25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CASH MADAME NI JIBU LA DUME SURUALI?

mg_2594

Na FESTO POLEA,

JUNI 7, 1988 mwanadada, Vanessa Mdee ‘Vee Money’ alizaliwa. Uwezo wake wa kipekee wa kufikiri tofauti na kufanya mambo kwa umahiri mkubwa ndiko kunakomweka tofauti na watu wengine katika kazi zake mbalimbali ikiwemo uandishi wa nyimbo, ujasiriamali, uigizaji, utangazaji wa runinga na redio pamoja na uimbaji.

Mwanadada huyo mzaliwa wa Arusha aliyewahi kutangaza kwa mafanikio kwenye kituo maarufu cha runinga cha MTV, shindano la Bongo Star Search na kipindi cha Dume Condom kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Cash Madame’ uliozua maswali mengi kama ni jibu la wimbo alioshirikishwa wa ‘Dume Suruali’ wa msanii Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ aliyezaliwa mwaka 1984.

Kwanini ni jibu?

Nyimbo hizi mbili zinahisiwa kuwa ni jibu kutokana na ujumbe wake ambapo ‘Dume Suruali’ unamzogoa mwanamke mpenda fedha huku ‘Cash Madame’ ukimpa ujasiri mwanamke apende zaidi fedha.

Baadhi ya maneno ya Mwana Fa katika wimbo wa ‘Dume Suruali’ ni ‘Nihonge nanunua nini kwanini yani kuna kipi nisichokijua ina tv ndani…’, ‘usipende ela kama mfuko au fanya ufanyavyo upate zako…’, ‘Na ujifunze pesa zinauza utu wako…’, ‘Unapenda ela zangu nami nazipenda pia kila mtu abaki na zake…’, ‘Na ukiniomba kesho unisikii tena kwani unauza nini dada…’.

Vanessa naye anaanza kwa kuimba ‘Dharau na pesa mi sitaki, eti mimi dada wa ku-party nasikia nina wengi mashuga dady, sipigi kazi niwie radhi’

Vanessa kuhusu Cash Madame, Dume Suruali

“Hapana si jibu la ‘Dume Suruali’ wimbo wa ‘Cash Madame’ niliurekodi Desemba mwaka jana na nimeutoa Desemba mwaka huu lakini huu wa ‘Dume Suruali’ nilioshirikishwa na Mwana FA tuliurekodi Agosti mwaka huu, ni mawazo tu yamegongana kutokana na ujumbe wake mmoja kuelezea wanawake mwingine kuelezea wanaume,” anafafanua Vanessa.

Vanessa anaongeza kwamba wimbo wa ‘Dume Suruali’ ulipotoka uliwaumiza baadhi ya wanawake walioona kama wanasemwa vibaya na wanaume kutokana na ujumbe uliopo katika wimbo huo hivyo alipotoa wimbo wake wa ‘Cash Madame’ wanawake wengi waliufurahia wakiona kama amewajibia.

Kisa cha Cash Madame?

Vanessa anaeleza kwamba kisa cha kuandika wimbo huo kinatokana na kudhulumiwa kwake na mmoja wa mwaprodyuza wenye majina makubwa Afrika.

“Kuna prodyuza mkubwa Afrika Mashariki alinidhulumu fedha zangu, kisa kilikuwa hivi, tulikubaliana anilipe kiasi fulani cha fedha lakini akawa anasumbua wakati mimi nikiwa nimeshafika ukumbini, mashabiki wengi wa Afrika Mashariki walihudhuria, nilifikiria mengi niliona ningegoma ningewakera na kuwapoteza mashabiki wangu wengi, niliamua kupanda jukwaani niliamini angenilipa baada ya shoo lakini haikuwa hivyo, alinidhulumu hapo ndipo nilipopata wazo la kuandika wimbo huu nikipinga dhuluma kwa wasanii hasa wa kike,” anaeleza Vanessa.

Anasema wimbo huo aliuandika kwa ajili ya wanawake wote wapiganaji akiwatia moyo waendelee kupigana katika kusaka haki zao na wasikubali kudhulumiwa licha ya vikwazo mbalimbali wanavyokutana navyo huku wakiamini kwamba Mungu ni wetu wote.

“Nimewatia moyo sana ndiyo maana mstari wa kwanza wa wimbo huo nimesema: ‘Dharau za pesa mi sitaki…,’’ anaeleza.

Wanenguaji wake

Kuhusiana na wanenguaji wake anasema huwa anaishi nao kama ndugu, aliwashauri wasiache kazi wanayoifanya ndiyo maana kwa sasa wapo nchini Marekani kwa kazi hiyo hiyo ya unenguaji inayowaingizia fedha nyingi za kujikimu na maisha yao.

“Wale ni ndugu zangu, naishi nao kama wadogo zangu, baada ya kumaliza upigaji picha za video yangu ya ‘Cash Madame’ jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini chini ya mwongozaji Justin Campos, wamekwenda Marekani kwa kazi yao itakayokamilika Januari mwakani ndiyo watarejea nchini,” anaeleza Vanessa.

Aliingiaje kwenye muziki?

Mwaka 2012, Vanessa alijiunga na studio ya B’Hits wakatoa wimbo alioshirikishwa na msanii mwenye mafanikio makubwa nadni na nje ya Afrika, Ambwene Yessayah, aliyezaliwa Julai 5, 1981 huko mkoani Mtwara.

Baadaye akashirikishwa pia na msanii Ommy Dimpoz katika wimbo wa ‘Me and You’ ambao aliutendea vyema na ukamwonyesha njia ya mafanikio katika uimbaji ikiwemo wimbo wa ‘Siri’, ‘Hawajui’, ‘Closer’ hadi hivi sasa.

 Vitu alivyoshiriki

Vanessa ameshiriki vitu vingi vikiwemo kampeni ya kupinga malaria. Mwaka 2008, akiwa balozi wa Alive Foundation alitembelea Uwanja wa fisi akiwa na balozi mwenzake, Kelly Rowland.

Mwaka 2009, alikuwa mtangazaji Tamasha la Sauti za Busara International Music Festival na mwaka 2011 alikuwa mtangazaji wa kituo cha redio kijulikanacho kama Choice Fm ambapo aliwahi kufanya mahojiano na wasanii mbalimbali akiwemo, Kelly Rowland, Mac Miller, Rick Ross, Ludacris na wengine wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles