya Tazara na barabara – kama sijakosea ( Tanzam). Zambia ingelikuwa imeumia sana kama si kwa ujenzi wa reli ya Tazara wakati wa ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Cuba mbona haijaangamia kwa kuwekewa vikwazo na Marekani kwa miaka yote hiyo? Juzi Obama si ameenda likizo mwenyewe, nadhani kwa kujialika mwenyewe ( it was not an official state visit). Heshima haiji kwa kuomba omba inakuja kwa kuchukua maamuzi magumu.

 SWALI: Unadhani nchi itaweza kuendelea bila misaada na kwamba tutaweza kujetegemea ndani ya muda mfupi?

Dk. Slaa: Kinachodumaza nchi ni mawazo ya viongozi wake na wananchi wake. Kinachoendeleza nchi si misaada ni jinsi Taifa linavyojisimamia. Canada ina pupulation karibu sawa na Tanzania. Kila barabara ina flyover, sisi leo tukiona daraja pale ubungo tunashangaa.

Walienda kuomba wapi? Kodi zao, rasilimali zao- mafuta, mbao, mazao ya kilimo yalifanya kazi. Yalisimamiwa vizuri. Uwanja mdogo tu wa mkoa kwa siku kuna flight minimum 2000. Reli na bandari zinaleta bidhaa mpaka Dar es Salaam.

Watu wao wanalipa kodi kwa wakati bila shuruti. Kulipa kodi ni heshima (ni kweli watu wana moyo wa kulipa kodi kwa kuwa wanaona matunda ya kodi zao.

Huduma muhimu zote; afya ni bure, elimu ni bure mpaka equivalent ya form VI yetu. Kwetu sisi hela za kodi sehemu kubwa inaishia mifukoni mwa watu.

Wakianza “kutumbuliwa” tunalalamika badala ya kuunga mkono anayewatumbua, jambo ambalo miaka yote haikutokea.

Hivyo ninaamini tuko kwenye njia sahihi, tukikaza uzi, tukaziba mianya yote bila huruma, kila chombo kikafanya kazi kwa mujibu sheria. Tutaweza kujenga uchumi wa heshima. Lazima kuwe na ” Zero Tolerance” kwa ufisadi, uwizi wa mali za umma na rasilimali zote za Taifa.

Tuondoe vyeo mbalimbali vya ” ulaji” vilivyotengenezwa kwa ajili ya Maswaiba, kila nafadi ya kazi haina sababu ya kujaziwa watu, kazi inayofanywa na mtu mmoja haina sababu ya kufanywa na watu

Tujifunze kinachoitwa ” lean Management”, najua wako watakaopiga kelele kwa sababu tumejijenga kwenye utamaduni wa kulindana.

Mbona wenzetu wameweza wana nini kuliko sisi? Ingekuwa Tanzania ishushwe kwa siku mbili tu, na ardhi yote nchi nzima ifunikwe na barafu, kwa hali yetu tutafilisika mara moja.

Lakini wenzetu kila  wakati wako barabarani ” kuondoa barafu tu” na heavy equipment. Sisi hata mafuriko ya siku moja tunaangamia na kulia.

Tunahitaji kubadili mtindo wetu wa kufanya kazi na kujituma hasa vijana, ambao wengi wamejenga utamaduni wa kukesha kwenye mitandao wakipiga propaganda au kwenye ” pool” wakiambiwa inakuwa “noma” nchi haijengwi kwa miujiza isipokuwa kwa kazi, na kila mmoja kutumiza wajibu wake mahali alipo.

Tukifika hapo hatutatetereka, na tusipofika hapo tumlaumu Magufuli kwa kuwa yeye siyo “omnipotent kama Mungu.

Aidha tusiposimama kama Taifa katika jambo kama hili, tatawaliwa tena kama ” Donald Trump” Mgombea urais wa Republican ( USA) anavyotabiri sahihi.

Siamini Watanzania tuko Tayari kutawaliwa na mgeni yeyote yule kwa sababu yeyote ile, na hasa siyo kwa sababu tumeamua kuendekeza uwizi, ufisadi au kwa  kuwa tunaendekeza ” anasa” badala ya ” kufanya anasa” baada ya kazi kama wenzetu wanavyofanya.

Ukienda mitaa ya Baa, bia zimejaa utadhani sisi ndio matajiri kuliko Marekani au Canada. Tuna mihela kwa ajili ya bia, lakini hatuna hela kwa ajili ya kusomesha watoto wetu. Tuondoe hii laana na aibu kwa kubadili Tabia zetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,220FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles