NA SHOMARI BINDA-MUSOMA
Uongozi wa Mgodi wa Acacia North Mara, uliopo Tarime mkoani Mara umekubali kulipa mishahara ya wachezaji wa timu ya Biashara United ya Mara ili kuongeza morali kwa wachezaji na mchezo wa soka nchini.
Meneja wa timu hiyo, Aman Josiah, amesema kupatikana mishahara kwa wachezaji kwa wakati ni jambo jema na imani yake mgodi huo utawasaidia kwenye eneo hilo.
Aman amesema uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na uongozi wa timu umekuwa ukijituma kutafuta mafanikio ya timu hiyo na kuwashukuru kwa namna wanavyojitoa kusaidia.
“Nishukuru sana kwa jitihada zinazofanywa kwa pamoja na uongozi wa timu, mkoa na wanachama kwa ujumla, hizi ni taarifa njema sana kwama mishahara ya wachezaji kuanzia Novemba hadi Januari italipwa itatusaidia sana benchi la ufundi kwa sababu wachezaji watapata utulivu,
“Lakini pia timu bado inahitaji mahitaji mengi ikiwemo ya kambi, maandalizi ya mchezo na usafiri hivyo tunawaomba wadau wengine wasaidie,” amesema Aman.
Timu ya Biashara United hadi sasa ina pointi tisa imeshuka  dimbani mara 12 kesho inatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Tanzania Prison kwenye Uwanja wa Karume.