29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE LAMUWEKA KIKAANGONI KIGWANGALLA

NA ESTHER MBUSSI-DODOMA


BUNGE limemuweka kikaangano Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala likitaka aundiwe kamati ndogo ya kibunge itayochunguza hatua mbalimbali anazochukua katika ofisi yake.

Rai ya kuundwa kwa kamati hiyo, ilitolewa jana bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kemilembe Lwota alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati yake.

Akisoma taarifa ya kamati yake, Lwota alisema uchunguzi huo uwe wa kujiridhisha kama mikakati inayochukuliwa na serikali ya kugawa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada imesaidia kuongeza pato la taifa.

Waziri Kigwangala amekwishafuta leseni zote za umiliki wa vitalu kwa mwaka 2018-2022 zilizotolewa na wizara hiyo kabla hajapewa dhamana ya kuiongoza kwa kile alichoeleza kuwa mchakato wa kuzitoa haukuzingatia taratibu.

Oktoba 22, mwaka jana, Kigwangala alitangaza kufuta umiliki wa vitalu vyote vya uwindaji na kitalii vilivyotolewa Januari 16, 2017 akieleza hatua hiyo inasaidia kupisha mfumo mpya wa ugawaji vitalu hivyo kwa njia ya mnada.

Jana, Lwota aliliambia Bunge wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake kuwa ilikutana na wadau na kupokea malalamiko yao kuhusu hatua zinazochukuliwa na  Waziri Kingagwala na kwamba serikali inapaswa kufahamu biashara ya utalii inahitaji umakini mkubwa, hivyo mabadiliko madogo yanaweza kuiathiri.

“Ni biashara inayohitaji muda kujipanga, kuitangaza na kuwapa imani watalii na wawekezaji katika sekta hii.

“Kamati inaishauri serikali kuangalia upya mfumo mzima wa ugawaji wa vitalu vya uwindaji nchini kwani ni eneo ambalo limelalamikiwa sana na wadau, kutokuwa na mfumo thabiti na mabadiliko ya mara kwa mara yamelikosesha taifa mapato kwa vile watalii wa uwindaji wamesitisha safari zao mara nyingi kwa sababu ya kukosekana kwa uhakika wa biashara hii.

“Kwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ametangaza kufuta leseni zote za vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria na kusababisha taharuki katika tasnia ya uwindaji. Na kwa kuwa hatua hiyo imeondoa utulivu na kuwafanya wawekezaji kusita kuendelea kuwekeza katika vitalu kwa kukosa uhakika wa kuvimiliki na baadhi ya wawindaji wa kitalii kusitisha safari zao, mapato yatokananyo na uwindaji wa kitalii yameshuka.

“Kamati inalishauri Bunge kuunda kamati maalumu itakayochunguza changamoto zilizoko katika tasnia hii na kuishauri serikali ipasavyo,” alisema Lwota.

Pamoja na mambo mengine, alisema mwenendo wa mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii unaonyesha yameshuka kutoka Dola za Marekani milioni 23.5, mwaka 2010 hadi kufikia Dola milioni 11.2 mwaka 2015.

Wakati Waziri Kigwangala akifuta vibali hivyo, alisema mchakato wa vibali alivyofuta ulijaa rushwa na upendeleo.

Alisema ufutaji huo unatoa nafasi ya kurekebisha sheria na kanuni kabla ya kuanza mchakato mpya ambapo waliokuwa na vibali vya zamani uhai wake unaisha uliisha Desemba 31, mwaka jana.

“Kimsingi mchakato wa vibali nilivyovifuta haukuwa halali kisheria, ulijaa rushwa na upendeleo na haukuwa wa kimkakati kwa sababu mpango wa Taifa wa miaka mitano (2016 – 2021) na matokeo makubwa sasa (BRN) unaelekeza twende kwenye njia ya mnada,” alisema Kigwangala.

Uamuzi mwingine wa Kigwangala ulioibua malalamiko ni kuwasimamisha kazi baadhi ya maofisa wa hifadhi kwa tuhuma za rushwa.

Aidha, hivi karibuni aliwatuhumu baadhi ya viongozi kuwa wana viwanja kwenye kiwanja cha moja ya taasisi za wizara yake kilichopo Arusha.

 

UJANGILI

Pamoja na mambo mengine, Lwota alisema ilitaarifiwa kuwapo kwa mbinu mpya ya ujangili inayotumiwa na majangili kwa kutumia sumu kuua wanyama pori.

Alisema mbinu hiyo ni hatari kwa uhifadhi kwani si tu inaua wanyama wengi bali pia inaua na wanyama wasiokusudiwa.

“Aidha, majangili wamekuwa wakibadili mbinu za usafirishaji wa nyara za taifa mara kwa mara hivyo kusababaisha kazi ya kuwadhibiti kuwa gumu.

“Kamati inaishauri serikali kubadili mbinu za kupambana na majangili kwa kuongeza vifaa vya mawasiliano, silaha za kisasa na kuunda kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kupambana na ujangili na kutumia kikosi chake cha Intelijensia kubaini mtandao wa ujangili wa Tembo nchini ili kuokoa rasilimali hii muhimu iliyo hatarini kutoweka,” alisema.

 

MPANGO WA KUENDELEZA JIJI LA ARUSHA

Lwota alisema kamati imeshtushwa na gharama zilizotumika kuandaa mradi wa mpango kabambe wa kuendeleza Jiji la Arusha kwa kutumia wataalamu elekezi kutoka nje ya nchi.

 

Alisema mradi huo unagharimu Dola za Marekani milioni 6.81  na hadi sasa serikali imekwishalipa Dola milioni 3.332, sawa na asilimia 54.8 ya gharama ya mpango.

“Kamati inashauri kuwa katika mipango ya kuendeleza majiji mengine, serikali ijielekeze kutumia wataalamu wa ndani kupunguza gharama.

“Aidha, kamati inaliomba Bunge liitake serikali imalize deni lililobakia ili kuwezesha mpango huo kukamilika, kuidhinishwa na kuanza kutekelezwa,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles