25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

AELEZA MTUHUMIWA ALIVYOTAKA KUMFANYIA MWANAFUNZI MTIHANI

 

FARAJA MASINDE Na KASANDRA HASSAN (TUDARCO)

-DAR ES SALAAAM

SHAHIDI wa pili katika kesi ya kufanya udanganyifu kwenye mtihani wa kidato cha nne, inayomkabili Miraji Miraji (19), ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala namna alivyombaini mtuhumiwa huyo kuwa siye aliyestahili kufanya mtihani huo.

Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Juma Hassan kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Grace Mwanga, shahidi huyo, Jackline Michael, ambaye alikuwa msimamizi katika kituo cha mitihani hiyo kilichokuwa Shule ya Sekondari Lilisia, Manispaa ya Ilala, alisema baada ya kupata wasiwasi juu ya picha iliyokuwa kwenye fomu na mtu aliye kwenye chumba cha mtihani, aliwasiliana na wakubwa wake ambao walimpa maelezo.

“Siku ya tukio ambayo ndiyo mitihani ilikuwa inaanza Novemba 1, 2016 mara baada ya kuripoti kwa mkuu wa kituo, nikiwa shule husika niliyopangiwa kusimamia wanafunzi wa kujitegemea (Private Candidate), muda ulipofika nilianza kwa kuita majina ya wanafunzi wote waliostahili kuingia kwenye chumba cha mtihani.

“Zoezi lililofuatia lilikuwa ni la kukagua picha kwa kuongozwa na fomu yangu iliyokuwa imechapishwa picha na majina ya wanafunzi husika niliopaswa kuwasimamia (Photo entry form),” alisema Jackline.

Aliendelea kuiambia mahakama hiyo kuwa baada ya kukagua picha hizo na sura za wanafunzi waliokuwa kwenye chumba hicho, alibaini kuwa mtahiniwa mwenye namba P. 38390-0039 alikuwa hafanani na picha iliyokuwa kwenye fomu hiyo.

“Nilimuuliza ‘mbona hii picha kwenye fomu siyo yako?’ Akajibu kuwa huenda Baraza la Mitihani (Necta) wamechanganya, baada ya hapo niliomba askari aniitie msimamizi mkuu wa kituo, ambaye yeye alikuwa akisimamia wanafunzi wa kidato cha nne.

“Baada ya kumtaarifu aliwasiliana na Ofisa Elimu Wilaya ambaye alielekeza kuwa mtahiniwa huyo aruhusiwe kuendelea na mtihani na asitoke nje ya chumba hicho pindi atakapomaliza mtihani wake.

“Baada ya kukamilika kwa mtihani wa siku hiyo, mtuhumiwa alifuatwa na kupelekwa mahala alipokuwa Ofisa Elimu na viongozi wengine kwa ajili ya mahojiano zaidi juu ya kwa nini aliyestahili kufanya mtihani huo hakuwapo na badala yake alikuwapo mtuhumiwa huyo,” alisema Jackline.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Miraji ambaye ni mkazi wa Ubungo, anakabiliwa na mashtaka matatu. Katika shtaka la kwanza inadaiwa kuwa katika tarehe isiyofahamika, 2016 akiwa Ukonga alikula njama na kufoji picha ya utambulisho (Pasipoti) ya kuhitimu mtihani wa elimu ya sekondari mwaka 2016.

Katika shtaka hilo Miraji anadaiwa kubadilisha picha halisi ya Emmanuel Hungo, iliyokuwa imesajiliwa kwa namba P. 3890-0039 na Necta ambapo alii-‘scan’ picha yake na kisha kuiziba picha halisi kuonyesha kwamba fomu hiyo ilikuwa imekosewa jambo ambalo si kweli.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa Novemba 11, 2016 Shule ya Sekondari Lilisia iliyoko ndani ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alifoji picha hiyo kwa kuonyesha kwamba alikuwa ni miongoni mwa watahiniwa waliopitishwa na Necta kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari kuanzi Novemba 1, 2016 akiwa na namba P. 3890-0039 jambo ambalo si kweli.

Na katika shtaka la tatu, Novemba 1, 2016 katika Shule ya Sekondari Lilisia, ndani ya Manispaa ya Ilala, alidanganya kwa kujitambulisha kwa msimamizi wa mitihani ambaye ni Jackline Michael, kuwa yeye ndiye Emmanuel Huago, aliyesajiliwa na Necta kwa namba P 3890-0039 jambo ambalo si kweli.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Agosti 22, mwaka huu kwa ushahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles