KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imetoa ofa ya mwezi mmoja kwa abiria watakaosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kwa kulipa nauli ya Sh 160,000 kwa safari moja.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Ofisa Mawasiliano wa ATCL, Lily Fungamtama alisema ndege za kampuni hiyo zimeanza kutoa huduma kuanzia Oktoba 15, mwaka huu.
“Safari hizo zilianza kwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwenda Comoro na hapa nchini zipo katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kigoma,” alisema Lily.
Alisema yalianza mazoezi ya vitendo kwa marubani na wafanyakazi wa ndani ya ndege na hatimaye zilianza safari za biashara ya kusafirisha abiria Oktoba 15, mwaka huu.
Alisema ATCL imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa kwa kuwapatia wateja wake ofa ya kubeba kilo 20 za mizigo na kilo saba za mzigo wa mkononi bure na kutoa vinywaji na ubadilishaji wa tiketi ni bure ndani ya mwezi.
Pamoja na hali hiyo alitoa ufafanuzi kwa kile kilichodaiwa kukwama kwa safari na kusema hakuna na ratiba inakwenda kama ilivyopangwa.
ATCL kwa sasa ina ndege tatu zikiwamo mbili aina ya Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na Dash8-Q300 moja yenye uwezo wa kubeba abiria 50.