Na LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM
CHAMA cha ACT Wazalendo, kimetoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kulinda uchumi wa nchi wakati huu ambao taifa likiwa linapambanana virusi vya corona (COVID19), ikiwa ni pamoja na kufunga baadhi ya miji na kulipa wananchi watakaokuwa karantini Sh 300,000 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana, wamependekeza nusu ya akiba ya fedha za kigeni itumike kuwalipa wananchi ili waweze kujikimu wakati nchi imefungwa.
Walisema iwapo Tanzania Bara itakuwa kwenye karantini kila kaya inaweza kulipwa Sh 300,000 kila mwezi kwa miezi miwili ambapo zitatumika dola za Marekani bilioni 2.3 kati ya dola bilioni 5.5 za fedha za kigeni zilizopo.
“Kama nchi tunaweza kumudu gharama za miji inayopendekezwa. Tunapendekeza kuwa wakazi wa Mwanza, Dar es Salaam, Arusha na Dodoma walipwe Shs 300,000 kwa mwezi ambao miji yao itakuwa kwenye lockdown.
“Malipo haya hayatawahusu watu waliopo kwenye ajira rasmi. Sekta binafsi ya Tanzania imeumizwa sana na mlipuko wa corona na hivyo haitakuwa na uwezo wa kulipa wafanyakazi wake. Tunapendekeza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Mei hadi Agosti, wafanyakazi wote kwenye sekta rasmi walipwe mishahara yao kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii kama fao la kukosa ajira.
“Hii itawezesha makampuni kuondokewa na gharama kubwa za uendeshaji na kuwekeza katika afya na kuinuka baada ya corona kuondoka nchini. Pia hii itawezesha wafanyakazi kutofukuzwa kazi,” ilisema taarifa ya chama hichi.
Pia ilipendekeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ielekeze benki zote nchini ambazo zimekopesha watu mikopo binafsi ziache kukusanya marejesho ya mikopo hiyo kwa miezi mitatu kuanzia Aprili na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) isikusanye kodi ya makampun kwa makampuni ya utalii hadi Oktoba mwaka huu.
Kwa upabde wa Zanzibar walipendekeza eneo lote lifungwe kwa muda wa mwezi mzima isipokuwa shughuli muhimu tu kama vile hospitali, ulinzi na usalama na shughuli za kiserikali zisizoepukika ndizo ziendelee.
“Shuhguli za masoko ya bidhaa za wananchi kutumia ziwekewe ratiba maalumu chini ya usimamizi wa Serikali kuruhusu wananchi kununua chakula na Serikali itoe msaada kwa wananchi wakati wa lockdown.
“Kila Kaya Zanzibar ilipwe Sh 300,000 kutoka mgawo wa Zanzibar katika akiba ya fedha za kigeni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na idadi ya watu Zanzibar na wastani wa idadi ya kaya Serikali itatumia Sh bilioni 128 tu, ambazo ni kiwango kidogo kulinganisha na akiba iliyopo ya Dola za Marekani milioni 550.
“Wafanyakazi wote wanaochangia kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) walipwe mshahara wao wa miezi mitatu kutoka mfuko huo. Hii itasaidia kampuni kuepuka gharama kubwa za uendeshaji na hivyo kutopunguza wafanyakazi,”ilisema taarifa hiyo.
Pia kilipendekeza marejesho ya mikopo ya watu binafsi kwenye mabenki yasimame kwa miezi mitatu na Mamlaka ya Mapato na Bodi ya Mapato Zanzibar isikusanye kodi ya mapato hadi Oktoba Mosi mwaka huu.
Kupitia taarifa hiyo chama hicho pia kimependekeza kupunguza msongamano magerezani kwa kuwapa dhamana watu wote wenye makosa yenye dhamana, ambao kesi zao upelelezi bado unaendelea, kuwaachia huru watu wote wenye umri unaozidi miaka 65, wanawake wenye watoto na wenye watoto wadogo magerezani.
Pia kimependekeza hospitali binafsi zenye uwezo kuwa sehemu ya karantini kuepusha kuelemewa kwa vituo vya umma na kwamba wako watu wenye uwezo ambao wako tayari kulipia kukaa hospitali wanazozipenda wao endapo watapata ugonjwa huo.
Ilieleza kuwa kwa hatua walizopendekeza zitaathiri watu wasio na ajira rasmi ambao ndio wengi nchini wanapendekeza Serikali ichukue hatua ya kuwalipa watu wote ambao hawamo kwenye ajira rasmi ili waweze kuendelea na maisha kwa muda huo wa kuwafungia ndani.
Uchumi
Kwa upande wa Tanzania Bara, taarifa hiyo ilieleza kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilitoa uchambuzi wa hali ya uchumi ya mataifa ya Afrika kulingana na janga la COVID 19 na shirika hilo linakadiria kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania itashuka kutoka asilimia 6.3 hadi asilimia mbili mwaka 2020.
Ilisema kasi hiyo ni kubwa ya kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi na kwamba uchumi wa Tanzania Bara unategemea zaidi huduma ikiwamo utalii kwa asilimia 44 ikifuatiwa na viwanda na kilimo kinachochangia kwenye Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 32.
“Hata hivyo sekta ya utalii peke yake inachangia asilimia 26 ya mapato yote ya fedha za kigeni zinazoingia nchini ambapo mwezi unaoishia Machi 2020 jumla ya Dola za Marekani biliini 2.6 ziliingia nchini kutokana na utalii kati ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 10 zilioingia nchini.
“Ni Dhahiri kuwa sekta ya utalii ndio imevurugwa zaidi na COVID 19. Hata hivyo sekta nyengine pia zitadidimia. Tayari tumeona kuwa usafiri wa anga umesimama haswa kwa safari za kutoka nje na hivyo kuathiri mnyororo mzima wa thamani unaofungaminishwa na usafiri wa anga.
“Uzalishaji viwandani pia utaathiriwa kutokana na kuanguka kwa soko la walaji nchini. Serikali ya Tanzania pia haijachukua hatua zozote iwe za kikodi, kifedha au sera za fedha za nje,” ilieleza taarifa hiyo.