NA RAYMOND MINJA, IRINGA |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini, kimesema Mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Peter Msigwa ajiandae kisaikolojia kuachia jimbo hilo.
Chama hicho kimesema hali hiyo inatokana na wimbi là madiwani wa Chadema waliohama na baada ya uchaguzi mdogo wamepoteza kata zote.
Katika uchaguzi mdogo uliomalizika hivi karibuni, CCM kilifanikiwa kuchukua kata tano bila kupingwa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Iringa, Joseph Mgongolwa alisema ushindi walioupata ni salamu tosha kwa Mchungaji Msigwa kujitafakari na kuangalia kazi nyingine ya kufanya kwa sababu hatarudi mwaka 2020.
Alisema sasa umefika muda wa kuwatumikia wananchi wa Iringa na si muda wa kufanya siasa zisizotekelezeka na za kupiga kelele majukwaani.
Alisema wana Iringa wa sasa ni watu wanaohitaji mabadiliko na maendeleo, lakini kumekuwapo na watu wanaokwamisha juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, hivyo ni vema wakaacha siasa.
“Ule muda wa kupiga kelele umekwisha, sasa ni vitendo, Watanzania wamechoka kudanganywa… wana Iringa wamechoka ahadi hewa, wanataka mabadiliko,”alisema.
Alisema umefika wakati wa kufanya siasa za kutenda zaidi kuliko siasa za vijembe na matusi ili kumkomboa Mtanzania.