29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe aipongeza kampuni ya GAKI

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameipongeza Kampuni ya GAKI Investment Ltd inayomilikiwa na Gaspar Kileo kwa uwekezaji wake wenye tija katika sekta ya pamba, hususan kwa kuwa mwekezaji na mnunuzi wa pamba kutoka Kata za Mbutu, Kishapu, na Meatu. Pongezi hizo zilitolewa Septemba 12, 2024, wakati wa ziara ya Waziri Bashe katika kiwanda cha GAKI, mkoani Shinyanga.

Waziri Bashe alisifu ushirikiano wa kampuni hiyo na Bodi ya Pamba, ikiwemo kuajiri Maafisa Ugani 15 chini ya mpango wa BBT Ugani, ambao wamewawezesha wakulima wa kata hizo kuboresha uzalishaji wa pamba. Mpango huo umesaidia kuongeza mavuno kutoka kilo 200 hadi kilo 1,000 kwa ekari, hatua ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima.

Akizungumza zaidi kuhusu mpango wa BBT Ugani, Waziri Bashe alieleza kuwa utaratibu wa kutumia Maafisa Ugani katika zao la pamba umekuwa na mafanikio makubwa, ambapo kila kijiji kinapewa Afisa Kilimo mmoja ili kuwasaidia wakulima kuongeza ufanisi katika kilimo cha pamba. Programu ya BBT Ugani, ambayo ilianzishwa msimu uliopita, ina jumla ya wahitimu 230, na inalenga kuhakikisha kila zao linafuata utaratibu huo wa kutoa huduma za ugani.

Aidha, Waziri Bashe alibainisha kuwa Serikali imetoa trekta kwa kila kijiji ili kusaidia shughuli za kilimo na itaendelea kutoa ruzuku za mbolea na mbegu kwa wakulima. Huduma za ugani pia zitaimarishwa zaidi ili kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini.

Ziara hiyo pia ilihusisha viongozi wa Mkoa wa Shinyanga, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Anamiringi Macha, na wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles