24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YAFUMULIWA

Mwenyeketi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli akifungua kikao cha kwanza cha Halmashauri Kuu (NEC).
Mwenyeketi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli akifungua kikao cha kwanza cha Halmashauri Kuu (NEC).

Na BAKARI KIMWANGA, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, amefanya mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho.

Chini ya mabadiliko hayo, Rais Dk. Magufuli amesema anataka kukifanya chama hicho kiongozwe na wanachama badala ya kuongozwa na mwanachama mmoja.

Rais Dk. Magufuli alitangaza mabadiliko hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, tangu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Julai mwaka huu mkoani Dodoma.

“Tunaposema juu ya mabadiliko tunataka tuyafanye na ni lazima tukubaliane. Sisi katika Kamati Kuu, tumekubaliana na tumeyapitisha nanyi naamini mtafanya hivyo.

“Ili kuweza kwenda na hali hiyo, kuanzia sasa wajumbe wa NEC watapungua kuliko ilivyo sasa. Hata na mimi nimeguswa, zamani nilikuwa nateua wajumbe 10 wa NEC, lakini sasa wamepungua wamebaki saba.

“Wapo wasaliti hasa nyakati za uchaguzi na kutokana na hali hii ninapenda kupongeza kamati za mikoa na wilaya kwa kuwachukulia hatua wasaliti wote.

“Chama ngazi ya chini kiwe imara na nitafurahi kuwa na wajumbe wachache katika vikao vya juu kwani lazima tuendeshe chama kwa mujibu wa kanuni za chama chetu zinazoeleza mwanachama kuwa na nafasi moja ya uongozi kuliko ilivyo sasa.

“Vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye katiba, vyote tunaviondoa na mfano halisi ni nafasi ya mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, makamanda na walezi.

“Nafasi hizo hazijatamkwa kwenye katiba yetu na pia ni lazima jumuiya za chama zifanye kazi kwa kuzingatia katiba ya chama chetu kwa kuwa na kanuni zinazokwenda na matakwa ya katiba,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Kuhusu mikakati ndani ya chama, alisema umebaki mwaka mmoja kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wa ndani ya chama hicho na kusema maandalizi ya kuwapata viongozi bora yanatakiwa kuanza.

“Mchakato huo unaanza hivi karibuni kuanzia Februari mwakani na kukamilika Novemba. Hapa tunatakiwa kuwa na wagombea wazuri watakaopanga timu nzuri ya ushindi.

“Hakikisheni hakuna mapandikizi, kuweni na wajumbe halali kwani hao ndiyo watakaoruhusiwa kushiriki uchaguzi kwa sababu tukigundua kuna mapandikizi, tutafuta uchaguzi wote,” alisema Rais Magufuli.

AWAJIBU WAPINZANI

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli aliwajibu baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani waliopinga uamuzi wake wa kufanyia Ikulu mikutano ya kisiasa.

Rais Magufuli alisema, hakuna wa kumpangia mahali pa kufanyia mkutano wa kisiasa  ukiwamo mkutano wa NEC.

“Nimelazimika kufanyia kikao hiki hapa Ikulu kwani inamilikiwa na Watanzania wote na si ajabu kwa CCM kuwapo hapo kwani ndiyo waliopewa ridhaa na Watanzania.

“Sioni ajabu kuwakaribisha wana CCM Ikulu kwani hapa ni kwenu na ni kwa Watanzania wote. Ila kama kuna vyama vingine vinataka kufanya mikutano hapa, viombe na wakija ni lazima tujue ajenda zao na tutawasikiliza.

“Kufanyia vikao hapa haitakuwa mara ya mwisho na hakuna mtu atakayenipangia nikafanyie wapi vikao.

“Kamati nyingi zimefanyika Ikulu, mabalozi wanakuja Ikulu na hata wao wanapokuwa na shida zao wanakuja Ikulu, cha ajabu ni nini?” alihoji Rais Dk. Magufuli.

Akizungumzia vipaumbele 10 vya mabadiliko ndani ya CCM, alisema katika uongozi wake, anahitaji kuwa na chama imara kwa ngazi zote na chenye uwezo wa kuisimamia Serikali kwa vitendo na si kuwa na chama legelege.

“Chama ni wanachama ni lazima tuongeze idadi ya wanachama wapya hasa vijana na si kuwa na wanachama hewa.

“Upo mtindo unapofika kwenye uchaguzi ndiyo tunakuwa na wanachama ambao ni wa mkakati na baada ya hapo hawaonekani, hili hapana.

“Rushwa ndani ya chama chetu ni miongoni mwa mambo yanayosemwa hasa nyakati za uchaguzi.

“Katika hili sitakuwa na msamaha na watoa rushwa. Ni lazima chama chetu kijenge tabia ya kujitegemea kiuchumi, haifai na ni aibu kwa chama kutegemea ruzuku au watu binafsi kukisaidia.

“Lazima rasilimali za chama zitumike inavyotakiwa kwa kunufaisha chama na wanachama wake,” alisema.

KINANA ANENA

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema kikao hicho cha NEC kinafanyika kikiwa na wajumbe halali 388 lakini kutokana na sababu mbalimbali waliohudhuria ni 355.

Kwa mujibu wa Kinana, NEC inafanyika kuelekea miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM na miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika pamoja na zaidi ya miaka 50 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles