CHADEMA YALIA KUHUJUMIWA SIMIYU

0
928

Na ANDREW MSECHU, Dar es Salaam                        |                             


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelalamika kufanyiwa hujuma katika kata mbili mkoani Simiyu.

Hiyo ni baada ya wagombea wake kunyimwa fomu za kukata rufaa baada ya majina yao kuenguliwa kwenye uchaguzi juzi usiku.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema wagombea hao ni wa Kata ya Tindabuligi, Zunzu Ndatulu Humu na wa Kata ya Kisesa, Shanemhanga Mabula Makonge wilayani Meatu, wamenyimwa fomu za kukata rufaa baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi.

“Jitihada za wagombea hao na viongozi wa chama kupata fomu hizo namba 12(c) kwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza, hadi sasa (jana jioni) hazijafanikiwa.

“Hiyo ni  baada ya msimamizi huyo kutoonekana ofisini tangu asubuhi tofauti na alivyokuwa amewaahidi na kuwataka wafike kwake wachukue fomu hizo. Hata simu zake ambazo alikuwa anapokea hadi jana usiku, hazipatikani,” alisema.

Alisema wagombea hao walirejesha fomu zao kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi katika kata hizo Jumatatu  Agosti 20, mwaka huu.

Alisema hadi kufikia jioni juzi,   mgombea wa Kata ya Tindabuligi alikuwa hajawekewa pingamizi lakini ghafla saa 1.30 usiku aliarifiwa kuwa amewekewa pingamizi na akapewa barua ya kuenguliwa kwenye uchaguzi.

Makene alisema taarifa za awali zilieleza kuwa mgombea huyo pamoja na viongozi wa chama walipohoji kuenguliwa bila haki ya kujibu mapingamizi yaliyowekwa, waliambiwa hakuna fursa hiyo.

Alieleza kuwa taarifa hizo zilidai kuwa kitendo hicho kilifanyika mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi) pamoja na maofisa wakuu wa vyombo vya dola ngazi ya wilaya waliokuwapo ofisini kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.

Alisema katika Kata ya Kisesa, mapingamizi yaliwekwa saa 4.00 asubuhi juzi, siku moja baada ya kurejesha fomu na yalijibiwa na mgombea kabla ya  kurejeshwa kwa wakati juzi, lakini ilipofika   2.30 usiku naye aliarifiwa kuwa ameenguliwa kwenye uchaguzi.

Makene alisema jitihada za wagombea wote kuwataka Wasimamizi Wasaidizi wawapatie fomu namba 12(c) kwa ajili ya kukata rufaa zilishindikana kwa kile kilichodaiwa kuwa fomu hizo hazikuwapo bali zilikuwa zinapatikana kwa Msimamizi wa Uchaguzi.

Alisema walipowasiliana na Msimamizi wa Uchaguzi juzi usiku, aliwataka wafike ofisini kwake jana  awapatie hizo fomu waweze kukata rufaa, lakini hadi jana jioni hakuonekana ofisini na simu zake za mkononi hazikuwa hewani.

Alisema katika Kata ya Mwanhuzi ambayo inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio, msimamizi msaidizi alikataa kuzipokea fomu za mgombea wao, baada ya kuzipitia na kuzihakiki, akisema kuwa zipelekwe leo, Alhamisi, Agosti 23 ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kurejesha fomu na kufanya uteuzi wa wagombea katika kata hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here