Nyemo Malecela -Kagera
DEREVA wa bodaboda Mugisha Theonest, amepigwa na kusababishiwa mauti baada ya bodaboda mwenzake, Frank Kafumba aliyekuwa akigombea nae abiria kumsingizia kuwa alitaka kumpora pikipiki.
Tukio hilo lilitokea Machi 3, mwaka huu saa 12 jioni, wakati Mugisha na mwenzake, Erick Cosmas wakitoka kupeleka abiria eneo la Ranchi ya Kagoma, wakati wanarudi Kayanga Karagwe ndipo walikuta abiria wengine njiani wakimsubiri Kafumba (bodaboda), aliyekuwa ameitwa kutoka Katagwe na abiria hao, lakini amechelewa kufika na kuamua kuwapakia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, alisema wakati Mugisha na Cosmas wakiwa njiani na abiria hao, walikutana na Kafumba ambaye alianzisha ugomvi, akidai arudishiwe gharama za mafuta aliyotumia, lakini hawakuelewana.
Alisema kuwa Kafumba aliamua kuwafuata wanakoelekea na walipofika kituo cha mwisho, ugomvi ukawa mkubwa na kuanza kupigana.
Kamanda Malimi alisema kuwa kuwa Kafumba aliamua kupiga simu kwa bodaboda wa kijiwe chake kuomba msaada kuwa anataka kuporwa pikipiki yake.
“Baada ya kuomba msaada kwa bodaboda wenzake na wananchi wengine walifika na kuanza kumpiga Mugisha na kumsababishia majeraha yaliyosababisha kulazwa hospitali ya Nyakahanga kwa matibabu, lakini kwa bahati mbaya alikuwa ameumia vibaya na kusabisha kifo chake ambacho kimetokea Machi 5, mwaka huu,” alisema Kamanda Malimi.
Alisema uchunguzi ulibainika Mugisha na mwenzake, Cosmas hawakuwa wezi au hawakuwa na nia ya kumpora pikipiki Kafumba kama ilivyodaiwa, bali ugomvi wao ulisababishwa na kugombea abiria. Kamanda Malimi alisema tayari mtuhumiwa amekamatwa na wengine waliohusika wanaendelea kusakwa ili wachukuliwe hatua kwa kosa la kujichukulia sheria mkononi