23.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

Aweso aitaka Exim kutoa kibali kuharakisha mradi wa maji miji 28

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amekutana na uongozi wa Benki ya Exim India kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28 ambao ni moja ya miradi iliyopangwa kutekelezwa na Serikali.

Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Maji, Mji wa Serikali Jijini Dodoma kwa lengo la kukamilisha taratibu muhimu na kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.

Waziri Aweso ameushukuru uongozi wa Benki ya Exim India kwa kusafiri kuja nchini mahsusi kukutana na Serikali ili kuona utekelezaji wa mradi huo unaanza, na kusema mpango wa Serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi inafika asilimia 95 katika maeneo ya mijini na asilimia 85 vijijini.

Amewataka Benki ya Exim kuhakikisha wanatoa kibali haraka ili mikataba ya ujenzi wa mradi wa miji 28 isainiwe kwa sababu kibali hicho kimechelewa kutolewa kwa muda mrefu.

Amesema India ni moja ya washirika wakubwa wa Sekta ya Maji na kielelezo ni mradi mkubwa wa maji wa Tabora – Igunga – Nzega uliogharimu Sh bilioni 600, na wananchi zaidi ya milioni 1.2 wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Aweso ameainisha kuwa Wizara ya Maji si kikwazo katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma ya maji, na lengo la Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani katika kona zote za nchi.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema wanufaika wa mradi huo wanasubiri kuona kazi inaanza na viongozi wamejipanga kuratibu kazi mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, amesema japo mradi huo umechukua muda kuanza kupitia vikao vinavyofanyika hivi sasa matarajio ya kuanza kwa mradi huo ni makubwa.

Ujumbe wa Benki ya Exim India umeongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Gaurav Bhandari, aliyesema uhusiano kati ya India na Tanzania ni mkubwa na wa muda mrefu na kuahidi kampuni bora zitatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini.

Mradi wa maji wa miji 28 unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 500 ikiwa ni zaidi ya Sh trilioni moja ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles