26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kenya: Hatujazuia safari za ndege za Tanzania

Na MASHIRIKA YA HABARI

KENYA imesema haijapiga marufuku safari za ndege kutoka nchi yoyote kutua kwenye ardhi yake.

Kauli hiyo ya Kenya imekuja baada ya Tanzania kuchukua uamuzi kama ule uliotangazwa kuchukuliwa na nchi hiyo juzi kwa kusimamisha Shirika la ndege la Kenya(KQ) kufanya safari zake nchini kuanzia jana Agosti 1.

Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa likiwamo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na vyombo vya habari ya Kenya juzi zilieleza kuwa Serikali ya Kenya ilitangaza kufungua anga lake kwa nchi 11 tu huku baadhi ya nchi jirani ikiwemo Tanzania ikiwa haipo kwenye orodha hiyo.

Hatua hiyo ilionekana kujibiwa na Tanzania ambayo kupitia barua kwa KQ iliyoachapishwa Ijumaa  Julai 31 iliyoandikwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari nayo ilizuia safari za Shirika hilo la ndege la Kenya.

Johari ambaye jana alipotafutwa na gazeti hili alisema yupo kwenye kikao lakini alilithibitishia gazeti hili kuwa barua hiyo ni ya TCAA.

Barua hiyo inaeleza kuwa; Serikali ya Tanzania iliamua kusimamisha safari za KQ kati ya Nairobi na viwanja vya Tanzania kama Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar hadi itakapotangazwa tena.

Saa chache baada ya barua hiyo ya TCAA kwa KQ, Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Macharia akizungumza katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta baada ya nchi hiyo kufungua anga lake kwa ndege za kimataifa, alisema ndege za Tanzania hazijapigwa marufuku.

“Hatujapiga marufuku nchi yoyote kuingia Kenya. Hatujafunga anga letu, kile tulichofanya ni kuweka hatua ya karantini kwa baadhi ya nchi kulingana na tathmini ya janga hilo,” alisema Macharia.

Macharia amesema kuwa amezungumza na Waziri mwenzake wa Tanzania, Isack Kamwelwe kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili na kuwa agizo la Tanzania litapitiwa tena hivi karibuni.

“Kenya haijapiga marufuku ndege kutoka Tanzania. Kenya haijapiga marufuku wasafiri kutoka Tanzania. Tulichofanya ni kuweka kanuni fulani za kiafya watu watakapowasili kutoka nchi mbalimbali,” alisema Macharia.

Aliongeza kuwa ndege za Kenya zitaruhusiwa kuingia katika anga la Tanzania baada ya kufikiwa kwa makubaliano.

Aidha, Macharia aliongeza kuwa orodha ya nchi 19 bado inapitiwa na itaendelea kubadilika kulingana na vile nchi zitakavyoendelea kukabiliana na usambaaji wa ugonjwa wa virusi vya corona katika maeneo ya mipakani.

Awali, Tanzania ilipiga marufuku Shirika la ndege la Kenya Airways kufanya safiri nchini humo kwa usiojulikana.

Awali katika barua yake TCAA ilieleza kwamba; “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebaini kupitia vyombo vya habari kutengwa kwake katika orodha ya nchi ambazo watu wao wataruhusiwa kusafiri kwenda Kenya kuanzia Agosti 1, mwaka tarehe ambayo Jamhuri ya Kenya itafungua anga lake kwa ndege za abiria za kimataifa za kibiashara baada ya kusimamishwa tangu Machi 25, mwaka huu.

“Mamlaka ya Usafiri wa Anga inasikitika kukujulisha kwamba kulingana na misingi yake ile ile ya kurejesha, Serikali ya Tanzania imeamua kuondoa idhini kwa ndege za Kenya Airways(KQ) kutua kati ya Nairobi na Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar  kuanzia Agosti 1, 2020 hadi pale itakapotangazwa vinginevyo,”  inaeleza barua hiyo na kuongeza;

“Aidha, barua hii pia inaondoa mipango yote ya zamani ambayo ilikuwa inaruhusu ndege za KQ kuingia Tanzania,” 

Juzi Ijumaa Serikali ya Kenya ilitangaza kufungua anga zake kwa safari za ndege za kimataifa baina ya Kenya na nchi mbali mbali zikiwemo nchi jirani za Ethiopia, Uganda na Rwanda isipokuwa Tanzania.

Itakumbukwa Tanzania na Kenya zimekuwa katika mvutano tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona ambapo Mei, mwaka huu nchi hizo zilifungiana mipaka kwa muda mfupi kwa madai ya kuambukizana virusi vya corona. 

Hatua hiyo ilizorotesha  usafiri wa mizigo baina ya nchi hizo kwa wiki kadhaa hadi pale zilipokubaliana kuhusu utaratibu wa kupima madereva wa malori ya mizigo.

Safari za ndege za kimataifa zilikuwa zimepigwa marufuku tangu Machi mwaka huu wakati maambukizi ya virusi vya corona yalipoanza kushuhudiwa nchini humo.

Juzi Macharia alizitaja nchi ambazo ndege zake zimeruhusiwa kutua nchini Kenya kuwa ni pamoja na China, Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe, Ethiopia, Switzerland, Uganda, Rwanda, Namibia na Morocco.

Alisema,  nchi hizo zimedhibiti janga la Covid- 19 kwa kiasi cha kuridhisha.

“Hizi ndizo nchi zilizo na idadi ndogo ya maambukizi, maambukizi ambayo hayana madhara sana ama idadi ya maambukizi yapungua kwa kasi katika nchi hizo,” alikaririwa waziri huyo  na gazeti moja nchini humo.

Alisema nchi hizo zimepunguza maambukizi ya ugonjwa huo na raia wake wamekuwa wakipata dalili za kawaida za ugonjwa wa mfumo wa upumuaji.

“Tutaendelea kuboresha orodha yetu kwa kutegemea na hali ilivyo na mazingira. Hii ni orodha yetu kwa leo tutaipitia tena kesho na siku zinazokuja.”

“Abiria wote watakaowasili kwa ndege za kimataifa wakiwa na hati zinazoonesha kuwa hawana dalili za Covid-19 na wale waliopima saa 96 kabla ya safari hawatakaa karantini,”’ alisema.

Katika orodha hiyo iliyotolewa na Kenya nchi za Afrika mashariki zilizomo ni Rwanda na Uganda tu.

Julai 27 mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alitoa kauli ambayo haikuilenga Tanzania moja kwa moja kuwa Kenya haifichi idadi ya watu wenye maambukizi ya Covid-19.

“Sisi tuko wazi na tunajua fika kuwa ugonjwa huu upo tofauti na majirani zetu ambao wanauficha ukweli huu,” alisema Rais Kenyatta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles