KAMPALA, UGANDA
JESHI la Polisi limemweka katika kizuizi cha nyumbani mwanamuziki na Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.
Jeshi lilichukua hatua hiyo saa kadhaa baada ya kutangaza mpango wake wa kuandamana hadi polisi kupinga ukatili dhidi ya matamasha yake ya muziki na wanasiasa wa upinzani.
Aliwataka Waganda wote wenye hasira kuungana naye katika mapambano dhidi ya ukosefu wa haki.
Polisi walisema lengo la uamuzi wao ni kumzuia mwanasiasa huyo wa upinzani kufanya mikutano iliyo kinyume cha sheria.
“Hizo zilikuwa ni hatua zilizochukuliwa chini ya sera ya kuzuia ili kulinda sheria na utulivu wa umma wakati bado anatishia kufanya mikutano kinyume cha sheria.
“Maofisa wetu wa ujasusi watatusaidia kumpata na tutaweza kuona ni nini kitakachofuatia. Hili limekuwa suala la usalama wa taifa,” alisema Msemaji wa Polisi, Fred Enanga.
Awali Bobi Wine alikuwa ametangaza mpango wa kufanya maandamano ya umma kote nchini kupinga hatua ya polisi kuendelea kuzuia matamasha yake ya muziki na ukatili dhidi ya wanasiasa wa upinzani.
Alitangaza hatua yake alipokuwa nyumbani kwake Magere, Kasangati katika Wilaya ya Wakiso muda mfupi baada ya polisi kumzuia asubuhi kufika katika makazi yake ya ufukweni ya One Love Beach yaliyopo eneo la Busabala na kumwingiza katika gari la polisi na kumbwaga nyumbani kwake hapo.