Asha Bani-Dar es salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amewahakikishia wanachama wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) kuwa atasimamia na kuunda kamati maalumu itakayosikiliza na kutatua kero wanazopata wafanyabiashara kutoka kwenye taasisi zinazowahudumia ambazo zinazolalamikiwa kwa na urasimu.
Waziri Bashungwa alikutana na wanachama hao Dar es Salaam jana na kusikiliza kero zao zingine zilitolewa majibu na wahusika papo hapo, na zingine kuahidi kuzishughulikia.
Katika mkutano huo ambao ulikutanisha taasisi zinazowahudumia zikiwamo Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirikisho la Viwango Tanzania (TBS), huku wakurugenzi wa taasisi hizo wakiahidi kushirikiana na CTI kwa kutatua kero na kuwafanya wafanye biashara kwa mafanikio .
Baadhi ya wafanyabiashara hao, akiwemo Isack Lupokela kutoka kiwanda cha saruji cha Tanga alilalamikia masuala mbalimbali katika nyanja ya ulipaji wa kodi.
Hussein Kamote alizungumzia utaratibu unaokwaza wafanyabiashara katika upimaji wa ubora na TBS ambapo wakurugenzi wa taasisi hizo waliweza kuahidi kusimamia hilo na kuondoa kero hizo.
Waziri Bashungwa alisema amesikia changamoto  hizo zingine zikiwa zinahitaji sera na baadhi ya sheria kufanyiwa marekebisho.
Alisema atafanya hivyo ili kuleta tija katika viwanda na biashara zao.
“Zipo sheria na sera zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho ya muda mfupi na zingine muda mrefu lakini kwa sasa niwahakikishie kuwa nitafanya na kutatua changamoto zote zilizomo ndani ya uwezo wangu,”alisema.
Alisema lengo la Serikali ni kuona viwanda vya Tanzania vinaongezeka upatikanaji rahisi wa masoko ya biadhaa ndani na nje ya Tanzania,kuwapo na umoja ni kitu muhimu katika kufanikisha hayo.
Alisema takwimu zinaonyesha viwanda vya ndani vinazalisha chini ya uwezo wao, jambo ambalo ni hasara kubwa na halikubaliki.
Alisema Tanzania inapaswa kutumia fursa ya masoko ya nchi wanachama,ikiwamo Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema sekta ya viwanda inasaidia kuzalisha ajira na kuchangia kuwezesha maendeleo endelevu kwa kuimarisha viwanda vilivyopo na vipya kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mkutano huo, umelenga kuimarisha sekta ya viwanda kuweka mikakakati itakayowawezesha kumudu ushindani wa bidhaa kutokab nje.
Alitumia fursa ya mkutano huo kuwashauri shirikisho la wenye viwanda kutumia fursa ya mkutano huo kuangalia watakavyoweza kushirikiana na wenzao ili kuongeza wigo wao wa biashara.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kwanza wa CTI, Paul Makanza aliipongeza Serikali kuweka juhudi kwenye uwekezaji na kuahidi kama shirikisho watakua bega kwa bega kwa lengo la kufikia uchumi wa viwanda ifika 2025.
Naye Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi (TRA), Richard Kayombo, aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa kero zote zitatatuliwa,huku akiwataka kulipa kodi kupata risiti ya kielekrotiki itakayokuwa inaonyesha uhalali wa umiliki wa mali au biashara husika.
Alisema mamlaka imeweka mifumo mbalimbali ya ulipaji wa kodi lengo, likiwa ni kuhakikisha pia inazuia watu kuuza mali feki na kuipatioa faida Serikali kwa njia ya kodi.