28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

JIWEKEE MALENGO YANAYOTIMIZIKA ILI KUFAIDIKA NA MAZOEZI

Dk. Fredirick L Mashili, MD,PhD.


HAKUNA ubishi kwamba mazoezi yanatakiwa kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Tafiti zinaonyesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara hutufanya wakakamavu na kutukinga na maradhi chungu nzima.

Licha ya kwamba wengi wetu tunalifahamu hilo, na hata kujaribu kuanza program ya mazoezi, utakubaliana name kwamba wako wengi ambao hushindwa kuendelea na program hizo. Mojawapo ya kitu kinachosababisha kushindwa huku ni kutokujiwekea malengo, au wakati mwingine kujiwekea malengo yasiyotimizika.

Leo tutajadili jinsi ya kujiwekea malengo yanayo timizika tunapoanza program ya mazoezi.

 

Jipange na ujiandae kuandika kila kitu

Unapotaka kuanza program ya mazoezi usikurupuke. Hakikisha unajiandaa kwa kupanga muda na kuwa na vitu vyote vinavyohitajika kama nguo na viatu vya mazoezi. Licha ya wengi wetu kupuuzia hili, ni vema kuwa na notebook ambayo itakusaidia kupangilia mazoezi yako na kurekodi kile unachokifanya. Hii itakusaidia kufuatilia maendeleo yako.

Fanya vipimo muhimu mwanzo wa program yako

Hii inategemea sana na kile unachokitaka au lengo lako kuu la wewe kuanza. Huenda unataka kupunguza uzito, kuongeza ukakamavu au labda unataka kujikinga na magonjwa. Kama nia yako ni kupunguza uzito hakikisha unapima uzito na urefu mwanzo kabisa wa program yako. Vipimo hivi vitakusaidia kukokotoa uwiano wa uzito na urefu au kwa lugha ya Kiingereza body mass index (BMI). Kufahamu uzito na BMI yako kabla ya kuanza program kutakusaidia kufuatilia maendeleo yako. Unaweza pia kupima kiasi cha mafuta mwilini.

 

Kwa wale wenye nia ya kuongeza ukakamavu au fitness, wanashauriwa kupima kasi ya mapigo yao ya moyo wakiwa katika hali ya utulivu kabisa (resting heart rate). Katika hali ya kawaida kasi ya mapigo ya moyo hupungua kadri mtu anavyozidi kuwa mkakamavu au fit. Kama nia yako ni kuimarisha afya ya moyo na mfumo wake (cardiovascular health) hakikisha unafanya vipimo kama vile shinikizo la damu (blood pressure) na kufahamu kiwango cha lehemu (cholesterol) katika damu yako. Kumbuka hii ni mifano tu lakini viko vipimo vingine vingi vitakavyokusaidia kufuatilia maendeleo yako.

 

Pata ufahamu wa jinsi mazoezi yanavyo fanya kazi

Ili usiwe na mategemeo yasiyo na ukweli, unashauriwa kupata ufahamu wa jinsi mazoezi yanavyofanya kazi. Ni vema kujisomea kwanza au kuongea na mtaalamu ambaye atakuelezea ni nini cha kutegemea kutoka katika program yako.

 

Usitegemee miujiza

Kuwa mkweli katika malengo. Usitegemee kupungua kilo tano ndani ya wiki moja, au usitegemee kuufanya moyo wako kuimarika ndani ya wiki moja. Ukweli ni kwamba, kama ni mara yako ya kwanza  kuanza mazoezi usitegemee mabadiliko yanayopimika katika wiki ya kwanza ya programu. Kwa maana hiyo, unashauriwa kupima tena uzito wako baada ya wiki mbili. Hapo unaweza kuona mabadiliko kidogo kutokana na jinsi ulivyojituma. Cha muhimu fuata ushauri wa wataalamu na jifunze kuhusu muda unaotakiwa kuleta mabadiliko fulani.

 

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,085FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles