NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema mageuzi na maboresho yaliyofanywa katika sekta ya madini, yamechangia kuongezeka kwa mapato kutoka Sh bilioni 196 hadi Sh bilioni 335 kwa mwaka.
Mageuzi hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa masoko ya madini, kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wachimbaji wadogo wa madini, kuondolewa kwa kodi ya zuio, uboreshwaji wa miundombinu na kanuni mbalimbali zinazosimamia sekta ya madini.
Akizungumza jana wakati wa mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini, Waziri wa Madini, Doto Biteko, alisema mageuzi hayo yamefanya mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa kuongezeka kwa kasi.
Mkutano huo una lengo la kuwakutanisha wadau wa madini katika nyanja tofauti, wakiwamo wanaochimba madini, wanaotengeneza na kuuza teknolojia, wenye mitaji na wasiyonayo na kutangaza fursa zilizopo katika sekta hiyo ili kuifanya iwe na tija kwa taifa.
“Zamani kulikuwa na urasimu, kupata leseni tu ilichukua zaidi ya mwaka, lakini leo mtu anaweza kupata kwa mwezi mmoja tu, Serikali inatamani kuona biashara ya madini inakuwa ya wazi na hakuna mtu anayesumbuliwa.
“Awali uchimbaji ulikuwa jambo la kificho, wachimbaji wadogo waligeuka kuwa vyanzo vya kufanya utafiti halafu wakigundua wanaondolewa kwenye maeneo, utaratibu wa kuwafanya wachimbaji wadogo waishi kwa presha hilo zilipendwa,” alisema Biteko.
Aliwataka wachimbaji kujenga utamaduni wa kulipa kodi bila kushurutishwa kwani si nia ya Serikali kutumia nguvu katika kudai kodi na tozo zingine.
“Sisi tunawategemea ninyi kuliko ninyi mnavyoitegemea Serikali, tulipe kodi itumike kubadilisha maisha yetu kwa sababu nchi bado ina mahitaji makubwa na hatuwezi kufanya kama hatuna rasilimali, na madini ndiyo rasilimali kubwa tuliyonayo,” alisema Biteko.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi na Wauzaji wa Madini Tanzania (Tamida), Sammy Mollel, alisema mabadiliko ya sheria yaliyofanywa mwaka 2017 yameleta faida kwa kufanikisha kuanzishwa kwa masoko ya madini.
“Asilimia moja ya Tasac (tozo za huduma za usafirishaji madini) ni tatizo na inaturudisha nyuma, tunaomba tozo ambazo bado ni kero ziondolewe ili tuongeze juhudi na hamasa kuongeza thamani ya madini kusaidia wachimbaji wadogo na wakubwa,” alisema Mollel.
Pia alishauri kuanzishwa kwa benki ya madini itakayosaidia wachimbaji na wafanyabiashara kupata mikopo yenye riba nafuu na kuwezesha sekta hiyo izidi kukua.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (Femata), John Bina, alisema karibu asilimia 80 ya changamoto zilizokuwapo sekta ya madini zimetatuliwa na kwamba sheria ya madini nayo imekuwa rafiki.
Mkutano huo ulioenda sanjari na maonyesho ya teknolojia ya uwekezaji na biashara ya madini, ni wa pili kufanyika baada ya ule uliofanyika Februari 22-23 mwaka jana na kukutanisha wadau wa madini kutoka nchi mbalimbali duniani.