29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

BODABODA ACHENI MSEMO WA PONDA MALI KUFA KWAJA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


KAMA kawaida safu hii huwa inakuletea taarifa kuwahusu wadau hawa wa sekta ya usafirishaji ambao kila kukicha hawaishiwi na vituko.


Ingawaje kundi kubwa linalojihusisha na biashara hii ni vijana ambao awali walikuwa ama wanajushughulisha na biashara nyingine au hawakuwa kabisa na kazi ya kufanya na hivyo kujikuta wakishinda vijiweni.


Serikali ilikuja na wazo hili la kuruhusu aina hiyo ya usafiri ili kupunguza idadi kubwa ya vijana waliokuwa wakishinda vijiweni na kupuliza sigara kali, kunywa pombe na kukaba watu ovyo kutokana na kukata tamaa ya maisha.


Lakini kadri muda unavyokwenda, tunashudia kundi kubwa la watu wazima nao wameamua kujikita katika biashara hii.


Siku moja nikiwa kwenye kituo cha daladala Mbezi kwa Msuguri nilisikia kauli ya mmoja wa madereva hao ambaye ana umri unaokaribia utu uzima akisema; “Jamani maisha yanakwenda mbio, siku kweli hazigandi… na mimi najiona naelekea utu uzima sasa lakini cha kusikitisha bado sijaweza kujimudu kimaisha kiasi cha kuja kukaa kijiweni na kuendesha bodaboda na vijana wadogo.


“Lol! inabidi nijizatiti sasa kuanza kujipanga kuachana na biashara hii maana kwa jinsi vijana wanavyokua na wengine wanabebesha mimba watoto wa watu ovyo, unaweza kujikuta unaendesha bodaboda na wajukuu zako, wenzangu tujipange.”


Vijana waliokuwa wakimsikiliza mzee huyo baada ya kauli hii ya mwisho walijikuta wakiangua kicheko huku wengine wakisikika wakimzodoa mzee huyo kwamba anapaswa aende kupumzika na kuwaacha wao wafanye kazi.


Ingawa vijana wale waliishia kumcheka na kumzodoa, ukweli ni kwamba alitoa somo kubwa kwao ambalo leo nimeona nitumie nafasi hii kufikisha ujumbe kwa bodaboda wote nchini.


Idadi kubwa ya vijana wanaojishughulisha na biashara hii wamekuwa hawana malengo endelevu ya kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadae.


Wengi huwa wakishapata fedha za kumpa bosi wake au zao wenyewe, basi huishia kuzitumia kwenye starehe hasa ile ya kunywa pombe hususan ‘kiroba’.


Wenyewe huona fahari kutumbua fedha kwa matumuzi yasiyokuwa ya lazima na kushindwa kabisa kutafakari kwa ajili ya maisha yao na familia zao hapo baadae.


Utagundua hili pindi utakapokaa nao karibu na kupiga stori mbili tatu, utasikia wanakuambia ponda mali kufa kwaja suala  hili huwa linanisikitisha.


Ingawa si wote wenye tabia hii lakini wengi wao wapo na msimamo huu wa kukusanya fedha na kuzitumia hadi ziishe na kisha kwenda kutafuta nyingine siku ijayo.


Nimalize kwa kusema kwamba waendesha bodaboda wanapaswa kubadilika na kuanza kujipanga ili kuja kufanikisha maisha yao ya baadae isije ikafika wakati umri ukiwa umewatupa mkono wakajikuta hawakujiandaa katika kukabiliana na maisha yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles