29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

MATATIZO YA PEMBEJEO YATATULIWE MAPEMA

Ni ukweli usiopingika kwamba kilimo nchini ndiyo uti wa mgongo wa uchumi na maendeleo yake.  Hiyo ni kwa kuzingatia kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa taifa hili wanategemea kilimo kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.

Vilevile, mazao ya kilimo ndiyo, kwa miaka nenda miaka rudi, yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa katika kuliingizia taifa fedha zikiwamo za kigeni.

Pia kwa miaka mingi imekuwapo mipango na miradi mbalimbali yenye lengo la kuimarisha  na kukuza kilimo kwa kuweka mbinu kadha wa kadha zikiwamo za kuwasaidia wakulima moja kwa moja.

Lakini pamoja na juhudi hizo, baadhi ya watendaji wamekuwa wakitumia fursa walizo nazo kufifisha maendeleo ya kilimo kwa kujinufaisha wenyewe.

Ndiyo sababu tunaunga mkono agizo la Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan la kuiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha  wanaohusika na madeni ya pembejeo za kilimo kufikishwa katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).

Kwa mujibu wa Samia, uhakiki wa madeni ya wazabuni wa pembejeo uliofanywa na serikali umebaini kuwapo unyonyaji mkubwa kwa wakulima, hali ambayo inachangia kuwadhoofisha.

Inadaiwa kuwa katika  baadhi ya maeneo uhakiki unaonyesha wakulima wametumia kiasi kikubwa cha pembejeo wakati si kweli.

Kilichopo ni kwamba baadhi ya watendaji hula njama na wazabuni wa pembejeo na kuandika takwimu za uongo kuonyesha wakulima wa eneo fulani wametumia pembejeo za mamilioni ya fedha, wakati ni pembejeo hewa huku fedha zikiwa zimeingia mifukoni mwao!

Udanganyifu huo na mwingine unaofanywa dhidi ya wakulima na taifa kwa ujumla ni hujuma kubwa kwa taifa kwa ujumla.

Hayo yamekuwa yakifanyika, wakati mwingine kwa kuwarubuni wakulima au kutokana na wakulima kutokuwa na uelewa mzuri kuhusu mfumo wa kupatiwa pembejeo za kilimo.

Yote hayo hufanywa kwa makusudi na watendaji wasiokuwa waaminifu kwa kushirikiana wazabuni wasiokuwa waaminifu.

Wakulima wanakatishwa tamaa na wanashindwa kuinuka na kufikia maisha mazuri wakati taifa nalo linapoteza mamilioni ya fedha kwa sababu ya watu wachache wenye uchu wa utajiri wa haraka haraka.

Ni hali ambayo inapaswa kurekebishwa haraka kwa manufaa na maendeleo ya taifa na watu wake.

Vyombo  vya dola vinavyohusika, Takukuru, polisi na vingine vichukue hatua madhubuti na zisizotetereka kulikabili suala hilo mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles