
Na Mwandishi Wetu, Tabora
BAADHI ya vijana wanaofanya shughuli za kusafirisha abiria kwa pikipiki maarufu ‘, jana walijitokeza kwa wingi katika hoteli aliyofikia Waziri Mkuu Mstaafuwa zamani, Edward Lowassa mjini Tabora kumweleza hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema yupo mkoani Tabora katika ziara ya na viongozi wengine wa chama hicho kufanya vikao vya ndani na wanachama wao katika mikoa mbalimbali nchini.
Lowassa ambaye katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana aligombea urais kupitia muungano wa vyama vya Ukawa, alivamiwa na waendesha bodaboda hao jana asubuhi.
Walimweleza namna wanavyokabiliwa na ugumu wa maisha, mfumuko wa bei za bidhaa katika mkoa huo unavyowaathiri katika uchumi, kukosekana kwa mzunguko wa fedha huku wakisema wanafanya kazi katika mazingira magumu.
“Tunakabiliwa na hali ngumu ya maisha, fedha haipo mtaani, hali imekuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya mwisho wa mwaka,”alisema mmoja wa vijana hao.
Vijana hao pia walimweleza Lowassa kuwa wamekuwa wakinyang’anywa vyombo vyao vya kufanyia kazi na waajiri wao kutokana na tofauti za siasa.
Hata hivyo, Lowassa aliwaambia vijana hao kuwa Tabora ni miongoni mwa mikoa yenye historia ya siasa kutokana na kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa serikali ya awamu ya kwanza ambao walifanya harakati za siasa.
“Tabora ni kitovu kikubwa katika historia ya siasa za nchi hii baada ya kuwapo wazee hodari katika siasa kama vile Hashim Mbita, hivyo endeleeni kuwaenzi wazee hawa na kuifanya Tabora kuwa kisima cha siasa kwa kuijenga na kuiimarisha Chadema,”alisema Lowassa huku akiwasisitiza kuwataka kuwa jasiri na kujipanga mara mbili zaidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ziara hizo za Chadema ni mwendelezo wa operesheni maalum iliyopewa jina la ‘Kata Funua’ ambayo inatekelezwa nchi nzima kwa viongozi wakuu wa chama hicho kutumia mikutano ya ndani kukutana na wanachama wao.
Katika ziara hizo, wajumbe wote wa Kamati Kuu na baadhi ya wabunge wa chama hicho wametawanywa katika mikoa mbalimbali kufanya mikutano ya ndani kuimarisha chama na kupanga mikakati ya ushindi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na ule mkuu 2020.
Katika mikutano hiyo, viongozi hao wamekuwa wakijadili matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana na kuangalia kasoro zilizojitokeza na jinsi ya kupambana na CCM katika uchaguzi huo ujao.