Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limeiondoa timu ya Biashara United katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushindwa kutokea uwanjani siku ya mchezo wake wa marudiano na Al Ahly Tripoli ya Libya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), wamepokea barua kutoka CAF leo Novemba 3,2021, inayosema uamuzi wa kuiondoa timu hiyo umefanya na Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo.
“Katika uamuzi wake, CAF imeeleza kuwa sababu zilizoifanya Biashara United kushindwa kwenda Libya kucheza mechi hiyo ya hatua ya pili ya raundi ya awali hazikutokana na dharura.Mechi hiyo ilikuwa ichezwe Oktoba 23,2021 jijini Benghazi, Libya,” imesema taarifa hiyo.
Mchezo wa kwanza timu hizo zilipokutana Oktoba 15,2021 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Biashara United iliibuka na ushindi wa mabao mawili.