24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, July 7, 2024

Contact us: [email protected]

BoT yaendelea na Ukomo wa Riba ya Asilimia 6 kwa Robo ya Tatu ya Mwaka 2024

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendelea kwa ukomo wa riba ya asilimia 6 kati yake na benki za biashara nchini kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024. Riba hiyo itatumika kuanzia Julai 4 hadi Septemba mwaka huu.

Akisoma taarifa hiyo leo, Julai 4, jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana wa BoT (Sera za Uchumi na Fedha), Dk. Yamungu Kayandabila, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Totuba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, alisema uamuzi huo umefanikiwa katika kikao kilichofanyika Julai 3, 2024.

Tathmini ya kamati kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia 5.

“Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania imeamua riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoisha Septemba mwaka huu,” alisema Dk. Kayandabila.

Amesema maamuzi ya kamati yamezingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia ambapo matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia.

Kamati hiyo inatarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi na upatikanaji wa chakula cha kutosha pamoja na kupungua kwa kasi ya kushuka thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kutokana na shughuli za utalii, pamoja na mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula.

“Katika tathmini ya mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati imebaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024. Mfumuko wa bei unaendelea kupungua na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na benki kuu katika nchi nyingi zimeanza kupunguza viwango vya riba.

Hata hivyo, bei ya mafuta ghafi imeongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi Juni 2024 huku bei ya dhahabu ikiendelea kuwa juu, ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama uwekezaji mbadala katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali kutokana na migogoro ya kisiasa duniani,” alieleza Dk. Kayandabila.

Amesema matarajio ni uchumi wa dunia kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024 na 2025, pamoja na kuwepo kwa hatari ya kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mizozo ya kibiashara.

Kuhusu mwenendo wa uchumi nchini, kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi.

Akizungumzia kushuka kwa thamani ya sarafu, Dk. Kayandabila alisema kwa Tanzania, thamani ya sarafu imeshuka kwa kiasi kidogo sawa na asilimia 11, tofauti na nchi zingine ambazo zimerekodi kushuka kwa thamani ya sarafu kwa asilimia 30. Mfumuko wa bei nchini Tanzania na Uganda ni mdogo, chini ya asilimia 5, ikilinganishwa na asilimia 20 hadi 50 katika nchi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles