Na JUSTIN DAMIAN, DAR ES SALAAM
WAKATI takribani benki sita zikishindwa kujiendesha na kuwekwa chini ya usimamizi maalumu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na nyingine kufungwa ndani ya miaka miwili, baadhi ya wachumi wamesema hayo yalikuwa yakitarajiwa.
Jana BoT ilitangaza kuiweka chini ya uangalizi Benki M baada ya kubaini ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.
BoT pia ilitangaza kuridhia muunganiko wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Benki ya Posta na kuwa benki moja itakayoitwa TPB Plc, huku ikiziruhusu Benki ya Wananchi ya Tandahimba (TACOBA) na Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) kuendelea na biashara baada ya kutimiza mashari ya kuongeza mtaji.
Januari 4 mwaka huu, BoT iliziongezea muda wa miezi sita TACOBA, TWB na KCBL ili kufikisha kiwango cha chini cha mtaji wa Sh bilioni mbili ambacho kwa mujibu wa sheria, ndicho kinachotakiwa kwenye benki za wananchi (community banks), muda ambao uliisha Julai 31, mwaka huu.
CHINI YA UANGALIZI
Matukio ya benki kuwekwa chini ya uangalizi, yalianza Oktoba mwaka juzi wakati Twiga Bancorp iliyokuwa ikimilikiwa na Serikali kwa kiasi kikubwa, iliwekwa chini ya uangalizi wa BoT kabla ya kuruhusiwa kuungana na Benki ya Posta Mei mwaka huu.
Januari mwaka huu, BoT ilizifutia leseni benki tano ambazo ni Covenant Bank, Benki ya Wananchi ya Meru, Benki ya Efatha, Benki ya Wananchi ya Njombe, Benki ya Ushirika wa Wakulima ya Kagera na mwezi Mei 2017 iliifutia leseni Benki ya Wananchi wa Mbinga kutokana na kutokidhi vigezo vya uendeshaji.
FAIDA YASHUKA
Gazeti moja linalochapishwa kwa lugha ya Kiingereza, juzi liliripoti faida inayotengenezwa na mabenki kushuka kutoka Sh bilioni 438 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 423 mwaka juzi na Sh bilioni 286 mwaka jana.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, jumla ya benki 40 za biashara zilizosajiliwa nchini, kwa pamoja zimepunguza wafanyakazi 381 hadi kufikia Juni mwaka huu.
WACHUMI WANENA
Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi, aliliambia MTANZANIA kuwa kushuka kwa faida na baadhi ya mabenki kushindwa kujiendesha kutokana na kutokidhi kigezo cha mtaji, kulitarajiwa kutokana na kutolewa kwa mikopo isiyolipika.
Profesa Moshi alifafanua kuwa kuwapo kwa mikopo isiyolipika ambayo ndiyo chanzo cha benki kushindwa kujiendesha na kupungua kwa faida, kunatokana na udanganyifu mkubwa uliokuwa unafanywa na wakopaji, wakati mwingine wakishirikiana na wafanyakazi wa benki wasiokuwa waaminifu.
“Ilikuwa ni jambo la kawaida mkopaji kuweka dhamana mali isiyokuwa ya kwake.
“Mteja alikuwa anakula njama na baadhi ya wafanyakazi wa benki wasio waaminifu na kisha kupiga picha nyumba isiyo yake na kupeleka nyaraka za uongo na kupewa mkopo.
“Inapofika ameshindwa kulipa mkopo, benki ndiyo inagundua kuwa imedanganywa,” alisema.
Mhadhiri huyo alisema sababu nyingine ya kuwapo kwa mikopo isiyolipika, ni baadhi ya wateja kuongeza thamani dhamana wanazoweka kwa ajili ya kupata mikopo.
“Utakuta mteja anasema nyumba anayoiweka kama dhamana ina thamani ya Sh milioni 100, lakini thamani halisi ni Sh milioni 50, anaposhindwa kulipa, benki inakuwa imepata hasara,” alisema Profesa Moshi.
Alisema usimamizi dhaifu ndani ya mabenki ndiyo chanzo kikuu cha kuwapo kwa mikopo isiyolipika, huku akielezea matumaini yake kuwa mambo yataanza kubadilika kutokana na usimamizi thabiti wa sheria.
“Kipindi cha nyuma hata BoT ilikuwa imelala kidogo. Kwa sasa imeamka na kuimarisha usimamizi kwenye mabenki na ndiyo maana haya yote yanaonekana hadharani.
“Kwa usimamizi thabiti kama huu, ni wazi kuwa huku mbeleni mambo yatakuwa mazuri,” alisema.
Profesa Samwel Wangwe ambaye ni mshauri wa uchumi anayefanya kazi na kampuni ya ushauri ya Daima Associate, alisema kufanya vizuri kwa mabenki kunategemea sana uimara wa uchumi.
Alisema kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, imekuwa na athari kwa wateja wa mabenki, hususani wakopaji na hivyo kushindwa kulipa mikopo.
“Sekta binafsi ambayo ni wakopaji wakubwa hawapo vizuri na hivyo utakuta wanashindwa kurudisha mikopo waliyoichukua na kuzifanya benki kupitia katika kipindi kigumu,” alisema.
Profesa Wangwe alisema pamoja na Serikali kushusha viwango vya riba, bado havijaweza kuwa na athari kubwa kwenye sekta ya fedha, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ili kuifanya sekta binafsi ifanye kazi kwa ufanisi.
Alisema mapendekezo yaliyotolewa na sekta binafsi kwa Serikali yanayojulikana kama ‘Blue Print’, endapo utekelezaji wake utafanyika utasaidia kuboresha utendaji wa sekta binafsi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi ikiwamo sekta ya fedha.
IDADI YA BENKI
Kwa mujibu wa tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuna benki 40 za kibiashara zinazoendesha shughuli zake nchini.
Benki hizo ni Accessbank (Tanzania) Ltd, Advans Bank (Tanzania) Ltd, African Banking Corporation (Tanzania) Ltd, Akiba Commercial Bank Plc, Amana Bank Ltd, Azania Bank Ltd na Bank M (Tanzania) Ltd ambayo jana ilitangazwa kuwekwa chini ya usimamizi.
Nyingine ni Bank of Africa (Tanzania) Ltd, Bank of Baroda (Tanzania) Ltd, Bank of India (Tanzania) Ltd, Barclays Bank (Tanzania) Ltd, Canara Bank (Tanzania) Ltd, China Commercial Bank Ltd, Citibank (Tanzania) Ltd, Commercial Bank of Africa (Tanzania) Ltd, CRDB Bank Plc, DCB Commercial Bank Plc na Diamond Trust Bank (Tanzania) Ltd.
Benki nyingine ni Ecobank (Tanzania) Ltd, Exim Bank (Tanzania) Ltd, Equity Bank (Tanzania) Ltd, FBME Bank Ltd, First National Bank (Tanzania) Ltd, Habib African Bank Ltd, I & M Bank (Tanzania) Ltd, International Commercial Bank (Tanzania) Ltd, KCB Bank (Tanzania) Ltd na Mkombozi Commercial Bank Plc.
Nyingine ni National Microfinance Bank Plc, NBC Bank Ltd, NIC Bank (Tanzania) Ltd, Peoples’ Bank of Zanzibar Ltd, Stanbic Bank (Tanzania) Ltd, Standard Chartered Bank (Tanzania) Ltd, Tanzania Postal Bank Ltd, Tanzania Women’s Bank Plc, TIB Corporate Bank Ltd, Twiga Bancorp Ltd, United Bank for Africa (Tanzania) Ltd na UBL Bank (Tanzania) Ltd.