Na MWANDISHI WETU-NAIROBI, KENYA
UMOJA wa Afrika (AU) kupitia Taasisi ya Uongozi wa Umoja huo (AULA), umeandaa mdahalo utakaofanyika leo ukishindanisha wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Afrika.
Balozi Amina Mohamed ambaye anapigiwa upatu na Serikali yake ya Kenya, atakuwa sehemu ya mdahalo huo wa kihistoria.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Kenya, pamoja na mambo mengine anatarajia kueleza vipaumbele vyake kwa Afrika.
Vipaumbele hivyo, vitajikita kwa vijana wa Afrika, utekelezaji wa Ajenda ya Afrika 2063, usawa wa kijinsia, maendeleo ya biashara, amani na usalama.
Mdahalo huo utaonyeshwa moja kwa moja kupitia mtandao wa www.au.int na pia utatangazwa katika mashirika mbalimbali ya kitaifa ya habari barani Afrika.
Utafanyika chini ya maudhui ya “Midahalo ya Uongozi Afrika” ukifahamika kama “MjadalaAfrika”, ambao ni jukwaa kwa wadau wakuu katika maeneo mbalimbali ya jamii.
Wadau hao hukutana na kujadili fursa mbalimbali ambazo zinaweza kuhakikisha Afrika inafikia malengo yake kwa mtanganamo na maendeleo endelevu na kulifanya kuwa bara lenye kushiriki kikamilifu katika jukwaa la kimataifa.