23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe atangaza neema sekta ya umwagiliaji Shinyanga

Na Mwandishi wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Kilimo, Husein Bashe ametembelea mradi wa umwagiliaji wa Nyida uliopo mkoani Shinyanga wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC) na kuelekeza kuwa ndani ya mradi huo lijengwe ghala kubwa la kuhifadhi mpunga.

Waziri Bashe ameelekeza ufanyike ujenzi wa kituo cha pamoja cha kununua mpunga na kufungwa mashine na kinu cha kuchakata mchele,sambamba na ujenzi wa barabara ya uhakika yenye urefu wa km 7.5 itayoungana na barabara kubwa ya lami na kujenga pamoja na kujenga mabirika kunyweshea wanyama.

Waziri Bashe amesema hayo katika muendelezo wa ziara yake akiwa anakagua mradi wa Nyida uliopo mkoani Shinyanga.

Aidha Waziri Bashe ameelekeza kuongezwa kwa mradi mdogo wa Nyida wenye hekta zaidi ya 400 na skimu hiyo itangazwe hivi karibuni.

Amesisitiza kuwa skimu ya Nyida yenye hekta 400 itangazwe ili ipate mkandarasi na aanze kujenga ili wananchi wanufaike.

“Mradi huu ni ndoto za muda mrefu nilikuja mwaka 2020 na leo namshukuru Mungu tumekuja hapa kuangalia maendeleo namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha…mradi huu utakuwa na mabwawa matatu na ujenzi wa skimu nyingine ya Lyamalagwa yenye hekta 1500 ikiwa na mfereji mkuu km 12 na mifereji ya ndani yenye km zaidi ya 50,”amesema.

Amesema, anatambua rasiliamali fedha ni chache lakini Dk.Rais ameamua kutenga fedha za ujenzi wa miradi hiyo itakayohudumia halmashauri mbili ambayo ni Nzega DC na Shinyanga vijijini.

Waziri Bashe, amesisitiza kuwa bwawa hilo lenye ujazo Mita za ujazo milioni 7 na mfumo wa kutoa maji yanapojaa itasaidia kuepuka maji yanayofurika na kuharibu miundombinu ya barabara.

“Bwawa hili litatumia mifumo miwili kuhudumia wakulima wakati wa kiangazi yatatumika maji ya bwawa na wakati wa masika yatatumika maji ya mvua, hatua ambayo itawawezesha wakulima kulima mara mbili kwa mwaka,”ameeleza Waziri Bashe.

Amesema ujenzi wa miradi hiyo iliyoanza Nyida pekee serikali inatumia fedha za walipa kodi zaidi ya sh.Bilioni 55 sawa na vituo vya afya 100, ambapo ingejengwa barabara za lami ni zaidi ya km 50.

Ameeleza kutokana na hatua hiyo ujenzi huo ufanyike kwa kiwango kinachotarajiwa na utunzwe kwa maslahi ya wananchi wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla.

Waziri Bashe amesema Rais Dk. Samia ameamua kuboresha sekta ya kilimo, kutoa ruzuku za mbolea, mbegu, ruzuku za maindi na nyingine kwa lengo la kuinua wakulima kiuchumi.

“ Wakulima lipeni ada za huduma za umwagiliaji ili inapotokea kunahitaji marekebisho katika miradi mfuko wa umwagiliaji uwezi kufanya kazi yake,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, amesema Tume inaendelea na mpango wa kujenga mabwawa, kukarabati skimu za zamani na kuibua maeneo mapya kwa ajili ya kilimo.

“Mkoa wa Shinyanga una jumla ya skimu 14, sikimu nyingi zilijengwa muda mrefu na hivyo kuwa chakavu na nyingine kutokamilika ikiwemo Ishololo, Mwamashele, na Kahanga,”alisema.

Mndolwa amesema ujenzi wa bwawa la Nyida ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika April mwakani ambapo hadi sasa umefikia asilimia 68, ukijumuisha ujenzi wa mabwawa ya Katunguru Sengerema Mwanza na Kasoli,Bariadi Simiyu yote matatu yakiwa na gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 29.

Aidha kwa mwaka wa fedha 2024/2025 serikali kupitia Tume imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mabwawa saba na katika mabonde ya Lunguya, Mwamkanga, Amani, Ngaganulwa, Nimbo, Bulungwa na Kisuke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles