Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Utafiti uliofanywa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) umebaini kuwa wenzi wengi wanaoingia katika ndoa hawana elimu kuhusu ndoa.
Kutokana na changamoto hiyo, BAKWATA itaanza kutoa elimu katika mikoa mbalimbali nchini ili kusaidia jamii kujua kuwa ndoa inataka nini.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 27,2024 jijini Dodoma na Naibu Kadhi Mkuu, Sheikh Ali Ngeruko, alipokuwa akizungumza katika mahafali ya Batch 7 ya Kitaifa ya ‘Bakwata Online Akademy’ BOA ambayo pia yamehudhuria na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubery na viongozi wengine.
Sheikh Ngeruko ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa amesema walifikia hatua ya kufanya utafiti huo baada ya wanandoa wengi kufika ofisini kwake kwa lengo la kutaka kuvunja ndoakutokana na sababu mbalimbali.
Amesema baada ya kuona ongezeko hilo, walifanya utafiti na kugundua wengi wanaoingia katika ndoa hawana elimu ya ndoa.
“Tuliingia mtaani tukafanya utafiti tukagundua tatizo kubwa ni elimu ya ndoa. Mke unatakiwa kumpiga mume wako chumbani lakini ukitoka chumbani piga magoti kwenye kila unachofanya.
“Bwanaharusi na bibi harusi kuta nne za chumbani ndiyo haki yenu pale mfanyiane kila kitu, wengi hawajui kuenziana na kudekeana,” amesema Sheikh Ngeruko.
Wengine waliohudhuria mahafali hayo ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Masheikh wa Mikoa wakiongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri.