Na BENJAMIN MASESE |
SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kushughulikia haraka malalamiko ya wafanyabiashara wadogo (machinga) wanaonyang’anywa bidhaa zao wilayani Sengerema,imeelezwa kuwa watalipwa fidia leo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo Agosti 18, mwaka huu baada ya kupita Wilaya ya Sengerema akienda Wilaya ya Chato kwa ajili ya mapumuziko.
Alisimama kuwasalimia wananchi ndipo wamachinga walipomweleza jinsi walivyonyang’anywa bidhaa zao.
Mmoja wa machinga hao, Jocob Mlinga alisema Agosti 10, mwaka huu ilifanyika operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara wadogo ambako wote waliokuwa wamepanga bidhaa zao kandokando ya barabara walinyang’anywa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, juzi alipiga kambi wilayani Serengerema kwa lengo la kutekeleza agizo la Rais Magufuli ambako ilibainika wafanyabiashara 11 wa mananasi walichukuliwa bidhaa zao.
Mongela alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Magesa Boniface kuwalipa fidia machinga hao 11 leo.
Pia alimwagiza kulifanyia marekebisho soko lililipo karibu na eneo wanalouzia mananasi kwa kujenga mabanda ya nguzo za mabomba yatakayoezekwa kwa mabati kuwatengenezea kivuli.
Alisema baada ya hapo wafanyabiashara hao washirikishwe katika kupanga na kuhamia katika eneo hilo.
“Kuanzia leo Jumatatu (juzi) nakuagiza wewe mkurugenzi kwa kusaidiana na Mkuu wa Wilaya, Emmanuel Kipole anzeni kuandaa utaratibu wa kuwalipa fidia wale waliochukuliwa mananasu yao.
“Ifikapo Agosti 22, hatua hiyo iwe imekamilika, kila mmoja atasema kiasi cha matunda yaliyochukuliwa.
“Rais Magufuli ameagiza nishughulikie tatizo hilo na kupata suluhu, sasa nami nakuagiza kuwalipa fidia na kuwaboreshea soko ili wahamie pale.
“Baada ya hapo hatutaki tena kuwaona kandakando ya barabara,”alisema Mongela.
RC vilevile alimwelekeza mkurugenzi kuwa maofisa maendeleo ya jamii watumike kwenda kwenye jamii kuwaelewesha wananchi kuhusu umuhimu wa masuala mbalimbali yenye tija na si watu wa mapato ambao kazi yao ni kukusanya mapato.
Mmmoja wa wamachinga, Jacob Mlinga alimweleza Mongela kwamba alichukuliwa mananasi yake 700 yaliyokuwa kwenye matoroli mawili.
Mfanyabiashara mwingine, Elina Taibu anayejishughukisha na biashara ya urembo alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge na kuomba kuendelea kuwatetea na kushughulikia matatizo ya watu wa chini.