LONDON, England
HATA kabla ya mchezo wao dhidi ya Koln ya Bundesliga, Arsenal ilikuwa imeshatinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Europa baada ya kuwa na pointi 10, ambazo zisingeweza kufikia na FK Crvena zvezda, FC BATE Borisov, wala Wajerumani hao.
Gunners, ambao wanashiriki michuano hiyo msimu huu baada ya kuikosa ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wameonekana kuwa moto, wakiwa hawajafungwa hata mchezo mmoja, wakishinda mitatu na kutoa sare moja.
Hata hivyo, baada ya raundi ya tano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, kuna baadhi ya timu ambazo huenda zikatua Europa na kuwa changamoto kubwa kwa vijana hao wa mzee Arsene Wenger.
Basel/ Moscow
Ni ngumu CSKA kuepuka kwenda Europa kwani katika nafasi ya tatu waliyopo kwa pointi tisa, sawa na Basel walio nafasi ya pili, watatakiwa waifunge Man United katika mchezo unaofuata wa Old Trafford.
Pia, waombe Basel wafungwe na Benfica ambayo hata hivyo haijashida hata mchezo mmoja kati ya mitano iliyopita. Kama Basel itashinda na CSKA kuchapwa au kutoa sare na Man United, basi Waswiz (Basel) watatinga 16 bora na kuwaacha Warusi wakienda Europa.
Celtic/Anderlecht
Nafasi pekee iliyobaki kwa timu hizo ni Europa. Katika Kundi B, PSG wenye pointi 15 na Bayern Munich (12) zimeshafuzu.
Ili kufuzu Europa, katika mchezo wa mwisho utakaozikutanisha timu hizo, Anderletch ambao hawana pointi watatakiwa kushinda zaidi ya mabao 3-0 ili kuipiku Celtic yenye pointi tatu na mabao matatu.
Atletico Madrid
Katika Kundi D, Atletico inashika nafasi ya tatu, ikiwa na pointi sita, huku Roma ikiwa ya pili (8) na Chelsea ikiongoza kundi kwa pointi 10.
Atletico watatua Europa kwani katika mchezo wa mwisho Roma watakuwa nyumbani kucheza na FK Qarabag na ni wazi watashinda na kufikisha pointi 11.
Je, Atletico wataweza kuichapa Chelsea na Qarabag waifunge Roma ili Wahispania hao wafuzu 16 bora? Ni wazi itakuwa ngumu.
Juve/Lisbon
Kati ya Juventus na Sporting Lisbon lazima moja itatue Europa. Juve yenye pointi nane haitakwenda Europa iwapo tu itaifunga Olympiakos inayoburuza mkia.
Lakini, kama Juve watakaziwa na Wagiriki hao na Lisbon ikaichapa Barca, ni wazi kuwa wababe hao wa Serie A watawafuata Arsenal Europa.
Sevilla/ Spartak
Liverpool haipo peke yake kwenye uwezekano wa kufuzu, kwani Sevilla, ambao wanakamata nafasi ya pili na pointi zao nane, nao watafuzu kama wataifunga Maribor na Liver wakaifunga au kutoa sare na Spartak Moscow.
Iwapo Sevilla watafungwa na Maribor, halafu Spartak wakaifunga Liver, moja kwa moja Spartak atatinga 16 bora na Liver huku Sevilla ikielekea Europa.
Shakhtar/ Napoli
Shaktar wenye pointi tisa, watasonga mbele hatua ya 16 Ligi ya Mabingwa Ulaya iwapo tu wataepuka kichapo dhidi ya Man City inayoongoza kundi kwa alama 15.
Shida ipo kwa Napoli kwani, wakali hao wa Serie A wenye pointi sita hadi sasa, wana matumaini ya kusikia Shaktar akibamizwa (kitu kinachowezekana) halafu wao washinde dhidi ya vibonde Feyenoord ambao hawana hata pointi moja ili wakwepe balaa la kwenda Europa.
Porto
Porto ina pointi saba kwenye Kundi G na mchezo wao wa mwisho watavaana na Monaco wakiwa na pointi mbili. Porto watakwenda Ligi ya Europa kukutana na Arsenal endapo watafungwa na Monaco na kisha Leipzig wakapata sare dhidi ya Besiktas.
Dortmund/Apoel
Baada ya kuikosa 16 bora ya Ligi ya Mabingwa, sare dhidi ya Madrid wanaoshika nafasi ya pili itaipeleka Dortmund Ligi ya Europa. Lakini, waombe APOEL wafungwe na Tottenham.