22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Bao moja tu wakimataifa chali

SHABANI mtanzaniadaily .indd

JUDITH PETER NA ADAM MKWEPU

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu ya Yanga, jana walishindwa kudhihirisha kuwa wa kimataifa, baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa mabingwa wa Afrika, TP Mazembe, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Bao la Mazembe lilifungwa na mchezaji Merveille Bope katika dakika ya 73, hivyo kuifanya Yanga kupoteza mchezo wa pili hatua hii ya makundi, baada ya kufungwa katika mchezo wa kwanza bao 1-0 na timu ya Mo Bejaia ya Algeria Juni 19.

 

Mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki wengi zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka Tanzania, baada ya kutokuwa na kiingilio ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye.

Yanga ilitumia baadhi ya wachezaji wake wapya ambao imewasajili hivi karibuni, mchezaji Juma Mahadhi alionyesha kandanda safi sana hali itakayowapa tumbo joto wachezaji wanaocheza naye namba moja kama Simon Msuva huku Mzambia, Obrey Chirwa, naye akionyesha alichonacho katika soka.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku timu zote zikionyesha kukamiana, ambapo katika dakika ya tano Mazembe nusura walione lango la Yanga baada ya Adama Traore kupiga krosi safi iliyokua inaelekea langoni mwa Yanga kabla ya kuokolewa kwa kichwa na mshambuliaji, Donald Ngoma.

Yanga walionekana kumiliki mpira vizuri lakini walikosa bao la wazi dakika ya sita, baada ya kipa wa Mazembe, Sylvain Guelassiongnon, kuokoa kirahisi mpira wa adhabu uliopigwa na Kamusoko nje ya 18, adhabu iliyotokana na Ngoma kuangushwa na Chritian Nekadio.

Mambo yalionekana kuwa magumu kwa Mazembe, kwani Yanga walionekana kuwapelekesha ambapo dakika ya 34 Ngoma alikosa tena bao baada ya mpira wa kichwa aliopiga akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Juma Abdul kudakwa na kipa wa Mazembe.

Yanga waliendelea kukosa mabao ya wazi katika kipindi cha kwanza, ambapo katika dakika ya 45 Kaseke na Ngoma walishindwa kuitumia nafasi waliyopata ya kufunga baada ya kuzidiwa maarifa na beki wa Mazembe aliyeokoa hatari hiyo.

Kipindi cha kwanza kilimalizika huku kukiwa hakuna timu iliyobahatika kuliona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, pia kila timu ikionekana kutaka kupata bao la mapema, lakini milango ilikua migumu.

Dakika ya 60 mshambuliaji, Jean Kilitsho, alishindwa kuifungia bao Mazembe, baada ya kupiga shuti hafifu lililotoka nje.

Mbuyu Twite alipewa kadi ya njano dakika ya 60, baada ya kumfanyia madhambi Roger Assale, huku dakika ya 69, Yanga walimtoa Mahadhi aliyeumia na kushindwa kurejea na nafasi yake kuchukuliwa na Geofrey.

Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm, dakika ya 71 alimpumzisha mchezaji, Chirwa ambaye aliichezea Yanga kwa mara ya kwanza jana na nafasi yake kuingia, Matheo Anthony.

Dakika ya 72, Yondani alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Mazembe, Mtanzania Thomas Ulimwengu.

Bope dakika ya 73 alifanikiwa kuandika bao la kuongoza kwa Mazembe, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Yanga kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa nje kidogo ya 18.

Bao hilo liliamsha ari kwa Mazembe, ambao walionekana kushambulia kwa kasi lango la Yanga ambapo kila mara walikuwa wanalichungulia.

Ulimwengu nusura aandike bao la pili dakika ya 84, baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga lakini shuti alilopiga lilipaa juu ya lango na baadaye dakika ya 89 mchezaji huyo alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu, Yondani.

Yanga: Deogratius Munishi, Deus Kaseke, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Obrey Chirwa, Haruna Niyonzima, Voncent Bossou, Donald Ngoma, Juma Abdul, Thaban Kamusoko na Juma Mahadhi .

TP Mazembe: Sylvain Guelassiongnon, Jean Kilitsho, Isama Mpeko, Salif Coulibaly, Roger Assale, Adama Traore, Merveille Bope, Nathan Sinkala, Koffi Kouame, Christian Nekadio na Thomas Ulimwengu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles